MH. OTHMAN MASOUD AMEAGIZA KUSITISHA MATUMIZI YA ENEO LA SHEHIA YA KIUNGANI NA BANDAKUU NUNGWI

Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar Mh. Othman Masoud Othman ameiagiza Uongozi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja kusitisha Matumizi ya eneo la shehia ya kiungani na bandakuu nungwi ili kumaliza migogoro ya ardhi iliyopo katika maeneo hayo.

Ametoa Agizo hilo wakati wa ziara ndani ya mkoa huo katika kijiji cha Nungwi iliyokuja kufuatia malalamiko ya wananchi juu ya kutumiwa kwa maeneo hayo bila ya kuzingatia utaratibu.

Mh Othman amesema lengo la Serikali ni kuwaletea maendeleo Wananchi hivyo ni njema kwa Uongozi wa Mkoa kushirikiana na wizara ya Ardhi na wananchikupanga maeneo ya uwekezaji ili kuleta maendeleo ya Nchi.

Mkuu wa Mkoa wa kaskazini Unguja Mh Ayoub Mohamed Mahmoud amesema Mkoa huo una migogoro isiyopungua 150 na tayari 20 imeshatatuliwa huku akiwaomba Viongozi wa juu kuendelea kutembelea maeneo mbali mbali kwa lengo la kupatiwa ufumbuzi matatizo yanayowakabili Wananchi.

Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi nd. Joseph John Kilangi amesema Wizara inaendeleza na utambuzi wa Ardhi katika maeneo hayo ili kuondosha matatizo ya Ardhi yaliyopo ndani ya Mkoa huo.

Wakati huo huo Mh Othman ameendelea na ziara yake kendwa Bondeni katika eneo linalotumika kwa shughuli za Uvuvi na kuwahakikishia Wananchi wa eneo hilo kuwa wataendelea kulitumia eneo hilo hadi serikali itakapoandaa utaratibu wa kuwatafutia eneo rafiki kwa kuendelea na shughuli zao za Maisha.

Comments are closed.