Recent Posts by Wardat Mohd

WADAU WA SEKTA YA UTALII WAMETAKIWA KUWEKA WAZI HATUA ZA KUTATUA KASORO ZA UENDESHAJI WA SEKTA HIYO

Waziri wa Habari Utalii na Mambo ya Kale Mh.Mahmoud Thabit Kombo amewataka Wadau wa Sekta ya Utalii kuweka wazi hatua za kutatua kasoro za uendeshaji wa Sekta hiyo Zanzibar zilizochukuliwa kwa pamoja na Serikali .

Akizungumza katika Kikao kati ya Wadau wa Sekta ya Utalii na Viongozi wa Jumuiya ya kuratibu masualaya Utalii ya Nchini Italia, amesema hatua hiyo itawezesha kupunguza malalamiko kutoka kwa Wawekazaji  wa Sekta hiyo inachangia pato kubwa la Taifa.

Waziri Mahmoud amefahamisha kuwa miongoni mwa juhudi hizo  ni pamoja kuimarisha huduma na ujenzi wa Uwanja wa Ndege, na  Barabara mbalimbali na pamoja na kuanzishwa mfumo wa Kisasa wa kupata  Viza  kwa Wageni kwa njia ya Kielektroniki.

Viongozi wa Jumuiya hiyo ya kuratibu masuala ya Utalii ya Nchini Italia, wamesema wamesisitiza kuwekwa Mfumo bora wa ulipaji Kodi kulingana na misimu ya Wageni wanavyotembele Nchini.

Jumuiya hiyo inayotambulika kwa jina la Astoi Confindustria Viaggi inaratibu Safari za kiasi ya  Watalii  laki moja na nusu wanaotembelea Zanzibar  kwa Mwaka.

TAASISI BINAFSI ZIMETAKIWA KUSHIRIKIANA NA SERIKALI KATIKA KUPAMBANA NA MABADILIKO YA TABIA NCHI

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Mh.Muhammed Aboud amesema upatikanaji wa fedha za uhakika ndio njia muhimu ya kufikia malengo ya pamoja ya kukabiliana na athari za   mabadiliko ya tabia Nchi.

Amesema  katika mpango hio ni muhimu kushirikishwa  Taasisi Binafsi zikiwemo Mabenki mbalimbali ili kusaidia mapambano hayo ambayo kwa sasa ni janga la Dunia.

Akizungumza katika Mkutano wa kuangalia mahitaji ya Kifedha katika kukabiliana na mabadiliko hayo kwa Nchi za Afrika Mashariki Mh.Aboud amewasisitiza Wataalamu hao kushirikiana katika kufikia lengo hilo muhimu kwa mustakbali wa Mataifa hayo

Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Nd. Bazivamo Cristopha amesema lengo kuu ni kusaidia Nchi zinazoendelea kupanga mahitaji na vipaumbele vyao katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabia Nchi kwa   ushikiriano.

Mkutano huo umewashirikisha Wataalamu wa masuala ya Mazingira za Nchi Wanachama wa Nchi za Afrika Mashariki umeandaliwa  kwa  Ushirikiano wa pamoja wa Ulaya.

DK.SHEIN AMESEMA KUNA UMUHIMU WA KUTIZAMA UPYA SHERIA ZINAZOSIMAMIA USALAMA WA CHAKULA NCHINI

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk.Ali Mohamed Shein amesema kuna umuhimu wa kutizama upya Sheria zinazosimamia mwenendo wa usalama wa Chakula Nchini, ili kuondokana na malalamiko mbali mbali ya Wafanyabiashara.

Dk. Shein ametowa ufafanuzi huo, wakati akipokea Taarifa ya utekelezaji wa mpango kazi ya Wizara ya Afya, kwa kipindi cha kuanzia Julai hadi Disemba, 2019, hafla iliyofanyika Ikulu Mjini hapa.

 

Alisema kuna umuhimu kwa Uongozi wa Wizara hiyo kuziangalia upya Sheria zinazosimamia Usalama wa Chakula, hususan katika suala zima la Ukaguzi wa bidhaa zinazotoka na kuingia Nchini,           kwa kigezo cha kuwepo malalamiko kutoka kwa wafanyabaishara juu ya tozo wanayolipa kugharamia   ukaguzi huo.

 

Alisema Wafanyabishara wamekuwa wakilalamikia gharama hizo, kwa kigezo kuwa dhima ya kuthibitisha ubora wa Bidhaa  uko mikononi kwa Serikali badala ya wao kubebeshwa Mzigo huo.

 

Alisema  pamoja na sheria zilizopo kuwa na uwiano katika nchi nne za afrika mashariki, kuna umuhimu wa kuzipitia upya kwa kuzingatia kuwa serikali ndio yenye dhima katika kufanya utafiti na kupata matokeo.

