Blog

WATUMISHI WA TAASISI ZA UMMA NCHINI KUWA TAYARI KATIKA KUYARIPOTI MATENDO YOTE MAOVU

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewataka  Wananchi pamoja  na watumishi wa taasisi za umma nchini kuwa tayari katika kuyaripoti matendo yote maovu yanayoonekana kwenda kinyume na Maadili ya Taifa.

Amesema wapo baadhi ya Watu wachache wamekuwa wakirejesha nyuma jitihada zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali katika mapambano dhidi ya Rushwa, jambo ambalo linapaswa kushughulikiwa kwa mujibu wa Sheria  na kanuni za Nchi

Akizungumza na Wananchi katika Maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binaadamu katika Kiwanja cha Michezo Gombani Chake Chake Pemba Balozi Seif amesema tatizo la Rushwa katika Jamii na mgongano wa Kimaslahi yanaendelea kuathiri Nchi nyingi Duniani ikiwemo Tanzania.

Balozi Seif alisema  vitendo hivyo hudhoofisha upatikanaji wa Haki za Binaadamu kwa kiwango kikubwa na kurejesha nyuma jitihada za kuimarisha misingi ya Haki na Utawala Bora.

Balozi Seif amesema kupitia   ripoti iliyotolewa Mwaka  2017 inayoangazia mapambano dhidi ya Rushwa inaonyesha Tanzania kuwa ni Nchi ya Pili ndani ya Ukanda wa Afrika Mashariki ikitanguliwa na jirani yake Rwanda katika mapambano dhidi ya Rushwa.

Huku kwa upande wa  Kimataifa Tanzania inashikilia nafasi  ya 103 kutoka nafasi ya 116  dhidi  ya vitendo hivyo ambapo aliwanasihi  Wananchi kushirikiana  na Serikali katika mapambano dhidi ya rushwa  ili kujiwekea nafasi ya kufanya vizuri katika ripoti itakayotolewa .

Pia  balozi seif  aliwanasihi wasimamizi wa Tenda kuwa makini katika kusimamia haki na Uadilifu kwa wanaoomba sambamba na kuepuka kuitia hasara Serikali .

Akisoma Risala Mwenyekiti wa Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma Nd. Assaa Rashid amesema misingi ya Utawala Bora itaimarika zaidi iwapo Jamii itajikita katika kuziba Mianya ya Rushwa na kuongeza Uwajibikaji.

Akimkaribisha Mgeni rasmi kwenye kilele cha Maadhimisho hayo ya Siku ya Maadili na Haki za Bianaadamu Waziri wa Nchi Ofisi yua Rais, Katiba, Sheria ,Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mh. Haroun Ali Suleiman aliwaomba Watendaji wanaosiamamia Suala la Maadili kuwa na Lugha nzuri katika kuuhudumia Umma.

Mapema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliyapokea Maandamano ya Taasisi mbali mbali zinazosimamia Maadili na Haki za binaadamu  pamoja na Wananchi katika kuadhimisha sherehe hizo.

Ujumbe wa Mwaka huu wa Siku ya Maadili na Haki za Binadamu unasema “ Tuimarishe Uadilifu, Uwajibikaji, Haki za Binadamu na Mapambano dhidi ya Rushwa kwa Maendeleo ya Taifa.

 

BARAZA LA MJI CHAKE KUFUATILIA KIWANGO CHA FEDHA KINACHOTOLEWA KATIKA KWARE

Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa Serikali za Mitaa na Idara Maalumu za SMZ Mh. Shamata Shaame Khamis ameliagiza baraza la mji chake chake kufuatilia kiwango cha fedha kinachotolewa katika kware ya Vitongoji ili kujua kuwa  kinakwenda na uhalisia na wananchi wanafaidika vipi katika eneo hayo.

Amesema serikali imeweka mashine za kukusanyia fedha kwa lengo la kudhibiti mapato yasipotee, kwani ndizo zinazotumika  katika utekelezaji wa miradi mbali mbali ya maendeleo kwa wananchi.

Mh. Shamata ametowa agizo hili baada ya kukagua kware ya uchimbaji wa kifusi Vitongoji na kupata maelezo kutoka kwa muwekezaji wa eneo hilo na uongozi wa wilaya na kusisitiza haja ya kuvitafuta vyanzo vipya ili kuongeza kiwango cha ukusanyaji.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Chake Chake Nd. Rashid Hadid Rashid amesema wataendelea kusimamia eneo la kwareni ili kuhakikisha baada ya kuchimbwa linafukiwa ili eneo liweze kutumika katika shughuli za uzalishaji.

Kwa upande wake Nd. Khamis ambae amekodi eneo hilo amelalamika ubovu wa barabara kuwa ni usumbufu kwa madereva wanaokwenda kufuata huduma hiyo.

