MATUMIZI MAZURI YA ARDHI NA USIMAMIZI BORA WA MAZINGIRA NI MSINGI WA MAENDELEO YA TAIFA

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein amesema kwamba matumizi mazuri ya ardhi na usimamizi bora wa mazingira ni misingi muhimu katika maendeleo ya Taifa lolote duniani.

Rais Dk. Shein aliyasema hayo leo katika Mkutano wa mwaka wa Jumuiya ya Majaji na Mahakimu wa Nchi za Afika Mashariki unaofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Madinat Al Bahr, Mbweni mjini Zanzibar.

Katika maelezo yake Rais Dk. Shein alisema kuwa mkutano huo umekuja wakati muwafaka ambapo changamoto kadhaa zinazohusiana na ardhi pamoja na mazingira zimekuwa zikiibuka katika nchi za Afrika Mashariki.

Alisema kuwa kuongezeka kwa idadi ya watu sambamba na kukua kwa uchumi kumeleta changamoto nyingi katika sekta ya ardhi na mazingira katika nchi hizo na kutolea mfano migogoro ya ardhi ambayo imeikumba miji na vijiji ambayo baadhi ya wakati hujumuisha wananchi na wawekezaji walioekeza katika nchi za Afrika Mashariki.

Aliongeza kuwa iwapo hali hiyo itaendelea itakuwa ni tishio kwa maendeleo ya kiuchumi na usalama kwa nchi za Afrika Mashariki huku akieleza jinsi alivyovutiwa na maudhui ya mwaka huu yasemayo ‘’Ardhi na Mazingira kwa Maendeleo Endelevu ya Afrika Mashariki”.

Rais Dk. Shein alieleza kuvutiwa na maudhui hayo ambayo yamekuja wakati muwafaka ambapo nchi nyingi za Afrika Mashariki zimeweka mikakati ya makusudi katika kuimarisha mazingira na matumizi mazuri ya ardhi.

Alieleza kuwa kutokana na mada zitakazojadiliwa katika mkutano huo wa siku nne ana matumaini makubwa kuwa hatimae mkutano huo utakuja na mbinu pamoja na njia mbadala za kutatua changamoto zilizopo.

Kwa upande wa Zanzibar, Rais Dk. Shein alieleza hatua zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kutatua migogoro ya ardhi huku akisisitiza kuwa Zanzibar ardhi yote ni mali ya Serikali kama ilivyoelezwa katika sheria namba 12 ya mwaka 1992.

Kwa upande wa mazingira, Rais Dk. Shein alieleza changamoto mbali mbali za mazingira zinazosababishwa na shughuli za kibinaadamu pamoja na athari za kimaumbile hasa suala zima la mabadiliko ya tabianchi.

Rais Dk. Shein alieleza haja kwa Jumuiya hiyo ikashirikiana na taasisi mbali mbali za serikali katika masuala ya kimazingira hasa ikizingatiwa kwamba uchumi wa nchi za Afrika Mashariki unaendelea kukua katika sekta nyengine mpya ikiwemo sekta ya mafuta na gesi ambayo imethibikika kwamba imekuwa ikileta changamoto nyingi za mazingira katika nchi za Afrika pamoja na zile nchi za Mashariki ya Kati.

Pia, alisisitiza kwamba taaluma ya Sheria inahitajika katika kusimamia sekta hizo mpya ili kwenda sambamba na ukuaji wa sekta hizo mpya.

Vile vile aliwahimiza Majaji na Mahakimu kushirikiana na Mihimili ya utungaji sheria ili kuweza kuja na sheria madhubuti katika kuja na sheria ya utalii ambayo vuile vue inaendelea kukua kwa kasi katika nchi wananchama.

Dk. Shein alieleza changamoto ya mazingira Zanzibar hasa katika tatizo la mchanga na athari zake huku akieleza haja ya kuimarisha sheria katika sekta ya utalii.

Katika hotuba yake hiyo, Rais Dk. Shein alifahamisha juhudi zinazochukuliwa na Serikali katika kuimarisha matumizi bora ya ardhi na uhifadhi wa mazingira kwa kutoa mfano semina na viongozi iliyofanywa tarehe 16 mwezi Machi mwaka 2019 iiyowashirikisha Majaji, Mahakimu, Wanasheria pamoja na watendaji wengine wa Serikali ili kupata rai kwa kutafuta mwelekeo na njia mbadala juu ya matumizi bora ya ardhi na mazingira na hatimae kuja na maazimio 28.

