Recent Posts by Wardat Mohd

VIONGOZI NA WANACHAMA WA SACCOS NCHINI WAMETAKIWA KUFANYAKAZI KWA USHIRIKIANO NA UADILIFU

 

Viongozi na Wanachama wa vyama vya Akiba na mikopo (Saccos) nchini wametakiwa kufanyakazi kwa ushirikiano na uadilifu    ili vyama hivyo viweze kuwa endelevu     na kufikia malengo yake.

Hayo ameyaeleza   Mwenyekiti  wa kamati ya Maendeleo ya Wanawake Habari na Utalii ya Baraza la Wawakilishi  Mhe. Mwantatu Mbarak wakati kamati hiyo   ilipotembelea taasisi ya fedha ya Wanaushirika ya Faraja Union Limeted iliopo Kisiwandui   Mjini Zanzibar.

Amesema taasisi hizo za fedha ni chombo muhimu hivyo masuala hayo ni ya kuzingatia pamoja na kuwa na lugha nzuri katika utoaji wa huduma .

Naye Katibu  wa Faraja Union Limeted Omar Juma Said amesema taasisi  yake ina wanachama 16 ambao ni Saccos na vyama vya ushirika kutoka unguja na pemba.

Amesema lengo la taasisi  hiyo  ni kupata nguvu ya pamoja ili kutowa mikopo itayoelekeza kwenye uwekezaji wa kati ,kilimo na uvuvi kwa wanachama wake . Faraja Union Limited imezinduliwa tarehe  7/1/2020.

 

 

MH. HAROUN AMESHIRIKI KATIKA MAHAFALI YA KUMI NA MBILI YA CHUO CHA UTAWALA WA UMMA IPA

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mh.Haroun Ali Suleiman ameutaka Uongozi wa Chuo cha Utawala wa Umma ,kufanya tathmin ya utendaji kwa  Wanafunzi wanaomaliza Chuoni hapo ili kwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia.

Waziri Haroun ametoa kauli  hiyo katika mahafali ya kumi na mbili ya Chuo cha Utawala wa Umma IPA ,ambapo amesema Serikali imetumia pesa nyingi  kuanzisha Chuo hicho hivyo ni jukumu lao kuhakikisha Taifa linapata Watumishi wenye ujuzi.

Aidha amewataka wahitimu waliokuwemo katika Utumishi wa Umma kutumia vyema Taaluma waliyoipata katika kufanya kazi kuleta mabadiliko chanya wakati wa kurudi kazini, na kuacha tabia ya kutekeleza majukumu yao kimazowea.

Mkurugenzi wa Chuo cha Utawala wa Umma Dr.Mwinyi Talib amesema licha ya mafanikio  mbali mbali yaliyo patikana  katika utoaji wa taalum bado chuo kinakabiliwa  changamoto ikiwemo uhaba wa Ofisi na Vyumba vya Kusomea .

Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Fatma Said amesema Chuo cha Utawala wa Umma kinaendelea kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo  watumishi wa umma ili kuendana na mabadiliko ya kiutendaji  na  Baraza la Chuo  linaendelea kushirikiana na Chuo katika utendaji wa kazi zao.

Jumla ya wahitimu 860 wa Cheti na Stashahada wametunukiwa vyeti vyao ambapo kati ya hao Wanawake ni 596 na Wanaume 264.

BALOZI SEIF AMETIA SAINI KITABU CHA MAOMBOLEZO KUFUATIA KIFO CHA SULTAN QABOOS

 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd ametia saini kitabu cha maombolezo kufuatia kifo cha aliyekuwa mtawala wa Oman Sultan Qaboos bin Said Al Said kilichotokea usiku wa kuamkia Jumamosi iliyopita kwenye Qasri yake Beit Al Baraka Nchini Oman.

Marehemu Qaboos Bin Said Al Said aliyefikisha umri wa miaka 79 aliitawala Oman kwa miaka 50 ambapo utawala wa nchi hiyo unaongozwa na mrithi mpya Binamu wake Haitham bin Tariq aliyekuwa Waziri wa Mirathi na Utamaduni wa Oman ambapo ametenga siku tatu za maombolezo.

DK. MAGUFULI AMEWAAPISHA MABALOZI 4 ALIOWATEUA KARIBUNI KUIWAKILISHA TANZANIA KATIKA NCHI NYENGINE

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mhe. Dk. John Pombe Magufuli amewaapisha mabalozi 4 aliowateua hivi karibuni kuiwakilisha Tanzania katika nchi za Afrika Kusini, Namibia, Zimbabwe na Nigeria.

Walioapishwa ni Mej. Jen (mstaafu) Gaudence Salim Milanzi anayekuwa balozi wa Tanzania Pretoria - Afrika Kusini, Dk. Modestus Francis Kipilimba anayekuwa balozi wa Tanzania Windhoek – Namibia, Prof. Emmanuel David Mwaluko Mbennah anayekuwa balozi wa Tanzania Harare – Zimbabwe na Dk. Benson Alfred Bana anayekuwa balozi wa Tanzania Abuja – Nigeria.

Akizungumza mara baada ya kuwaapisha Mabalozi hao, Mhe. Rais Magufuli amewataka kuripoti katika vituo walivyopangiwa ndani ya wiki 2 kuanzia sasa na amewasisitiza kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria, na kuzingatia maslahi ya Taifa hasa kiuchumi na kuwawezesha Watanzania kupata ajira katika fursa zilizopo katika nchi hizo.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi amewataka Mabalozi hao kuitangaza vyema Tanzania ambayo kwa sasa inapiga hatua kubwa katika maeneo mengi.

Hafla ya kuapishwa kwa Mabalozi hao imefanyika Ikulu jijini Dar es salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Makamu wa Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa

Recent Comments by Wardat Mohd

No comments by Wardat Mohd yet.

error: Content is protected !!