Category Archives: Kitaifa

Habari za ndani ya nchi

NBS YAFANYA MAPITIO YA KANUNI ZA TAKWIMU ZA MWAKA 2017

Ofisi ya Taifa ya takwimu (NBS) inafanya mapitio ya kanuni za takwimu za mwaka 2017 ili kuwezesha marekebisho ya sheria ya takwimu no 9 ya mwaka 2015 kwa lengo la kuimarisha mfumo wa uzalishaji  na utoaji wa takwimu na sio kudhibiti uzalishaji takwimu.

Mkurugenzi mkuu wa ofisi ya taifa ya takwimu Dr. Albina Chuwa ameeleeza hayo katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es salaam wakati akitoa taarifa ya marekebisho ya sheria hiyo  ambayo ilitungwa mwaka 2015 na kurekebishwa kupitia sheria ya marekebisho ya sheria mbalimbali na: 8 ya mwaka 2018.

Dr. Albina ameyabainisha maudhui makuu manne yaliyojikita kwenye  marekebisho ya sheria iliyopo kuwa ni  pamoja na kuweka  utaratibu wa uchambuzi wa kina kwa kutumia kanzi data ambazo zimeshatolewa na nbs, kuainisha mwongozo wa utoaji wa takwimu ambazo zinatofautiana na zilizotolewa na nbs, kuzuia utoaji wa takwimu zenye nia ya upotoshaji, na kuweka utaratibu wa uchapishaji wa taarifa za kitakwimu.

Aidha Dkt Albina amefafanua  kuwa marekebisho hayo ya sheria, yatachanganua na kuainisha namna bora ya utekelezaji wa matakwa ya sheria.

Kw aupande wake mkurugenzi mtendaji  wa taasisi ya utafiti ya repoa Dr. Donald Mmari amesema miongozo katika sheria inaelekeza wanatakwimu kutumia njia sahihi ili kupata takwimu bora.

WANANCHI WAKUBALI KUVUNJA NYUMBA ZAO KATIKA ENEO LINALOTARAJIWA KUJENGWA BARABARA

Mkuu wa mkoa wa Mjini Magharibi Ayoub Mohammed Mahmoud amewapongeza wananchi wa shehia za Kinuni, Mwembemajogoo na Nyarugusu kwa kukubali kuvunja nyumba zao katika eneo linalotarajiwa kujengwa barabara ya Tundaua – Kinuni Skuli kuanzia mwezi ujao.

Akizungumza na wananchi wa maeneo hayo jana baada ya kukagua eneo la ujenzi wa barabara hiyo, amesema hatua hiyo ya kizalendo inahitaji pongezi kwani inaunga mkono juhudi za serikali ya Zanzibar ya  kuwafikishia maendeleo wananchi wake.

Alisema uamuzi wa kujenga barabara hiyo unatokana na agizo la Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein alilolitoa wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi wa skuli 9 za kisasa za Unguja na Pemba katika shehia ya Kinuni, wilaya ya Magharibi ‘B’, Unguja mwezi Januari mwaka huu ili kurahisisha mawasiliano kati ya wananchi wa eneo hilo na maeneo mengine ya mkoa huo.

Aidha Mkuu wa Mkoa amesema ujenzi huo pia umezingatia umuhimu wa barabara hiyo kiuchumi na kijamii utaiunganisha barabara hiyo na barabara ya Magogoni - Tundaua – Kijitoupele iliyojengwa mwaka 2016/2017, utapunguza changamoto ya usafiri inayowakabili wananchi wa maeneo hayo.

Mheshimiwa Ayoub aliyeambatana na viongozi, maafisa na watendaji mbali mbali wa ngazi ya Mkoa,Wilaya,Manispaa,Wizara na viongozi wa Jimbo la Pangawe katika ziara hiyo iliyolenga kukagua maandalizi ya ujenzi huo, aliwahakikishia wananchi hao kuwa serikali ya Mkoa kwa kushirikiana na Manispaa ya Magharibi ‘B’ itatoa matofali 2,000 na mifuko 100 ya saruji itakayogaiwa kwa wananchi walioathiriwa na ujenzi huo ili kuharakisha marekebisho ya nyumba zao kupisha ujenzi huo.

