Recent Posts by Wardat Mohd

DK. SHEIN AMEAGWA SUZA

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein , amelitaka Baraza la Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA) kuendelea kushirikiana na kuongeza bidii na ubunifu katika kuiendeleza Programu ya ufundishaji wa Kiswahili ili kufikia dhamira ya kuifanya SUZA kuwa ‘Oxford ya Kiswahili’.

Dk. Shein ambae pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar  (SUZA) ametoa rai hiyo katika hafla ya kuagwa, baada ya kukiongoza chuo hicho kwa miaka kumi,  hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Dk. Ali Mohamed Shein Tunguu, Mkoa wa Kusini Unguja.

Amesema ni vigumu kuzungumzia historia na maendeleo ya Kiswahili bila kuzungumzia historia na maendeleo ya Kiutamaduni wa Zanzibar, huku  akibainisha kuwa  Zanzibar ni nchi ya Kiswahili kinachozungumzwa kwa ufasaha katika maeneo ya mjini.

Alisema watu wengi huridhika kupata tafsiri ya maneno kutoka makamusi ya Kiingereza kutoka ‘Oxford’ kuliko makamusi mengine duniani, jambo ambalo linaweza kufikiwa nchini kwa kuweKa nguvu katika kuikuza na kuiendeleza lugha hiyo.

Aidha, alihimiza umuhimu wa kuimarisha skuli ya Kiswahili na lugha za kigeni ili kuifanya Zanzibar kuwa ‘Centre of Exellence’.

Alieleza kuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki imefungua kituo cha Kiswahili katika eneo la Gymkhana hapa Zanzibar, hivyo ni vyema SUZA ikachangamkia jambo hilo na kuwa kituo cha Kiswahili.

Dk. Shein alisema ni jambo la kufurahisha hivi sasa Zanzibar kuwa na Vyuo vikuu vitatu ambavyo kwa wastani hutoa wahitimu 3,000 kila mwaka na kubainisha umuhimu wa Wazanzibari kusoma elimu ya juu hapa nchini, kwani itamuwezesha mhitimu kufahamu changamoto ziliopo na jinsi ya kuisaidia jamii.

Akigusia mafanikio ya SUZA katika kipindi cha miaka kumi (10) ya uongozi wake, Dk. Shein alisema katika kuhakikisha nchi inajitosheleza kwa wataalamu, imeanzisha fani mbali mbali ili kwenda sambamba na mahitaji.

Alisema katika kipindi hicho kuna mafanikio makubwa ya kielimu yaliofikiwa kupitia SUZA , ikiwemo uanzishaji wa Skuli ya Afya na Sayansi za Tiba pamoja na mafunzo ya Udaktari (doctor of Medicine), mafunzo yalioanza mwaka 2017/2018 na wanafunzi 25 kufaulu pamoja na wengine 48 waliofanikiwa kumaliza masomo yao mwaka 2018/2019.

Alisema SUZA imefanikiwa kuanzisha mafunzo ya shahada ya kwanza ya Udaktari wa meno mwaka 2019/2020 ambapo jumla ya wanafunzi sita wanaendelea vizuri na masomo hayo.

Rais Dk. Shein alisema jitihada za kusomesha madaktari ndani na nje ya nchi zimewezesha kuongeza idadi ya madaktari na watumishi wengine wa afya nchini, akibainishwa kuwepo uwiano wa madaktari na watu wanaowahudumia.

Alisema hivi sasa Daktari mmoja anawahudumia watu 6,276 kutoka wastani wa daktari mmoja aliekuwa akiwahudumia watu 31,838 mnamo mwaka  2010.

Alisema lengo hilo linaendana na Manifesto ya Chama cha Afro Shirazi pamoja na kiwango kilichowekwa na Shirika la Afya Duniani kwa nchi zinazoendelea cha daktari mmoja kuwahudumia watu 10,000.

Alieleza kuwa katika kipindi cha miaka kumi ya Uongozi wake, chuo hicho kimefanikiwa kupata Ithibati kamili (full Accreditation) ya Tume  ya Vyuo vikuu Tanzania (TCU) .

Aidha, alisema Serikali ilifanya uamuzi wa kuziunganisha na SUZA taasisi mbali mbali, ikiwemo Chuo cha Utawala wa Fedha Chwaka, Chuo cha Kilimo Kizimbani, Chuo cha Habari Kilimani, Chuo ca Afya Mbweni pamoja na Chuo cha Utalii Maruhubi, kwa lengo la kuinua hadhi na kiwango cha elimu inayotolewa na taasisi za elimu ya juu.

Hata hivyo alisema wakati vyuo hivyo vinaunganishwa na SUZA wako watu walioonyesha kutokuelewa, hivyo akatumia fursa hiyo kuipongeza Kamati maalum iliyoundwa kushauri na kutoa mapendekezo ya kuunganisha vyuo hivyo.