MKUU WA WILAYA YA KASKAZINI B KUFANYA MKUTANO NA WAKAAZI WA SHEHIYA HIYO NA KUSIKILIZA KERO ZAO

Mkuu wa wilaya ya kaskazini b Nd Rajab Ali Rajab ametoa wiki moja kwa wamiliki wa mashamba ya mpunga  shehiya ya kilombero ambao  wamepanda miembe  katika mashamba  hayo  kuwasilisha hati miliki zao  kwa uongozi wa shehiya hiyo ili serikali ya wilaya iweze kujiridhisha kabla ya kuchukua hatua  zinazostahiki  dhidi  yao.

Amesema kitendo cha baadhi ya watu kuanza kujitokeza na kuwapa vitisho wakulima wa eneo hilo kwa madai ya kuwa eneo hilo ni la kwao  sio jambo zuri kwani serikali imetenga eneo hilo kwa ajili ya kilimo cha mpunga  na si vyenginevyo

Akiwa katika muendelezo wa ziara zake katika shehiya mbalimbali za wilaya hiyo mkuu huyo wa wilaya  kabla ya kufanya mkutano na wakaazi wa shehiya hiyo  na  kusikiliza kero zao  alitembelea shamba linalolalamikiwa na wakulima kuhusu uwepo wa watu kupanda miembe  pamoja na kuwakataza kuchuma embe katika miembe hiyo kwa madai ya kuwa mashamba hayo ni yao  kitendo ambacho sio kweli

Amesema taarifa alizonazo juu ya mashamba hayo ya mpunga ni kuwa mashamba ni mali ya serikali ambayo yalitolewa kwa lengo la kilimo cha mpunga na si kwa ajili ya kupandwa miembe kama baadhi ya watu wanavyofanya  hivi sasa

Akizungumzia kero ya baadhi ya wakulima kuunganisha mipira ya maji kutoka katika kisima kinachosambaza maji katika shehiya hiyo ndugu rajab amesema ni vyema wakulima hao wakachimba visisma katika mashamba yao ili kutoa fursa kwa wakaazi wa kijiji hicho kunufaika na kisima hicho kutokana na kisima kilichopo kutokukidhi mahitaji ya wakaazi hao

Mapema wakiwasilisha kero zao mbele ya mkuu huyo wa wilaya baadhi ya wakaazi  wamesema katika shehiya yao wanatatizo la utoro kwa wanafunzi ambao kwa kiasi kikubwa wamejihusisha na vitendo vya ngono,uwepo wa wizi wa mazao na mifugo,kuvamiwa kwa mashamba yao na kuanza kupandwa miembe pamoja na kutokuridhia kunyang’anywa kwa eneo lao la kilimo katika shamba ya mpira kichwele kwa kupewa muekezaji wa kiwanda cha sukari mahonda ambapo hadi sasa bado hajalitumia kwa shughuli yoyote eneo hilo.

MUONGOZO WA UKAGUZI WA USALAMA NA AFYA KAZINI NI JAMBO LA HESHIMA KATIKA SEKTA YA UTUMISHI WA UMMA.

Mwenyekiti wa kamisheni ya utumishi wa umma Mhe.Balozi Mohammed Fakih amesema muongozo wa ukaguzi wa usalama na afya kazini ni jambo la heshima katika sekta ya utumishi wa umma.

Kauli hiyo ameitoa wakati akifungua  mafunzo ya kujenga uwelewa na kuutangaza muongozo ,wa ukaguzi wa usalama na afya kazini katika utumishi wa umma, yaliyofanyika katika ukumbi wa ofisi ya mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali uliopo maisara wilaya ya mjini.

Balozi Fakih amesema muongozo huo utasaidia kuimarika kwa hali ya usalama na afya kazini na sekta ya umma kutekeleza majukumu yake kuzingatia viwango vya kazi vya kitaifa na sheria za kazi kufikia viwango vya kimataifa..

Akiwasilisha mada ya muongozo wa ukaguzi katika sehemu za kazi  mkurugenzi wa usalama na afya kazini mwalimu Suleiman Ali amesema usalama na afya kazini inajikita zaidi katika kinga ili kuepuka madhara katika sehemu za kazi.

Mapema katibu wa kamisheni ya utumishi wa umma ndugu Mdungi Makame Mdungi amesema umuhimu wa muongozo ni kuhakikisha watumishi wa umma wa umma wanafanya kazi katika mazingira yaliyo salama na kutoweza kuletea madhara ya kiafya.

Mafunzo hayo ya siku moja yamewashirikisha maafisa wa utumishi wa taasisi za serikali