Category Archives: Kimataifa

habari za nje ya nchi

MH. MGENI HASSAN AMESEMA WANAWAKE WANA NGUVU KUBWA KATIKA NGAZI ZOTE ZA KIUCHUMI, KISIASA ,KIJAMII

Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Mhe. Mgeni Hassan Juma amesema Wanawake Wana nguvu kubwa katika ngazi zote za Kiuchumi, Kisiasa na Kijamii ya kulifanya Taifa kupiga hatua za Maendeleo

Akizungumza katika kongamano la Shamra shamra za kuadhimisha siku ya Wanawake Duniani Mhe Mgeni amesema katika kufikia hatua hizo Wanawake nao wako mstari wa mbele kupiga vita Umasikini ili kuwepo na usawa.

Amewataka kinamama kubadilika kwa kujiendeleza katika nyanja mbali mbali za Maendeleo ikiwemo ushiriki  kugombea nafasi za uongozi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

Wakichangia mada zilizowasilishwa katika mdahalo huo washiriki wamevitaka vyama vya siasa kuweka miongozo ya nafasi za uongozi kwa Wanawake  katika vyama vyao ili waweze kufanikisha mawazo yao kuweza kuleta mabadiliko.

Mdahalo huo uliotayarishwa na Asasi za Kiraia zinazopigania Maendeleo ya Wanawake  Nchini, chini ya ufadhili wa UN WOMEN, umewashirikisha Viongozi   wa vyama vya siasa, Tume ya Uchaguzi, Viongozi wa Dini na Wanawake ukiwa na kauli mbiu ya “Ushiriki wa Wanawake ni chachu ya Maendeleo.

 

 

BALOZI ALIYETEULIWA NA GUAIDO ACHUKUA UDHIBITI WA UBALOZI NCHINI MAREKANI

Balozi aliyechaguliwa na kiongozi wa upinzani wa venezuela juan guaido kuwa mwakilishi wa nchi yake nchini marekani carlos vecchio, ametangaza kuchukua udhibiti wa maeneo matatu nchini marekani ambayo kidiplomasia ni mali ya venezuela. Vecchio ameingia katika majengo mawili ya jeshi la venezuela mjini washington, huku waziri anayehusika na masuala ya ushauri gustavo marcano aliyeteuliwa na guaido akiuchukua ubalozi mdogo mjini new york. Waziri wa mambo ya nje wa venezuela jorge arreaza ambaye ni mtiifu kwa rais nicolas maduro amelaani hatua hiyo, akiita kuwa ukaliaji haramu na wa kimabavu. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya marekani amethibitisha kwamba serikali ya rais donald trump imeridhia hatua hizo zilizochukuliwa na upande wa guaido, ambaye imemtambua rasmi kama kiongozi wa mpito wa venezuela.

WASHUKIWA 3 WAKAMATWA KUHUSIANA NA SHAMBULIZI LA RISASI UTRECHT, UHOLANZI

Washukiwa watatu wanaaminika kuwa wamewekwa kizuizini na polisi kufuatia shambulizi la risasi ndani ya treni katika mji wa ultrecht nchini uholanzi, ambapo watu watatu waliuawa. Haijabainika sababu ilichomfanya mshukiwa aliyetambuliwa kwa jina gokmen tanis mzaliwa wa uturuki mwenye umri wa miaka 37, kuwafyatulia risasi abiria ndani ya tramu na kukimbia. Meya wa mji wa ultrecht jan van zanen amesema watu watano wamejeruhiwa kwenye shambulizi hilo, watatu kati yao wakiwa katika hali mbaya. Mshukiwa wa pili alitiwa nguvuni kuhusiana na uhalifu huo, lakini haijabainika wazi alihusika kwa kiwango gani.

BALAA LA KIMBUNGA IDAI LAWATESA WAMSUMBIJI

Huenda zaidi ya watu 1000 wameuwawa na kimbunga idai kilichosababisha mafuriko makubwa katika maeneo mbali mbali ya msumbiji,mpaka zimbabwe na malawi. Nchini msumbiji kimbunga hicho kilichosababisha mafuriko mabaya kabisa kimeendelea kuzusha hofu na wasiwasi. Rais wa nchi hiyo phillipe nyusi ameiambia redio msumbiji kwamba idadi ya waliouwawa huenda ikafikia watu 1000. Mashirika ya msaada yamesema  kiwango kamili cha uharibifu uliosababishwa na kimbunga hicho pamoja na mafuriko hakijuulikani hadi sasa. Kimbunga cha idai kilichoandamana na upepo mkali uliopiga kwa kasi ya kilomita 160 kwa saa kilisababisha maporomoko ya ardhi nchini msumbiji kabla ya kupungua kasi na kuelekea nchini zimbabwe