Mapema, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Riziki Pembe Juma alitoa shukurani kwa Mkuu wa Chuo hicho kwa juhudi kubwa za kusimamia mendeleo ya chuo hicho pamoja na hatua za kuhamasisha elimu ya juu kwa  akinamama, hivyo kuongeza ufaulu kwa jinsia hiyo kwa kiwango cha juu.

Nae, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo hicho, Said Bakari Jecha alisema katika kipindi cha miaka kumi ya uongozi wa Dk. Shein, SUZA imepata mafanikio makubwa na ya haraka na kufanikiwa kupata umarufu mkubwa wakati ambapo vyuo vingi Duniani hupata mafanikio kama hayo baada ya  miaka mingi kupita.

Akisoma maelezo hayo kwa niaba yake, mwanatalaamu Mwita Mgeni alisema   Chuo hicho kimetekeleza kikamilifu Ilani ya CCM , ambapo pamoja na mambo mengine kwa zaidi ya asilimia themanini ya wanafunzi wanasoma kupitia  mikopo inayotolewa serikalini.

Aidha, Makamo Mwenyekiti wa Chuo hicho Dk. Zakia Mohamed Abubakar alisema katika kipindi cha Uongozi wake, Dk. Shein alifanya juhudi kubwa  kukiendeleza chuo hicho kiasi cha kupata mafanikio ya kupigiwa mfano, ikiwemo kukuza ubora wa elimu kufuatia hatua za uimarishaji wa miundo mbinu ya elimu, nguvu kazi pamoja na upatikanaji wa maslahi bora.

Alisema kutokana na msukumo mkubwa wa Dk. Shein, chuo hicho kimeweza kuanzisha ‘SUZA TV’ iliyoanzishwa kwa lengo la kutoa taaluma kwa wanafunzi wa Sekondari, hususan wanaosoma masomo ya Sayansi na Hisabati.

Katika hatua nyengine, Mwanataaluma Ameir Mohamed Makame, akisoma risala ya wanataaluma, alitoa pongezi kwa Dk. Shein kwa mchango mkubwa wa kukiendeleza chuo hicho ndani ya kipindi cha miaka kumi ya uongozi wake kwa kuangalia maslahi yao pamoja na kuwepo uwazi katika suala la upandishaji vyeo.

Alisema katika kipindi hicho wanataaluma walipata fursa za masomo ndani na nje ya nchi pamoja na kupata  nyadhifa za kufanyakazi katika maeneo mbali mbali.

Alisema Jumuiya ya wanataaluma inampongeza kwa dhati Dk. Shein kwa hatua ya kuwaamini na kuwateua wanataaluma wanawake kushika nyadhifa za kuiongoza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali pamoja chuo hicho.

Hata hivyo, mwantaaluma huyo alisema bado kada hiyo inakabiliwa na changamoto mbali mbali, ikiwemo ya kuwepo idadi ndogo ya wanataaluma katika kiwango cha shahada ya Uzamivu.

Aidha, aleleza kuwa wanataaluma wa SUZA wanakabiliwa na kuwepo kwa tofauti kubwa ya maslahi (mishahara) kati yao na wenzao wanaovitumikia vyuo vikuu mbali mbali Tanzania Bara.

Ameir alieleza matumaini makubwa waliyonayo wanataaluma wa SUZA ya kuwa Mkuu wa Chuo hicho ajae atayapatia ufumbuzi masuala hayo ili kuwatia moyo wanataaluma.

Katika hafla hiyo, viongozi mbali mbali wa Serikali walihudhuria,akiwemo Makamo wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania mstaafu,  Dk. Mohamed Gharib Bilali, Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, Mgombea wa Urais kupitia CCM Dk. Hussein Ali Mwinyi, Mawaziri pamoja na wake wa Viongozi wakuu.

 

 

 

 

 

DK. MWINYI AKUTANA NA WAUMINI WA DINI YA KIKRISTO KUZUNGUMZA

Mgombea  wa  Urais wa  Zanzibar  kwa  Tiketi  ya  CCM  Dr.Husein  Ali  Mwinyi  Amesema  njia  bora  ya   kuwatumikia   Wananchi   ni  kukutana   nao   jambo  ambalo  ataliwekea   utaratibu  maalum  katika  Serikali   atakayoingoiza   baada  ya Uchaguzi  .

Amesema  kuwa   anaamini  utaratibu  huo   ni  sahihi   na  utasaidia  kumaliza   matatizo   yaliomo  katika   makundi  mbali mbali  ya  kijamii kwani  kutatoa  nafasi  ya   Kiongozi   kuyatambua  haraka   mambo  yanayowakwa za  Wanchi  katika  maisha  yao  ya  kila  siku.

