MH. HAROUN AMESHIRIKI KATIKA MAHAFALI YA KUMI NA MBILI YA CHUO CHA UTAWALA WA UMMA IPA

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mh.Haroun Ali Suleiman ameutaka Uongozi wa Chuo cha Utawala wa Umma ,kufanya tathmin ya utendaji kwa  Wanafunzi wanaomaliza Chuoni hapo ili kwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia.

Waziri Haroun ametoa kauli  hiyo katika mahafali ya kumi na mbili ya Chuo cha Utawala wa Umma IPA ,ambapo amesema Serikali imetumia pesa nyingi  kuanzisha Chuo hicho hivyo ni jukumu lao kuhakikisha Taifa linapata Watumishi wenye ujuzi.

Aidha amewataka wahitimu waliokuwemo katika Utumishi wa Umma kutumia vyema Taaluma waliyoipata katika kufanya kazi kuleta mabadiliko chanya wakati wa kurudi kazini, na kuacha tabia ya kutekeleza majukumu yao kimazowea.

Mkurugenzi wa Chuo cha Utawala wa Umma Dr.Mwinyi Talib amesema licha ya mafanikio  mbali mbali yaliyo patikana  katika utoaji wa taalum bado chuo kinakabiliwa  changamoto ikiwemo uhaba wa Ofisi na Vyumba vya Kusomea .

Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Fatma Said amesema Chuo cha Utawala wa Umma kinaendelea kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo  watumishi wa umma ili kuendana na mabadiliko ya kiutendaji  na  Baraza la Chuo  linaendelea kushirikiana na Chuo katika utendaji wa kazi zao.

Jumla ya wahitimu 860 wa Cheti na Stashahada wametunukiwa vyeti vyao ambapo kati ya hao Wanawake ni 596 na Wanaume 264.

Comments are closed.