 

Dk. Shein alieleza wafanyabiashara wamekuwa wakilalamikia kuwepo kwa utitiri wa taasisi za uchunguzi, jambo linaloongeza urasimu.

 

Alieleza kuwa mbali na taasisi hizo kuongozwa  na sheria yake kila moja, kuna umuhimu wa viongozi kukaa pamoja ili kuwa na mfumo maalum wa utoaji wa tozo moja.

 

Alisema serikali haiwezi kupuuza malalamiko ya wafanyabiashara hao na kubainisha kuwa itafanya juhudi za kuzitafutia ufumbuzi changamoto hizo ili kuondokana na  malalamiko.

 

Aidha,   aliitaka wizara hiyo kujikita katika suala la kusomesha na kuwaendeleza  wafanyakazi wake katika nyanja tofauti, ikiwemo za injinia na nyengine zenye upungufu ili waweze kufanyakazi kwa ufanisi.

 

Alisema kuna umuhimu wa kuwa na program maalum ya mafunzo , itakayotoa fursa kwa wafanyakazi kusoma ndani na nje ya nchi, hatua aliyobainisha itaiwezesha wizara kuwa na wataalamu wa kutosha katika kipindi kifupi.

 

Sambamba na hilo Dk. Shein alisisitiza umuhimu wa kufanya Tafiti mbali mbali , ikiwa ni hatua muafaka katika kuzipatia ufumbuzi changamoto mbali mbali zinazojitokeza.

 

Rais Dk. Shein aliutaka Uongozi wa Wizara hiyo kuhakikisha huduma zote za Maabara zinafanyika Ndani ya Hospitali za Serikali badala ya kufanyika Taasisi za Nje, kwa kigezo kuwa Serikali imekuwa ikitenga kiwango kikubwa cha Fedha na kubainisha kuwa huduma za Maabara ndio msingi wa Matibabu.

 

Aliushauri Uongozi wa Wizara hiyo kuendleea kuviimarisha vituo vya Afya , hususan vile vilioko Vijijini Kisiwani Pemba kwa kuvipatia Nyenzo, vifaa tiba na dawa, ili Wagonjwa wasikimbilie Hospitali ya Abdalla Mzee.

 

Aidha, aliipongeza Wizara hiyo kwa juhudi kubwa inazoendelea kuchukuwa katika kukabiliana na Ugonjwa wa Malaria, sambamba na kupunguza kiwango cha maambukizi ya Virusi vya Ukimwi kutoka asilimia 0.6 hadi kufikia asilimia 0.4.

 

Vile vile aliipongeza Wizara hiyo kwa kuandaa mpango mzuri wa taarifa yake, pamoja na hatua mbali mbali ilizozichukuwa kuimarisha huduma za Afya hapa Nchini.

 

Nae, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Dk. Abdulhamid Yahya Mzee aliupongeza Uongozi wa Wizara ya Afya kwa kuandaa vyema Taarifa hiyo ya utekelezaji.

 

Aidha, aumeutaka uongozi huo kufanya juhudi kukiimarisha Kitengo cha Mifupa katika Hospitali kuu ya Mnazi mmoja, ikizingatiwa mahitaji makubwa yaliopo kutokana na kuwepo ongezeko kubwa la Ajali za barabarani hapa nchini.

 

Mapema, Waziri wa Wizara Afya Hamad Rashid Mohamed akiwasilisha muhtasari wa utekelezaji wa mpango kazi wa Wizara hiyo, alisema katika kipindi hicho Wizara ilipanga kutumia zaidi ya shilingi bilioni 57.8 , kati yake shilingi bilioni 47.8 kwa ajili ya Idara na Taasisi zilizozomo ndani ya Wizara hiyo na shilingi bilioni 9.9 kwa ajili ya Hospitali ya Mnazimmoja.

 

Alisema Wizara ilipanga kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 4.6 kutoka vyanzo mbali mbali vya mapato ili kuchangia mfuko mkuu wa Serikali.

 

Alisema katika kipindi hicho Wizara hiyo imefanikiwa kutekeleza shughuli mbali mbali kwa mafanikio makubwa ikiwemo ununuzi wa dawa (shilingi bilioni nane), hivyo kuwezesha upatikanaji wa dawa muhimu katika vituo vya afya na hospitali kwa asilimia 90.

 

Aidha, alisema katika kipindi hicho Gharama za Usafirishaji wa Wagonjwa Nje ya Nchi zilipungua kutoka shilingi 341,292,993 hadi  kufikia shilingi 32,186,488 .

 

Waziri Rashid alisema  Wizara ilifanikiwa kuajiri Wafanyakazi 479, ikiwemo Madaktari , Wauguzi, Fundi  Sanifu Maabara na wataalamu wengine.

 

Alisema kupatikana kwa mashine ya CT scan mpya katika Hospital ya Mnazimmoja kutapunguza mrundikano wa  Wagonjwa  wanaosubiri  huduma hiyo.