Ili kufikia mustakabali mzuri wa ugawaji wa msaada huo Mhe Ayoub aliagiza kuundwa kwa kamati maalum inayotokana na wananchi wenyewe itakayofanya kazi kwa karibu na masheha wa shehia maeneo hayo ili kuratibu ugawaji wa msaada huo na kuongeza muda wa kuondoa majengo hayo hadi machi 15 mwaka huu badala ya machi 1.

Awali wakizungumza katika ziara hiyo baadhi ya wananchi wa maeneo yaliyoathiriwa na ujenzi wa barabara hiyo wamesema wameupokea kwa mikono miwili ujenzi huo na kuomba kupatiwa fidia kutokana na athari walizopata na kuongezewa muda uliowekwa kuondoa majengo yao.

Akitoa maelezo katika hafla hiyo Mhandisi Mkuu wa wizara ya nchi ofisi ya Rais, Tawala za mikoa, serikali za mitaa na idara maalum za SMZ Ali Omar Ali alisema barabara hiyo itakayojengwa kwa kiwango cha lami itakuwa na urefu wa kilomita 1 na upana wa mita 7 unaojumuisha mita 6 za lami na mita 1 ya mabega ya barabara itakayotumika kwa mitaro ya maji ya mvua.

Amesema usanifu wa barabara umefanyika kwa umakini mkubwa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha barabara inajengewa njia maalum za kupitishia maji ya mvua ili iwe imara zaidi lakini pia maji hayo yasiathiri makaazi ya wananchi.

Ujenzi wa barabara hiyo unatarajiwa kuchukua muda wa miezi 6 hadi kukamilika kwake, unajengwa kwa fedha za serikali ni mwendelezo wa uimarishaji wa miundombinu ya barabara za ndani katika Mkoa wa Mjini Magharibi unaofanywa kutekeleza ilani ya uchaguzi ya CCM na ahadi na maelekezo ya viongozi wakuu wa serikali.

MKURUGENZI WA VIPINDI NA UZALISHAJI WA CLOUDS MEDIA GROUP TANZANIA RUGE MUTAHABA AMERAFIKI DUNIA

Mkurugenzi wa vipindi na uzalishaji wa clouds media group tanzania ruge mutahaba amerafiki duniani nchini afrika kusini alipokuwa  akipatiwa matibabu ya figo.

Ruge ametoa mchango mkubwa katika tasnia ya habari, burudani, na alikuwa na juhudi za kujenga fikra za maendeleo ya vijana tanzania.

Mutahaba amezaliwa mwaka 1970 huko brooklyn nchini marekani na kupata elimu ya msingi arusha baadae akajiunga na skuli ya sekondari ya forodhani jijini dar es salaam pamoja na pugu.

Baadae alirejea nchini marekani kwa masomo ya elimu ya juu ikiwemo shahada ya uzamili na uzamifu.

Kupitia ukurasa wake rasmi wa twitter, rais magufuli ametoa pole kwa familia, ndugu jamaa na marafiki zake wa karibu wakiwemo wasanii wa hapa nchini.

WANANCHI WATOLEWA WITO WA KUYATUNZA MAENEO YENYE VIANZIO VYA VYA MAJI KWA HALI NA MALI

Wakati Wananchi wakitolewa wito wa kuyatunza maeneo yenye vianzio vya vya Maji kwa hali na Mali, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inafikiria kuyahifadhi Kisheria maeneo yote yenye vianzio hivyo kama ilivyohifadhi Kisheria Misitu Mikuu ya Jozani na Ngezi ili kuilinda  Rasilmali hiyo muhimu kwa ustawi wa Jamii.

Akiahirisha Mkutano wa Kumi na Tatu wa Baraza la Tisa la Wawakilishi huko Chukwani Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema maeneo ya vianzio vya Maji hayataruhusiwa kufanywa shughuli zozote za Kibinaadamu, hivyo aliwanasihi wale waliojenga katika maeneo hayo wajitayarishe kuondoka kwa hiari yao.

