DK.SHEIN AMETOA MKONO WA POLE KWA FAMILIA YA BALOZI MSTAAFU JOB LUSINDE

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, ametoa Mkono wa pole kwa Familia, Ndugu, Jamaa na Marafiki wa Marehemu Balozi Mstaafu job Malecela Lusinde aliyefariki Dunia Jumanne Julai 7, Mwaka huu.

Rais Dk. Shein alifika nyumbani kwa marehemu Balozi Mstaafu Job Lusinde majira ya asubuhi huko katika Mtaa wa Uzunguni Jijini Dodoma mbapo alitoa mkono wa pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki ikiwani pamoja na kumpampole Mjane wa Marehemu Sara Lusinde.

Akitoa mkono wake wa pole Rais Dk. Shein alieleza jinsi alivyoguswa na kifo cha aliyekuwa miongoni mwa Mawaziri 11 wa Kwanza wa Tanganyika ambapo alieleza kuwa kiongozi huyo Mkongwe wa siasa atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa akiwa Waziri, Balozi, Mdhamini wa CCM na kiongozi wa Wazee wa Dodoma.

Aidha, Rais Dk. Shein alipata fursa ya kuuaga mwili wa Marehemu Balozi Lusinde na kutoa heshima ya mwisho akiwa pamoja na ndugu, jamaa, marafiki pamoja na viongozi mbali mbali hapo nyumbani kwake mtaa wa Uzunguni Mjini Dodoma.

 

Mapema Rais Dk. Shein alipofika nyumbani kwa Marehemu alitia saini kitabu cha maombolezi ambapo alitoa pole kwa kifo cha Mzee Balozi Job Lusinde kwa wafiwa wote, ndugu na jamaa huku akimuomba  Mwenyezi Mungu awape subira na aiweke roho ya Marehemu pahala pema.

 

Akitoa neno la shukurani kwa Rais Dk. Shein Waziri Mkuu Mstaafu John Samweli Malecela alimshukuru na kumpongeza Rais Dk. Shein kwa kushiriki kikamilifu katika msiba huo na hatimae kuuaga mwili wa marehemu.

Mwanasiasa huyo mkongwe, Balozi Job Lusinde (90) alikuwa mmoja wa viongozi katika Baraza la Kwanza la Mawaziri la Mwalimu Julius Nyerere baada ya uhuru ambaye alifariki dunia katika Hospitali ya Mloganzila jijini Dar es Salaam.

 

Familia ya Balozi Lusinde na Malecela ilieleza kuwa taratibu za mazishi zinaendelea asubuhi hii na baadae mwili wa marehemu utapelekwa Kanisani kwa ajili ya kuendelea na taratibu nyengine za mazishi. Marehemu Lusinde ni kaka wa Waziri Mkuu wa zamani wa Tanzania, John Samweli Malecela.

Marehemu Balozi Lusinde amezaliwa Oktoba 9, 1930 na aliwahi kuwa Waziri wa Mawasiliano mwaka 1965 na ni miongoni mwa watu waliofanya kazi kwa ukaribu na Mwalimu Julius Nyerere kama Waziri wa Serikali za Mitaa mwaka 1961.

Pia, aliwahi kuwa Balozi wa Tanzania nchini China kuanzia mwaka 1975 hadi mwaka 1984 pamoja na kuwa Balozi wa Tanzania nchini Kenya.

Aidha, Marehemu Balozi Lusinde ndio kiongozi pekee aliyekuwa amebaki hai akiwa miongoni mwa Mawaziri wa Baraza la Kwanza la Mawaziri wa Serikali ya Awamu ya Kwanza iliyoongozwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Mwili wa kiongozi huyo unatarajiwa kuzikwa leo katika makaburi ya Kikuyu jirani na Chuo Kikuu cha Mtakatifu Yohana Jijini Dodoma.

Mara baada ya kutoa mkono wa pole Rais Dk. Shein ambaye pia, ni Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar alielekea katika Ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete Jijini Dodoma kushiriki kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM (NEC).

 

 

 

Comments are closed.