CHANGAMOTO ZA MUUNGANO KUONDOLEWA

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amepongeza juhudi za makusudi zinazoendelea kuchukuliwa kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuondoa changamoto za Muungano.

Rais Dk. Hussein Mwinyi aliyasema hayo leo Ikulu Jijini Zanzibar katika mazungumzo kati yake na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Ummy Mwalimu aliyefika Ikulu kwa ajili ya Kujitambulisha.

Rais Dk. Hussein Mwinyi alipongeza hatua hiyo ambayo imekuwa ikifanyiwa kazi kwa makusudi katika kutatua changamoto hizo na kueleza matumaini yake kwamba hatua hiyo italeta mafanikio makubwa kwa pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Alisema kuwa mategemeo yake ni kutafutiwa ufumbuzi wa changamoto hizo na kueleza kwamba kwa yake yanayohusu ngazi za juu kwa upande wao wako tayari kuyafanyia kazi ili kufikia pale palipokusudiwa.

Nae Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Maziringira Mhe. Ummy Mwalimu alitumia fursa hiyo kwa kuanza kumpongeza Rais Dk. Hussein Mwinyi kwa kuchaguliwa kwa kura nyingi na wananchi wa Zanzibar.

Waziri Mwalimu ambaye alifuatana na Mkurugenzi wa Muungano Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk alieleza matumaini yake kwamba Zanzibar itafika mbali na kupata mafanikio makubwa kutokana na uongozi wa Rais Dk. Mwinyi hasa kutokana na kasi yake ya kutaka kuwaletea maendeleo wananchi wa Zanzibar.

Katika mazungumzo hayo, Waziri Ummy Mwalimu alimueleza Rais Dk. Hussein mwinyi juhudi za makusudi zinazoendelea kuchukuliwa katika kuzipatia ufumbuzi changamoto za Muungano ambazo kwa kiasi kikubwa juhudi hizo zimezaa matunda.

Aliongeza kwamba nyingi ya changamoto hizo tayari zimeshapatiwa ufumbuzi na zilizobaki ambazo ni chache utakeleza wake unatarajiwa kufanyika hivi karibuni katika vikao vitavyokaa kati yaviongozi wa SMT na SMZ.

Sambamba na hayo, Waziri Ummy Mwalimu alieleza azma ya kukaa kikao cha Kamati  ya pamoja ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ajili ya kuendelea na mchakato wa kuondoa changamoto zilizobaki.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi Dk. Khalid Mohammed Salum alisema kuwa mbali ya Waziri Mwalimu kuja kujitambulisha kwa Rais pia, Waziri huyo anatarajia kufanya ziara katika miradi ya Maendeleo ya Jamii (TASAF) pamoja na miradi ya Miundombinu ya Masoko, Uongezaji Thamani na Huduma za Kifedha Vijini(MIVAP).

Miongoni mwa mafanikio katika kutatua changamoto zilizopo mnamo Oktoba 17 mwaka huu 2020, SMT na SMZ zilisaini hati za makubaliano ya kuondoa hoja tano za changamoto zilizopatiwa ufumbuzi ambapo nyengine sita zinasubiri kupatiwa ridhaa ya kikao cha Kamati ya Pamoja kati ya SMT na SMZ ili nazo ziondolewe kabisa.

Kuondolewa kwa hoja hizoni miongoni mwa utaratibu wa kawaida wa kurekebisha changamoto zilizopo sambamba na kuuendeleza, kuuenzi, kuulinda na kuudumisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao tayari umeshatimia miaka 56 tokea kuasisiwa kwake.

Comments are closed.

error: Content is protected !!