Balozi Seif alisema Serikali imejipanga kupambana na changamoto mbali mbali zinazoikabili Sekta ya Maji ikiwemo upotevu wa Maji unaosababishwa na uchakavu wa Miundombinu, uvamizi wa vianzio vya Maji, mwitiko mdogo wa kuchangia huduma ya Maji pamoja na utumiaji ovyo wa Maji majumbani na Ofisini.

Alisema lengo la Serikali Kuu ni kuongeza Miundombinu  itakayowezesha kujenga nguvu za kuwapatia huduma ya Maji safi na Salama Wananchi wote Unguja na Pemba ambapo usambazaji wa huduma hiyo unakadiriwa ufikie asilimia 97%  kwa maeneo ya Mjini na asilimia 85% Vijijini ifikapo Mwaka 2020.

Aliwaomba Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi washirikiane na Serikali katika kupambana na changamoto hizo ili kuihifadhi Rasilmali hiyo ya Maji inayoonekana kupungua kwa kasi Duniani kutokana na sababu tofauti ikiwemo kuchafuka kwa Mazingira.

Balozi Seif alisema kwa mujibu wa Ripoti ya Shirika la Afya Duniani {WHO} ifikapo Mwaka 2025 nusu ya Watu wanaoishi Duniani wapatao zaidi ya Bilioni Nane watakuwa wanaishi kwenye maeneo yenye matatizo ya upatikanaji wa huduma ya Maji.

Akizungumzia Mipango ya kukabiliana na uharibifu wa mazingira Nchini Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema Serikali inatayarisha Mkakati Shirikishi wa Kitaifa wa usimamizi wa Taka taka wenye lengo Kuu la kuhakikisha taka zote zinazozalishwa Nchini zinasimamiwa ipasavyo ili Miji yote iwe safi kwa faida ya Kiuchumi, Kimazingira pamoja na Kijamii.

Alisema suala la uchafuzi wa mazingira Nchini hasa utupaji taka na uchimbaji mchanga ovyo bado linaendelea kuleta changamoto kwa Taifa na Wananchi wenyewe katika maeneo mbali mbali Nchini.

Balozi Seif alisema Mamlaka za Serikali za Mitaa zina uwezo wa kusimamia wastani wa asilimia 50% ya Taka zote zinazozalishwa zikiwa na wastani wa Tani Laki 238,700 kwa Mwaka Unguja na Pemba.

Alisema ni jambo la kusikitika kuona taka zinazobakia hutupwa ovyo vichakani badala ya kupelekwa kwenye jaa jipya lililotengenezwa Kitaalamu katika eneo la Kibele.

Alionywa kwamba kuna taarifa zinazoelezea uwepo wa baadhi ya Hoteli za Kitalii hutumia Makampuni ya kukusanya taka taka ambazo kwa tamaa zao za kutaka faida kubwa huishia kuzitupa taka taka hizo kwenye vichaka badala ya eneo maalum lililotengwa na Serikali liliopo Kibele.

Balozi Seif  alizitaka Mamlaka za Serikali za Mitaa kuzanzia sasa kuhakikisha kwamba Hoteli zote zilizomo kwenye Mamlaka yao zinatumia Makampuni yanayofuata Sheria ya Utunzaji wa Mazingira badala ya kuzitupa ovyo katika Mitaa.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwakumbusha Wananchi kuacha tabia ya kutupa taka ovyo kwenye mitaro hasa kipindi hichi kinachokaribia kuingia msimu wa Mvua za Masika ambazo wakati mwengine husababisha mafuriko yanayoweza kuleta maafa hapo baadae.

Alisema juhudi za Serikali ilizozichukuwa na inayoendelea kuzichukuwa katika kukabiliana na maafa haziwezi kufanikiwa bila ya mashirikiano ya kina pamoja na Wananchi wake.

Balozi Seif alifahamisha kwamba Serikali kwa upande wake imejipanga kupambana na maafa yanayoweza kusababishwa na mvua hizo kwa ujenzi wa daraja la Kibonde Mzungu na Mwanakwerekwe sambamba na ujenzi wa Mitaro inayoendelea ya maji ya Mvua katika maeneo mengi ya Mkoa Mjini Magharibi ambayo huonekana kuathirika zaidi wakati wa mvua kubwa zinaponyesha.

