BALOZI SEIF AMEZITAKA TAASISI NYENGINE HAPA NCHINI KUENDELEA KUWASAIDIA WATU WENYE MAHITAJI MAALUM

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema  uamuzi wa Kampuni ya Sigara Tanzania {TCC} wa kuwa karibu na watu wenye mahitaji maalum unapaswa kuendelea kuungwa mkono na taasisi nyengine hapa nchini.

Balozi Seif Ali Iddi amesema hayo hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar wakati wa mazungumzo yake na uongozi wa ngazi ya juu wa Kampuni ya Sigara Tanzania ambao upo Zanzibar kujitayarisha kutoa msaada wa vifaa tofauti kwa watu wenye ulemavu Visiwani Zanzibar.

Amesema zipo taasisi na Makampuni mengi ndani na nje ya nchi yenye uwezo na fursa kubwa ya kusaidia kundi hilo maalum lakini matokeo yake ni machache mno yanayotenga muda wa kujitolea kufanya hivyo kwa watu hao wenye haki ya kupata huduma kama yalivyo makundi mengine

Balozi Seif aliushukuru na kuupongeza uongozi wa Kampuni ya Sigara Tanzania kwa uamuzi na moyo wake wa kizalendo uliopelekea kuliona kundi hilo la watu wenye mahitaji maalum na hatimae kulisaidia kwa vifaa pamoja na uwezeshaji wa kiuchumi.

Aliueleza uongozi huo wa TCC kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini jitihada za Kampuni hiyo na itajitahidi kuunga mkono katika kuona changamoto zinazoikwaza kampuni hiyo katika harakati zao za kusaidia jamii zinaondoka.

Mapema Mkurugenzi wa Sheria na mahusiano wa Kampuni ya Sigara Tanzania {TCC}

Nd.Godson Kiliza alisema uamuzi wa kampuni hiyo wa kuanzisha mradi wa kusaidia kundi la watu wenye mahitaji maalum ni kurejesha mafidha kwa jamii.

Nd. Godson alisema mradi huo ulioanza kwa takriban mwaka mmoja sasa kwa kushirikiana na serikali kupitia shirikisho la jumuiya ya walemavu nchini umekuwa ukiwapatia vifaa tofauti watu wenye ulemavu.

Alisema vifaa hivyo ikiwa ni pamoja na Baskeli za Walemavu, Magongo na Fimbo hutolewa sambamba na kuwapatia baadhi ya watu wenye ulemavu vibanda kwa lengo la kuendesha biashara ndogo ndogo ili kukidhi matihaji yao ya msingi.

Alieleza kwamba bajeti yao ya mradi huo kwa mwaka 2019 ambayo ni endelevu inamalizia katika Visiwa vya Zanzibar ambapo jumla ya watu wenye mahitaji maalum wapatao 210 kutoka Unguja na Pemba wanatarajiwa kupata msaada wa baskeli, magongo pamoja na fimbo.

Amesema katika kuunga mkono jitihada za kuuendeleza mradi huo maalum kwa jamii nd.Godson Kiliza alizihamasisha taasisi na Jumuiya za kiufundi zilizopo Zanzibar kuchangamkia tenda ya utengenezaji wa vifaa kwa ajili ya kundi hilo maalum kupitia uwezeshaji wa Kampuni hiyo.

 

 

 

Comments are closed.

error: Content is protected !!