Category Archives: Kitaifa

Habari za ndani ya nchi

WANAFUNZI WALIOTOKA MASOMONI NCHINI CHINA WAMEIOMBA SERIKALI JUU YA SUALA LA AJIRA

Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu Zanzibar imewataka Wanafunzi waliorejea Nchini kutoka Masomoni Nchini China kuwa tayari katika kulitumikia Taifa lao ili kuongeza Wataalamu katika fani tofauti.

Akizungumza na Wanafunzi kumi na moja huko Uwanja wa Ndege wa  Abedi Amani Karume waliorejea  Kutoka China Mkurugenzi wa Bodi hiyo Nd.Idd Khamis Haji amesema hatua hiyo pia itasaidia kuleta ufanisi katika kazi.

Amesema Taifa lenye Wasomi husaidia kupata Mabadiliko ya haraka ya maendeleo hali iliyopelekea Serikali kupitia Bodi hiyo kutafuta nafasi hizo za Masomo zaidi ili kuona inayafikia mabadiliko hayo, aidha mkurugenzi haji ameishukuru serikali ya china kwa ushirikiano waliowapa katika kuwalinda Wanafunzi hao dhidi ya Janga la Covid 19 na kupelekea kutopata athari ya Ugonjwa huo na kurejea Nyumbani wakiwa salama .

Wanafunzi hao wameishukuru Serikali kwa kuwapatia huduma muhimu hali iliyowafanya waongeze juhudi katika masomo yao pamoja na kukabiliana na vikwazo vilivyojitokeza  ikiwemo lugha ya kichina na kusoma kwa njia ya Mtandao wakiwa katika Makaazi yao katika kipindi chote cha mripuko wa Corona.

Nao wazee wa Wanafunzi hao wamesema ujio wa Wanafunzi hao umeleta faraja na kuiyomba Serikali kuwapatia Ajira ili kuweza kujikwamua na ukali wa maisha.

Zaid ya Shilingi Milioni mia mbili zimetumiwa na Bodi hiyo katika kuwasomeshea Wanafunzi hao waliomaliza Shahada ya Habari ambapo gharama nyengine zimetolewa na Serikali ya China.

 

DK.MAGUFULI AMEMSHUKURU DK. SHEIN KWA USHIRIKIANO WAKE KATIKA KUWATUMIKIA WANANCHI

Rais Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr.John Pombe Magufuli amevitaka Vyama vya Siasa vitakavyoshiriki Uchaguzi Mkuu Mwaka huu kujiepusha na vurugu na kwamba Serikali ipo macho kusimamia amani ya Nchi.

Dr.Magufuli akilifunga Bunge la Kumi na moja Mjini Dodoma amesema Uchaguzi huo utafuata Demokrasia kwa kuwa huru na haki na kuviomba Vyama vya Siasa kutoa nafasi za kugombea kwa Wanawake, Vijana na wenye Ulemavu.

Ameeleza kuwa Uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Mwezi wa Oktoba ni lazima ufanyike amani bila ya kuendeleza kejeli na matusi na kuviomba Vyama vya Siasa kushinda na kwa hoja na kushindanisha ilani za Vyama vyao.

Aidha Dkt. Magufuli amemshukuru Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Ali Mohamed Shein kwa kushirikiana nae katika kutumikia umma kwa kiasi kikubwa na amehaidi kumuenzi kama viongozi wengine.

Ameeleza kuwa amekuwa akifanya kazi kwa karibu zaidi na Viongozi wa pande zote mbili katika kuwaletea Maendeleo Wananchi wa Tanzania na kuimarisha Sekta mbali mbali ikiwemo Elimu, Afya, Kilimo, Miundombinu na Sekta nyenginezo.

Akizungumzia suala la Corona Rais Dr.Magufuli amesema kwa vile Maradhi hayo yamepunguwa kwa asilimia kubwa ameruhuru shughuli za Kijamii kuendelea pamoja na kufungliwa Skuli zote kuanzia ngazi ya msingi kuanzia June 29 Mwaka huu.

MFANYABIASHARA SAID BOPAR AKABIDHI MSAADA KWA WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA AMALI

Wanafunzi wa Kidato cha Sita Nchini wametakiwa kuendelea kuchukua juhudi katika kujitayarisha na Mitihani yao inayotarajiwa kufanyika hivi karibuni ili waweze kupata ufaulu mzuri.
Akizungumza na Wanafunzi wa Kidato cha Sita wakati akiwakabidhi vifaa mbali mbali kwa ajili ya kujikimu katika kipindi cha Mitihani yao ya Taifa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Mh.Riziki Pembe Juma amesema licha ya Dunia kukumbwa na Janga la Corona lakini juhudi zao ndio chachu ya kufikia malengo yao.
Mfadhili wa Misaada hiyo Ndugu Said Bopar amesema lengo la misaada huo ni kuwaandali Mazingira bora yakufanya Mitihani yao katika hali ya utulivu kwa kuwaondoshea usumbufu katika kipindi cha Mtihani.
Baadhi ya Walimu na Wanafunzi hao wamesema licha ya Kufungwa Skuli kwa muda kutokana na changamoto ya Maradhi ya Corona bado matumaini yao ni kupata Matokeo mazuri kwani wameitumia fursa hiyo kujiandaa vyema na Mitihani yao.

