WAZAZI NA WALEZI WAMESHAURIWA KUFUATILIA NYENDO NA TABIA ZA WATOTO WAO.

Wazazi na walezi wameshauriwa kufuatilia nyendo na tabia za watoto wao ili  wakue katika maadili mema na kuwaepusha na wimbi la udhalilishaji linaloiathiri jamii.

Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar mama Asha Suleiman Iddi alisema hayo katika shughuli ya maghafali ya kwanza ya skuli ya Fat-hi International Community iliopo Shangani  ilioambatana na zoezi la kuwakabidhi vyeti na kuwapongeza wanafunzi  waliomaliza ngazi ya maandalizi  { kg-ii}.

Mama Asha alitumia fursa hiyo kwa kuwashajiisha na kuwasisitiza wazazi kutenga muda wao kwa kuchunguza tabia za watoto wao zitakazowasaidia kugundua mabadiliko yoyote  mabaya yaliyowazunguuka na kwa haraka  kuyapatia ufumbuzi unaostahiki.

Aliwaeleza wazazi na walezi kuwa elimu ina mchango mkubwa katika kujenga mustakabali wa maisha ya watoto. Hivyo kuna kila sababu kwa wazazi kutumia jitihada zao zote katika kuwarithisha elimu watoto wao ambayo itawasaidia katika maisha yao ya baadae.

Mke huyo wa Makamu wa Pili wa Rais aliwapongeza waanzishi  wa skuli binafsi nchini kwa kuunga mkono jitihada za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar  katika kuinua kiwango cha elimu bila ya kujali ukubwa wa gharama wanazozitoa kwa lengo la kuwafinyanga watoto.

Akisoma risala mwalimu wa skuli ya Fat,hi International Community  ndg. Sheha Ngweshani alisema skuli hiyo  imepata mafanikio makubwa kutokana na watoto wanaosoma katika skuli hiyo wana uwezo mzuri wa kusoma, kuandika na kuhesabu sambamba na kuwajenga wanafunzi katika silka na desturi za mzanzibari.

Mwalimu Sheha Ngweshani alimueleza mama Asha kuwa ingawaje yapo mafanikio yaliofikiwa lakini bado inakabiliwa na baadhi ya changamoto ikiwemo kukosekana kwa vifaa kama vile fotokopi na kompyuta vifaa ambavyo vinakwenda sambamba na ulimwengu wa sasa wa sayansi na teknolojia.

Nae naibu katibu mkuu taaluma kutoka Wizara ya elimu na mafunzo ya amali Zanzibar  ndg. Madina Mjaka Mwinyi alisema  ushirikiano unahitajika baina ya wazazi, walezi na walimu katika kuhakikisha watoto wanasoma katika mazingira wezeshi kwani kufanya hivyo ndio njia pekee ya kuwajenga watoto wakiwa katika hatua ya awali.

Alifafanua kwamba Serekali ya Mapinduzi  Zanzibar itaendelea kutoa elimu kuanzia ngazi maandalizi, msingi na sekondari,  hivyo skuli binafsi nazo zina wajibu wa kuunga mkono jitihada hizo.

Katika shughuli hiyo ya maghafali mama asha aliahadi kuchangia vifaa kama vile kopyut na printa ili kutatua miongoni mwa changamoto zinazowakabili wanafunzi wanaosoma katika skuli hiyo ya fat-hi international comuunity.

 

 

 

 

Comments are closed.

error: Content is protected !!