 

Kuhusiana na uimarishaji wa  Miundombinu na Majengo, Waziri huyo alisema  ujenzi wa Bohari kuu Kisiwani Pemba unaendelea vizuri na unategemewa kukamilika ifikapo Mwezi  April, mwaka huu.

 

Alisema miongoni mwa changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa mpango huo ni pamoja na  mabadiliko ya ushuru kutoka Mamlaka ya kukusaya ushuru Tanzania (TRA), ambayo kwa kiasi kikubwa umeathiri Usafirishaji wa Dawa muhimu kutoka Msd  kwenda Bohari ya Dawa (Cms).

 

Nae, Mshauri wa Waziri katika Wizara hiyo,Nd .Mohamed Saleh Jidawi, alipongeza juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, chini ya Uongozi wa Rais Dk. Ali Mohamed Shein katika kuimarisha huduma za Afya Nchini.

 

 

 

 

 

 

 

WAZIRI ZUNGU AMEAHIDI KUSHUGHULIKIA ATHARI ZA KIMAZINGIRA ZITAKAZO JITOKEZA KWA UNGUJA NA PEMBA.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mh. Mussa Azan Zungu ameahidi kuteua Wataalamu maalum wa masuala ya kimazingira watakaopewa jukumu la kuangalia athari za Mazingira zinazoendelea kujitokeza katika Maeneo tofauti ya Visiwa vya Unguja na Pemba.

Alisema hatua hiyo ikiwa ni Jukumu la Ofisi yake imekuja kuafuatia Maeneo mengi hasa zile Sehemu zilizo Pembezoni mwa Barahi ya Hindi kukumbwa na changamoto mbali mbali za kimazingira ikiwemo mmong’onyoko wa Ardhi.

Mh. Mussa Azan Zungu alitoa ahadi hiyo wakati wa mazungumzo yake na Makamu wa Pili wa Rais wa  Zanzibar  Balozi  Seif  Ali Iddi   Vuga  Mjini  Zanzibar alipofika kujitambulisha rasmi baada ya kuteuliwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania  Dr. John Pombe Magufuli kushika wadhifa huo.

Alisema Visiwa vikubwa na hata vile vidogo ni sehemu muhimu zinazopaswa wakati wote kushughulikiwa na kuangaliwa kwa umakini mkubwa kulingana na maumbile yake ya kuzunguukwa na maji sehemu zote ili kulinda mazingira yake licha ya mabadiliko ya tabia Nchi yanayoikumba Dunia hivi sasa.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira  alimuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba atapanga Ziara maalum ya kuangalia hali ya Mazingira katika maeneo ya Zanzibar kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar inayoratibu na kusimamia mambo yote ya Muungano na mazingira kwa upande wa Zanzibar.

Mh. Zungu aliupongeza Uongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  Dr. Ali Mohamed Shein akisaidiwa na Makamu wake Balozi Seif Ali Iddi kwa usimamizi wao makini wa kuwaletea maendeleo Wananchi wa Visiwa vya Unguja na Pemba.

Naye kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh.Mohamed  Aboud  Mohamed alimpongeza Mwenza wake kwa upande wa Muungano kwa Uteuzi aliopewa na kumuahidi milango iko wazi wakati wote katika kuona Jukumu alilokabidhiwa analisimamia vyema kwa upande wa Zanzibar.

Waziri Aboud alisema yapo mambo mengi yanayoendelea kushirikisha Viongozi wa pande zote mbili za Muungano ambayo Waziri Zungu atapaswa kupewa Ushirikiano wa kina ili kutekeleza jukumu lake hasa vile vikao vya Wataalamu, Watendaji Waandamizi, Mawaziri na  Viongozi wa juu wa pande hizo mbili wanaounda kamati ya pamoja na Muungano.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi  Seif Ali Iddi alisema Zanzibar kwa kiasi kikubwa imefaidika sana na uwepo wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar licha ya Wananchi wa pande hizo mbili kuwa na udugu wa damu kwa Karne nyingi zilizopita kabla ya Muungano huo.

Balozi Seif alimueleza Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira kwamba zipo fursa nyingi zinazoendelea kuwafaidisha  Wananchi wa Zanzibar ndani ya Ardhi yaJamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa upande wa Bara.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alizitaja baadhi ya fursa hizo kuwa ni pamona na Sekta ya Biashara na Ardhi inayowapa nafasi pana Wananchi wa Zanzibar walioamua kuishi Bara kuendeleza shughuli zao za uwekezji katika masuala ya kilimo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais  Muungano na Mazingira Mh. Mussa Azan Zungu alikuwepo Zanzibar kujitambulisha Rasmi baada ya kuteuliwa kushika nafasi hiyo iliyoachwa na Mh. George Simba Chawene aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani.

 

Recent Comments by Wardat Mohd

No comments by Wardat Mohd yet.

error: Content is protected !!