Aidha, Rais Dk. Shein alieleza mwelekeo wa Zanzibar katika hatua za ufukiaji wa bahari kwa lengo la kupunguza changamoto zilizopo.

Aliwafahamisha wanasemina hao kwamba Zanzibar suala la ufukiaji wa bahari sio geni na kufahamisha kwamba baadhi ya maeneo ya Mjai Mkongwe yamejenwga katika ardhi iliyofukiwa karibu karne moja na nusu iliyopita yakiwemo maeneo ya Mji Mkongwe wa Zanzibar hasa katika eneo la Darajani.

Anaamini wkamba jambo hilo linawezekana hivi sasa, alifahamisha kwamba tayari mafanikio yameshaanza kuonekana katika suala la ufukiajai wa ardhi wka kutoa mfano mradi uliofanywa na mwekezaji wa ndani Sheikh Said Salim Bakhresa kupitia Kampuni yake ya SSB ya kufukia bahari na kufanya shughuli za maendeleo katika eneo la Mtoni kwa kujenga hoteli ya kisasa, viwanja vya watoto, michezo ya maji na mambo mengineyo.

Alikipongeza kitendo hicho kilichofanywa na mwekezaji huyo kwa kuonesha matumizi mazuri ya ardhi hapa Zanzibar inayoenda sambamba na maudhui ya mkutano huo.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein aliitaka Jumuiya hiyo kufanya bidii katika kuhakikisha kunafanywa tafsiri ya Sheria kutoka lugha ya Kiingereza na kwenda lugha ya Kiswahili jambo ambalo litawasaidia na kuwarahisishia wananchi katika kupata haki zao za kisheria katika kuzifahamu sheria jambo ambalo ni muhimu katika kutafuta haki zao za kisheria na kuwafanya kuwa raia bora wenye kutii sheria.

Alieleza kuwa ufahamu wa Sheria ni jambo muhimu katika kupata haki kwa wananchi hivyo, Majaji na Mahakimu wana dhima ya kushirikiana na taasisi nyengine za nchi za Afrika Mashariki katika kuiendeleza lugha ya Kiswahili ili lugha hiyo iendelee kukua kwa kasi zaidi na na kutumika katika mikutano mikubwa ya Kimataifa.

Aliwataka Majaji hao wahakikishe kwamba lugha hiyo ina msamiati wa kutoka katika masual ya sheria pamoja na masuala mengine ya kiuchumi, teknolojia na kijamii.

Alisisitiza na kupendekeza kuwa katika mikutano ijayo kukatumika lugha ya Kiswahili huku akieleza haja ya kutumia lugha hiyo na kuhakikisha Kiswahili inakuwa na msamiati wa kutosha katika sheria na masuala mengineyo na kimaendeleo.

Rais Dk. Shein aliipongeza Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania kwa juhudi zake inazozichukua katika kutafsiri Sheria kutoka lugha ya Kiingereza kwenda lugha ya Kiswahili.

Nae Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa Rais Dk. Shein kwa juhudi zake alizozichukua katika kuhakikisha watendaji katika kada ya Sheria wakiwemo Majaji, Mahakimu na Wanasheria wanatizamwa vizuri ikiwa ni pamoja na kuwaongezea mishahara.

Aidha, Jaji Makungu alimpongeza Rais Dk. Shein kwa kuipa ardhi Mahakama Kuu kwa ajili ya Ujenzi wa Mahakama Kuu huko Tunguu, Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja ambapo hapo jana Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilitiliana saini na Kampuni ya “ADVET Constraction Limited kwa ajili ya kuanza ujenzi.

Nao viongozi wengine wa Jumuiya hiyo kutoka nchi za Afrika ya Mashariki akiwemo Rais wa Jumuiya hiyo Jaji Anjeline Rutazama walieleza hatua mbali mbali zinazochukuliwa na Jumuiya hiyo katika kuhakikisha suala zima la sheria linapewa kipaumbele katika sekta zote muhimu ndani ya nchi za Afrika Mashariki.

Aidha, waliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuufadhili mkutano huo kwa asilimia 90 za bajeti ya mkutano huo pamoja na kutoa shukurani kwa Taasisi nyengine ambazo zimewaunga mkono katikia kufanikisha mkutano huo.

Viongozi kadhaa walihudhuria katika Mkutano huo akiwemo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid, Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu, Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Profesa Ibrahim Juma, Majaji, Wanasheria, Majaji Wastaafu, Mahakimu kutoka nchi za Afrika Mashariki , Mawaziri na viongozi wengine.

 

Comments are closed.

error: Content is protected !!