Akizungumzia jitihada zinazochukuliwa na Serikali za mapambano dhidi ya vitendo vya Udhalilishaji Nchini Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema kadhia hiyo bado inaendelea kuwatesa Wanawake na Watoto siku hadi siku na hivi sasa vinaonekana kutokea kwa njia nyengine.

Balozi Seif alisema katika kipindi cha Mwezi Julai hadi Disemba 2018, jumla ya matukio Mia 466 yanayohusu vitendo vya udhalilishaji vikiwemo kubaka 257, kulawiti 56, kuingilia kinyume cha maumbile 8, kutorosha 70, shambulio la aibu 75 yameripotiwa katika vyombo vya Dola.

Alisema kwa vile hali bado ni mbaya katika Jamii aliwashauri na kuwaaidhi Wazazi pamoja na Jamii yote kuwa karibu kwa kufuatilia mienendo ya Watoto wao ili kuweza kujua walipo na wanachofanya muda wote.

Hata hivyo Balozi Seif  aliwakumbusha Masheha na Wananchi Mitaani wanapogundua uwep wa Mtu asiyeeleweka  katika maeneo yao wanapaswa kutoa Taarifa haraka kwenye vyombo husika ili kufuatiliwa na hatimae kujiridhisha na hali halisi ya mazingira ya uwepo wa Mtu huyo.

Alitoa msisitizo kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, Viongozi wa Dini, Asasi za Kiraia, Makundi ya Malezi kuendelea kuwaelimisha Wananchi Mitaani katika kusimamia Malezi bora yanayoendana na Mila, Silka na Tamaduni zilizoachwa na Wazee waliopita.

Akigusia Sekta ya Utalii ikiwa ni miongoni mwa muhimili muhimu unaotegemewa na Taifa katika Uchumi wa Nchi Balozi Seif  alisema tukio lolote linaloweza kuhatarisha Sekta hiyo halitavumiliwa na Serikali kwani linaweza kuviza Ustawi wa Jamii kupitia Sekta hiyo.

Alitahadharisha kwamba Serikali inatoa onyo kali kwa wale wanaoendesha vitendo vya uhalifu kwenye Fukwe wanapaswa kuacha mara moja tabia hiyo mbaya inayolitia aibu Taifa kwa wageni wanaoamua kufika Nchini kimatembezi.

“ Hatutamuonea haya Mtu ye yote atakayeendesha vitendo vya uhalifu na hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake”. Alionya Balozi Seif.

Halkadhalika Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  aliwataka Vijana wanaofanya biashara ndogo ndogo kuacha mtindo wa kuwabughudhi Watalii wanapotembea ufukweni kwa kuwalazimisha kununua bidhaa zao hata kama hawazihitaji.

Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi  walijadili Miswada Miwili, kupokea Ripoti za Kamati za Baraza ikiwemo ile ya Kamati Teule ya kuchunguza Majengo ya Skuli 19 za Sekondari  katika Mkutano wa Kumi na Tatu za Baraza la Tisa la Wawakilishi Zanzibar.

Pia Wajumbe hao walipokea Taarifa ya Serikali inayohusu Hoja ya Mjumbe kuliomba Baraza la Wawakilishi kutoa Maazimio ya kushughulikia kwa haraka tatizo la kuharibika kwa vifaa Tiba vya Hospitali ya Abdulla Mzee Mkoani Pemba pamoja na kupokea Muelekeo wa Mpango wa Taifa.

Jumla ya Maswali ya msingi yapatao Mia Moja na Thalathini na Tano na Mia Moja na Kumi na Saba ya nyongeza yaliulizwa na Wajumbe wa Baraza la Waakilishi na kujibiwa na Waheshimiwa Mawaziri wa Wizara Tofauti.

Baraza la Wawakilishi Zanzibar {BLW} limeahirishwa hadi Jumatano ya Tarehe 08 Mei Mwaka 2019.

error: Content is protected !!