WATAALAMU WA LUGHA YA KISWAHILI ZANZIBAR KUITUMIA LUGHA HIYO ILI KUISAIDIA NCHI KUINGIZA MAPATO

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdalla amewashauri Wataalamu wa L ugha ya Kiswahili Zanzibar kuitumia Lugha hiyo kama bidhaa ya kuisaidia Nchi kuingiza Mapato hasa katika Jumuiya za kikanda Afrika na Duniani kote.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar akifungua Kongamano la Maadhimisho ya miaka 40 ya Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika SADC lililoandaliwa kwa ushirikiano wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Tanzania na cChuo Kikuu cha Taifa SUZA, amesema Kiswahili ni lugha inayokua kwa kasi hivyo Zanzibar ina nafasi nzuri ya kuliteka soko la Jumuiya hiyo kutokana na kuwa na Wataalamu mahiri wa Lugha hiyo.

Amesema Zanzibar ina Wahitimu wengi wa Kiswahili ambao hawana ajira hivyo ni fursa kwao kuchangamkia nafasi hiyo ikizingatiwa kuwa kiswahili ni Lugha ya nne inayozungumzwa katika Jumuiya ya SADC.

Ameliagiza baraza la Kiswahili Zanzibar Bakiza kuchukua Jukumu la kuhakikisha Kiswahili kinakua na kuimarishwa kwa Maslahi ya Nchi.

Aidha Makamu wa Pili amesema Zanzibar pia inaweza kutanua wigo wa kunufaika na kuwepo Jumuiya ya SADC,kuitekeleza kwa vitendo dhana ya Uchumi wa Buluu na imedhihirika kwa Wafanyabiashara wengi wa zanzibar kulitumia Soko la Kongo kusafirisha bidhaa ya Dagaa.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Mh. Simai Mohamed Said ameshauri kuwa na mkakati wa kuangalia ni eneo gani linaloweza kufanya vizuri zaidi katika Jumuiya ya SADC.

Mwakilishi wa Wizara ya Mambo ya nje Balozi Masoud balozi amesema kupitia SADC Zanzibar ijiandae kuibua fursa za kiuchumi na kibiashara huku Makamu Mkuu wa SUZA Dk. Zakia Mohamed Abubakar amesema Kongamano hilo litaendelea kuitambulisha suza kitaaluma kati yavyuo vikuu vilivyomo katika jumuiya ya SADC na kupewa heshima ya kuandaa Kongamano hilo miongoni mwa Vyuo vikuu Tanzania vikiwemo UDOM na Chuo cha Diplomasia.

 

Comments are closed.