Blog

RAIS DKT. HUSSEIN AKIZUNGUMZA KATIKA KONGAMANO LA UDHALILISHAJI UKUMBI WA SHEIKH IDRISSA ABDUL WAKIL

Rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali haitasita kumchukulia hatua kiongozi ambae atabainika kuhusika na vitendo vya udhalilishaji ndani ya jamii.

Akizungumza katika kongamano la harakati za kutokomeza vitendo vya udhalilishaji katika ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdul-wakil amesema Serikali imekuwa ikitafuta njia mbali mbali kupitia wasimamizi wa sheria kuona inaondosha hali hiyo hivyo itakapobaini kuwepo miongoni mwa watendaji wake wanahusika watashughulikiwa.

Amesema amekuwa akifanya uteuzi kwa kuzingatia utendaji kwa ajili ya kuwafanyiakazi wananchi katika kuwaondolea matatizo yao ikiwemo upatikanaji wa haki hivyo amekuwa akitengua teuzi hizo baada ya kuona wanakwenda kinyume na malengo hayo.

Aidha Dk Mwinyi amesema upo umuhimu wa kujipanga upya katika kushughulikia tatizo la udhalilishaji kutokana na ukubwa wake ambapo watendaji wa vyombo vya kutoa haki wanapaswa kujitathmini juu ya utendaji wao na kuandaa ripoti za hatua wanazochukua ili kuona kunakuwa na mabadiliko.

Ameipongeza Zafela na asasi mbali mbali pamoja na mashirika ya kimataifa ambayo yamekuwa yakitoa fedha nyingi katika kufanikisha mapambano hayo ili kuona jamii inakuwa huru dhidi ya vitendo hivyo.

RAIS WA JAMUHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA MH SAMIA SULUHU HASSAN AMEZINDUA CHANJO YA UVIKO -19.

Hafla ya uzinduzi wa chanjo hiyo imefanyika katika viwanja vya Ikulu Jijini Dar es salaam ambapo viongozi mbalimbali wa vyama na Serikali,viongozi wa dini na wasanii ni miongoni mwa waliojitokeza katika kuchanjwa na chanjo hiyo aina ya Johson&Johnson inayotengenezwa nchini Afrika ya kusini.

Viongozi wengine waliopata chanjo hiyo ni pamoja na Waziri mkuu Kassim Majaliwa, Jaji mkuu wa Tanzania pro. Ibrahimu Juma  na Waziri mkuu mstaafu Mh. Mizengo Pinda wote   wamejitokeza kuungana na Rais katika kupata chanjo hiyo.

Rais Samia amesema chanjo hiyo ni salama kwani yeye ni mama wa watoto wanne na wajukuu na mke lakini pia Rais na Amir Jeshi mkuu amesema asingeweza kujitowa mwenyewe kujipeleka kwenye kifo kwani chanjo hiyo iko salama baada ya watalamu kujiridhisha hivyo atahakikisha kwamba kila Mtanzania anayetaka kuchanjwa atapata chanjo hiyo.

Katika uzinduzi huo Mh. Samia amewataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo ambapo kuna walioathirika na waliopoteza ndugu zao ambao wangefurahia kupata chanjo hiyo mapema.

WAKAAZI WA ENEO LA MTOPEPO NA MTONI WAMEIOMBA SERIKALI KUWAJENGEA MITARO.

Wakaazi wa eneo la Mtopepo na Mtoni katika Jimbo la Mwera wameiomba Serikali kuwajengea mitaro ya kupitishia maji ya mvua ili kuepusha madhara yaliyowahi kutokea.

Wakitoa malalamiko katika ziara ya Waziri wa nchi afisi ya makamu wa kwanza wa Raisi Dk. Saada Mkuya Salum iliyoandaliwa na Mbunge wa jimbo la Mwera wananchi hao wameeleza ukosefu wa mitaro katika eneo la Mtoni kidatu na Mtopepo ni tatizo ambalo linarudisha nyuma maendeleo yao kwani yanasababisha mafuriko na hata kupoteza maisha ya watoto wao.

Akitoa ufafanuzi juu ya tatizo hilo  Dk. Mkuya amesema atakutana na Waziri wa Idara maalum kujua mipango ya halmashauri katika ujenzi wa mitaro hiyo akiwasisitiza wananchi hao kuwa na subira wakati Serikali ikilitafutia ufumbuzi suala hilo.

Mbunge wa jimbo hilo Mh Zahor Mohamed amesema anaendelea kutafuta njia ya kutatua tatizo hilo na kuwahimiza wananchi kuacha uharibifu wa mazingira kwani baadhi ya maendo yameathiriwa sana na uharibifu huo.

MH MASOUD AMEWATAKA MAAFISA MAPATO KUKUSANYA KODI KWA MASHINE ZA KIELEKTRONIKI.

Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Tawala za mikoa Serikali za Mitaa na Idara maalum za SMZ Mh Masoud Ali Mohamed, amewataka maafisa mapato kukusanya kodi kwa mashine za kielektroniki ili kudhibiti upotevu wa mapato ya Serikali.

Akikabidhi mashine 75 za kukusanyia kodi kwa wakuu wa mikoa mitatu ya Unguja, amesema kwa kipindi kirefu kumekuwa na upotevu wa mapato ya Serikali kutokana na ukusanyaji kodi kwanjia ya mikono, hivyo uwepo wa mashine hizo kutaepusha tatizo hilo.

Wakati huohuo Mh masoud amefungua mafunzo ya mfumo wa usajili wa wajasiriamali wadogo katika Ukumbi wa kikosi cha Valantia Mtoni, na kuwataka Maafisa kodi wa Mabaraza ya miji na manispaa kutoa taarifa kwa Wakuu wa Mikoa wanapokwenda kukusanya kodi katika maeneo yao.