DK. HUSSEIN MWINYI AMEIPONGEZA SERIKALI YA INDIA ZA KUENDELEA KUIUNGA MKONO ZANZIBAR

Rais wa zanzibar na mwenyekiti wa baraza la mapinduzi dk. Hussein aali mwinyi amezipongeza juhudi za serikali ya india za kuendelea kuiunga mkono zanzibar katika kuimarisha sekta za kiuchumi na kijamii.

Wakati huo huo rais wa zanzibar amesema hatua ya kuunda serikali ya umoja wa kitaifa imelenga kuwawezesha wananchi kuishi kwa amani na utulivu na hivyo kuharakisha kasi ya kupata maendeleo.

Rais Dk Mwinyi aliyasema hayo leo Ikulu Jijini Zanzibar wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi Mdogo wa India anayefanyia kazi zake hapa Zanzibar Bhagwant Singh.

Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa Zanzibar inathamini sana uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo kati ya Zanzibar na India ambao umeipelekea nchi hiyo kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuendeleza miradi yake ya maendeleo.

Katika maelezo hayo, Rais Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kuipongeza Serikali ya India kwa kuiunga mkono Zanzibar katika sekta ya afya, elimu, maji, kilimo, biashara, huduma za jamii, uendelezaji wa rasilimali watu na nyenginezo.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi aliipongeza azma ya Serikali ya India ya ujenzi wa chuo cha amali huko kisiwani Pemba ambacho kitatoa mafunzo ya utalii pamoja na usarifu wa vyakula mbali mbali.

Alisema kuwa hatua hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kutimiza malengo ya Serikali ya kukuza ajira kwa vijana pamoja na kuifanya Pemba kuwa ni sehemu maalum ya uekeza sambamba na kuweza kutoa mafunzo kwa vijana katika kuendeleza sekta maendeleo ikiwemo utalii.

Rais Dk. Mwinyi pia, alizipongeza juhudi za Serikali ya India za kuuunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha huduma za maji safi na salama.

Pia, Rais Dk. Mwinyi alizipongeza mashirikiano yaliopo kati ya Zanzibar na India katika kusaidia masuala tiba pamoja na kutoa nafasi za masomo kwa wanafunzi kutoka Zanzibar.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kuzikaribisha Kampuni binafsi za India kuzitumia fursa mbali mbali zilizopo hapa Zanzibar kwa kuja kuekeza.

Aliongeza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itatafuta namna bora ya kuzitumia hudumz a mikopo zinazotolewa na India kwa ajili ya kuendeleza miradi mbali mbali ya maendeleo hapa nchini.

Pamoja na hayo, Rais Dk. Mwinyi alimuhakikishia Balozi huyo kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendeleza uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo baina ya pande mbili hizo.

Mapema Balozi Mdogo wa India anayefanyia kazi zake Zanzibar Bhagwant Singh aliupongeza uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu uliopo kati ya India na Zanzibar na kusisitiza kwamba nchi yake itauendeleza kwa manufaa ya pande mbili hizo.

Balozi Singh alimpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa kasi kubwa ya maendeleo sambamba na azma yake ya kuipaisha Zanzibar kiuchumi na kuahidi kwamba India itaendelea kuziunga mkono juhudi hizo.

Aidha, Balozi Singh alieleza kwamba nchi yake itaendea kutoa nafasi za masomo kwa Zanzibar zikiwemo zile za muda mfupi kwa watendaji wa Serikali kupitia Mpango wa India Technical and Economic Cooperation Program” (ITEC) na “International Forestic Science’(IFS).

 

Comments are closed.