CCM YATAFAKARI KIONGOZI ATAKAYEFAA KWA MIAKA MITANO IJAYO

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema wakati muda wa kuelekea katika uchaguzi Mkuu unakaribia Wana CCM na Wananchi wana fursa nzuri ya kutafakari Kiongozi  atakayefaa kuwaongoza katika kipindi kijacho cha Miaka Mitano.
Alisema Viongozi wanaofaa kushika hatamu ya kuwaongoza vyema ni wale wenye uwezo kamili wa kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM inayokwenda kisasa katika mazingira ya Karne ya sasa ya Sayansi na Teknolojia Ulimwenguni.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa Kauli hiyo akimuwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduziu Dr. Ali Mohamed Shein katika uzinduzi wa Tangi kubwa la Kuhifadhia Maji safi na salama pamoja na uzinduzi wa Ofisi ya Jimbo la Kikwajuni iliyofanyiwa matengenezo makubwa ikiwa ni umaliziaji wa Utekelzaji wa Ilani ya Uchaguzi ndani ya Jimbo hilo.
Alisema Wananchi wanapaswa kufanya tathmini ya kina itakayoweza kuwaibulia mchapakazi imara  atakayejitolea kusimamia kwa wakati wote masuala yao ya Maendeleo na Uchumi  katika maeneo yao.
Alibainisha kwamba kumchagua Kiongozi kabla ya kumfanyia uhakiki wa kina huleta hatari kwani matokeo yake ni majuto yasiyokuwa na suluhu na hata kama uchaguzi wenyewe ukiambatana na rushwa inayokuwa kaa la moto ndani ya Miaka Mitano ya yule aliyechaguliwa.

Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif aliwakumbusha Wanachama wenye nia ya kuchukuwa Fomu kwa ajili ya kuomba Uongozi ndani ya CCM wazingatie Sheria, Muongozo na Taratibu zilizowekwa.
Aliupongeza Uongozi wa Jimbo la Kikwajuni kwa kazi kubwa ya kuwaletea Maendeleo Wananchi wake wakiwemo wale wa Mitaa ya jirani kazi iliyoleta Mafanikio Makubwa na ya kupigiwa mfano ndani ya Utekelezaji wa Ilani ya Chama ikienda sambamba na utekelezaji wa Ahadi uliyotoa wakati wa Kampeni.
Wakiwasilisha Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2015 – 2020 Mwakilishi wa Jimbo la Kikwajuni Mh. Nassor Salum Jazira na Mbunge wa Jimbo hilo Mhandisi Hamad Yussuf Masauni wamesema CCM kwenye uchaguzi ujao haitapata shida kuwanadi Wagombea wake watakaopata fursa ya kuteuliwa kugombea Jimbo hilo.
Walisema hiyo inatokana na Utekelezaji mkubwa wa Ilani ya Uchaguzi  ndani ya Jimbo la Kikwajuni Wilaya ya Mjini ambayo imepindukia kwa asilimia 100%.
Mh. Nassor Jazira na Mhandisi Masauni  walieleza kwamba uimarishaji wa Sekta ya Maji uliosimamiwa na Uongozi wa Jimbo kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maji Zanzibar {ZAWA} umelea Ukombozi mkubwa kwa Wananchi  waliowengi ndani ya Jimbo hilo ambao sasa utabakia kuwa Historia kutokana na kuondoka kwa changamoto ya huduma ya Maji.
Mapema Katibu wa Chama cha Mapinduzi Jimbo la Kikwajuni Nd. Farid Abdullah Hamad alisema kwa Niaba ya Wanachama na Wananchi wa Jimbo hilo wanaishukuru Serikali Kuu kwa nguvu kubwa iliyochukuwa ya kuimarisha Miundombinu mingi ya Maendeleo ndani ya Jimbo hilo.
Nd. Farid alisema Wananchi wa Jimbo la Kikwajuni na maeneo jirani wana haki ya kujivunia kutokana na neema ya Maendeleo hayo ambayo wameiomba Serikali kupitia Taasisi yake kutoa upendeleo wa fursa za Ajira kwa ile Miradi ya Uwekezaji iliyoanzishwa katika Jimbo hilo.
Katika shughuli hiyo Balozi Seif Ali Iddi amekabidhi Kadi za C.C.M kwa Wanachama 31 Waliohama Vyama tofauti vya Upinzani na kuhamia Chama cha Mapinduzi.
Halkadhalika akakabidhi  mchango wa Computer na Printer Zake, Garil Moja ya Jimbo, Basi Moja na Seti za Jazi kwa Chuo cha kuwafundishia Vijana masuala mbali mbali ya Michezo na ushoni.

error: Content is protected !!