MKUU WA WILAYA YA KASKAZINI B KUFANYA MKUTANO NA WAKAAZI WA SHEHIYA HIYO NA KUSIKILIZA KERO ZAO

Mkuu wa wilaya ya kaskazini b Nd Rajab Ali Rajab ametoa wiki moja kwa wamiliki wa mashamba ya mpunga  shehiya ya kilombero ambao  wamepanda miembe  katika mashamba  hayo  kuwasilisha hati miliki zao  kwa uongozi wa shehiya hiyo ili serikali ya wilaya iweze kujiridhisha kabla ya kuchukua hatua  zinazostahiki  dhidi  yao.

Amesema kitendo cha baadhi ya watu kuanza kujitokeza na kuwapa vitisho wakulima wa eneo hilo kwa madai ya kuwa eneo hilo ni la kwao  sio jambo zuri kwani serikali imetenga eneo hilo kwa ajili ya kilimo cha mpunga  na si vyenginevyo

Akiwa katika muendelezo wa ziara zake katika shehiya mbalimbali za wilaya hiyo mkuu huyo wa wilaya  kabla ya kufanya mkutano na wakaazi wa shehiya hiyo  na  kusikiliza kero zao  alitembelea shamba linalolalamikiwa na wakulima kuhusu uwepo wa watu kupanda miembe  pamoja na kuwakataza kuchuma embe katika miembe hiyo kwa madai ya kuwa mashamba hayo ni yao  kitendo ambacho sio kweli

Amesema taarifa alizonazo juu ya mashamba hayo ya mpunga ni kuwa mashamba ni mali ya serikali ambayo yalitolewa kwa lengo la kilimo cha mpunga na si kwa ajili ya kupandwa miembe kama baadhi ya watu wanavyofanya  hivi sasa

Akizungumzia kero ya baadhi ya wakulima kuunganisha mipira ya maji kutoka katika kisima kinachosambaza maji katika shehiya hiyo ndugu rajab amesema ni vyema wakulima hao wakachimba visisma katika mashamba yao ili kutoa fursa kwa wakaazi wa kijiji hicho kunufaika na kisima hicho kutokana na kisima kilichopo kutokukidhi mahitaji ya wakaazi hao

Mapema wakiwasilisha kero zao mbele ya mkuu huyo wa wilaya baadhi ya wakaazi  wamesema katika shehiya yao wanatatizo la utoro kwa wanafunzi ambao kwa kiasi kikubwa wamejihusisha na vitendo vya ngono,uwepo wa wizi wa mazao na mifugo,kuvamiwa kwa mashamba yao na kuanza kupandwa miembe pamoja na kutokuridhia kunyang’anywa kwa eneo lao la kilimo katika shamba ya mpira kichwele kwa kupewa muekezaji wa kiwanda cha sukari mahonda ambapo hadi sasa bado hajalitumia kwa shughuli yoyote eneo hilo.

No Comments Yet.

Leave a comment

error: Content is protected !!