Category Archives: Kitaifa

Habari za ndani ya nchi

WIZARA YA AFYA IMEPOKEA MSAADA WA VITANDA VYA KUJIFUNGULIA KUTOKA KWA JUMUIYA YA GLOBAL KINDNESS

Wizara ya Afya Ustawi wa jamii wazee jinsia na watoto imepokea msaada wa Vitanda vitano vya kujifungulia  vyenye thamani ya zaidi ya milioni nane kutoka kwa Jumuiya ya Global Kindness Foundation ya Nchini Canada kupitia Nyota Foundation ya Zanzibar.

Akipokea Msaada huo Waziri wa Wizara hiyo nd. Nassor Ahmed Mazuri amesema  msaada huo  uliotolewa  utasaidia katika kuimarisha huduma za Uzazi Nchini.

Aidha Mazrui amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara Afya Ustawi wa Jamii Wazee Jinsia na Watoto itahakikisha Huduma za Afya  zinaimarika zaidi na kuwataka Wafanyakazi kuwahudumia vyema Wananchi wanaohitaji huduma.

Mwakilishi wa Jumuiya ya Global Kindness Foundation kupitia Nyota Foundation  nd. Zainab Mvungi amesema  wameamua kutoa msaada huo kwa vituo vya Afya ili kina mama waweze kupata huduma zenye ubora.

Baadhi Wafanyakazi wameshukuru msaada huo na kuahidi kutimiza wajibu wao katika kutoa huduma stahiki kwa Wananchi.

Vituo vilivopata msaada huo ni Unguja Ukuu,  Chwaka, mwera selem na Bumbwini Misufini.

 

MASHIRIKIANO YA TAASISI ZA MIKOPO KWA WANAFUNZI WA ZANZIBAR NA TANZANIA KUZALISHA WATAALAMU NCHINI

Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar imesema mashirikiano ya kiutendaji kati ya taasisi zinazotoa Mikopo kwa Wanafunzi wa Zanzibar na Tanzania yatasaidia kuzalisha Wataalamu watakaosimamia maendeleo ya Nchi

Akizungumza katika hafla ya utiaji saini Hati za makubaliano ya Mkataba wa mashirikiano kati ya Bodi hizo mbili katibu Mkuu wa Wizara hiyo bw Ali Khamis Juma amesema hatua hiyo pia itasaidia kutanua huduma za kielimu kwa Wanafunzi ambapo ameshauri kutafuta njia bora katika kusaidia kutatua vikwazo vinavyowakabili ikiwemo urejeshwaji wa Mikopo

Mkurugenzi wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya juu Zanzibar bw Iddi Khamis Haji amezitaja miongoni mwa fursa watakazozipata kati yao ni kubadilishana watendaji kwa lengo la kujifunza mbinu bora za kukuza huduma wanazozitoa

Amewaomba  Wanafunzi kuhakikisha wanarudisha Mikopo baada ya kumaliza Masomo kwani Bodi hiyo imetoa wastan wa Shilingi Bilioni 66 kwa miaka 10  ambapo mrejesho ni wastan wa Shilingi Bilioni 3 kwa mwaka

Nae Mkurugenzi mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Tanzania bara bw Abdul-razak Badru amesema wamekuwa na mahusiano na Bodi ya Zanzibar kwa muda mrefu hasa katika kusaidia masuala ya urejeshaji wa Mikopo ambapo kwa Zanzibar wamekuwa wakifanya vizuri ukilinganisha na Tanzania Bara.

SERIKALI IMEWATAKA WAMILIKI WA VYOMBO VYA HABARI NCHINI KUENDANA NA MABADILIKO YA TEKNOLIJIA

Serikali imewataka wamiliki wa Vyombo vya habari Nchini kuhakikisha wanaendesha Tasnia ya Habari kwa kuendana na mabadiliko ya Teknolijia hiyo Duniani.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Dkt Ally Possi wakati akifungua kongamano la utangulizi la kuelekea siku ya Uhuru wa Habari, lililoandaliwa na Shirika la Elimu sayansi na Utamaduni la Umoja wa Taifa (UNESCO).

Amesema kwa upande wa Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa Habari Nchini ili kuweza kuboresha utendaji katika tasnia hiyo ambayo inatambulika kama muhimili wa nne usio rasmi.

Pia nd. Possi amesema serikali inaheshimu na kutambua uhuru wa Vyombo vya Habari na kuwataka wanahabari kutekeza majukumu yao kwa mujibu wa sheria na kanuni zilizopo nchini.

Katika kongamano hili kulitolewa tunzo kwa waandishi habari Wanawake, ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wao katika tasnia hiyo na Jamii kwa ujumla

Kitaifa maadhimisho ya siku ya Uhuru wa Habari yanatarajiwa kuanza Mei Mosi na kuhitimishwa mei tatu mwaka huu ambapo kitaifa yatafanyika Mkoani Arusha.