Dr .Hussein ametoa  tamko  hilo  wakati  Akizungumza  na  Waumini  wa   Madhehebu  ya  Kikiristo  katika  Ukumbi  wa  Idrissa  Abdul Wakil   ikiwa  ni  muendelezo  wa   utaratibu  wa   kuomba  kura  kwa   makundi  tofaiuti  kuelekea  Uchaguzi  Mkuu.

Amewahakikishia  Waumini  wa  Dini  ya  Kikristo  kuwa   ana  dhamira  ya   dhati   ya   kumaliza   aina  zote  za  Ubaguzi   ikiwemo   za  Udini.  Kabila  .  Jinsia   au  eneo  mtu  analotoka    na kusimamia  misingi  ya  haki    katika   kuliongoza Taifa   .

Askofu  wa  Kanisa  Katoliki  Dayosisi  ya  Zanzibar   Askofu  Augostino  Shao  amemuomba   Mgonbea  Dr.Hussein   kusimamia  haki   kwani   ndio  inayolinyanyua   Taifa    na  kwamba   Waumini  wa  Kikirsto   wana  matumaini  makubwa  na  Serikali   atakayiongoza.

DK. MAGUFULI AMTEMBELEA MGONJWA ALIOJERUHIWA KWA MAPANGA PEMBA

Mgombea Urais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi Dk.John Pombe Magufuli awasili Zanzibar na kumjulia hali Mgojwa aliyeshambuliwa kwa Mapanga Msikitini hivi karibuni huko Kisiwani Pemba.

Mapema baada ya kuwasili Dk.Magufuli amepokelewa na Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Dk.Bashiru Ali, Naibu Katibu wa CCM Zanzibar Dk.Abdallah Juma Sadalla na Katibu wa Idara ya Itikadi na Uwenezi CCM Zanzibar Nd.Catherene Peter Nao

Aidha Dk.Magufuli amevitaka Vyombo vya Ulinzi na usalama kuhakikisha vinawachukuliwa hatua wale wote waliohusika na kitendo hicho.

Dk.Magufuli kesho Anatarajia kuendelea na Kampeni kwa kufanya Mkutano wa Chama hicho katika Viwanja vya Mnazi Mmoja.

DK. SHEIN AFUNGUA BARABARA YA FUONI KOMBENI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa mafanikio yanayoendelea kupatikana katika sekta ya miundombinu ni kielelezo cha kuyaendeleza Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya  Januari 12, 1964 kwa shabaha ile ile ya kuwakomboa wananchi ili waweze kujiletea maendeleo ya uhakika.

Dk. Shein aliyasema hayo leo huko Kombeni wakati akiwahutubia wananchi katika hafla ya uzinduzi wa barabara ya Kombeni hadi Fuoni iliyokwenda sambamba na uzinduzi wa barabara ya Koani hadi Jumbi.

Katika maelezo yake, Rais Dk. Shein alisema kuwa Mapinduzi ndiyo yaliyokomboa kila kitu ikiwa ni pakoja na ujenzi wa barabara kwani kila kitu cha maendeleo katika visiwa vya Unguja na Pemba kilianza mara baada ya Mapinduzi ya mwaka 1964.

Akieleza historia ya miundombinu ya barabara hapa Zanzibar, Rais Dk. Shein alisema kuwa Idara ya Kazi ya Barabara (PWD) ndio iliyokuwa ikifanya kazi ya barabara mpya pamoja na zile za zamani mara baada ya Mapinduzi na baadae ikabadilika na kuitwa Idara ya Ujenzi na Utengenezaji wa Barabara (UUB).

Rais Dk. Shein alisema kuwa hatua ya ujenzi wa barabara hizo pia, ni miongoni mwa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015-2020 na kutumia fusra hiyo kuipongeza Wizara ya Ujenzi, Mawasilino na Usafirishaji kwa kusaidia katika utekelezaji wa Ilani hiyo.

Alisema kuwa shughuli nyingi za kiuchumi na kijamii zinategemea miundombinu ya barabara zilizo bora ambapo pia, juhudi za kuimarisha kilimo,utalii,uwezeshaji na sekta zote za kiuchumi kunahitaji kuwepo kwa barabara za kisasa.

Aliongeza kuwa kuimarika kwa miundombinu ya barabara ndio chachu ya maendeleo na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imedhamiria kwa kasi sana kuimarisha miundombinu ya barabara ili itoe msukumo katika jitihada za kuendeleza sekta nyengine.

Rais Dk. Shein alitoa pongezi kwa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji kwa kuendelea kuitekeleza vizuri Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM ya mwaka 2015-2020 na kusimamia ahadi alizozitoa katika nyakati mbali mbali za uongozi wake huku akiipongeza Kampuni ya  “China Civil Engineering Construction Corporation” (CCECC).

“Nimefarajika kuona kwamba  tumefanikisha kumalizika kwa barabara hizi tatu nilizoahidi kuzimaliza kabla ya muda wangu wa uongozi kwa nafasi ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kumalizika ambazo ni Fuoni-Kombeni, Koani-Jumbi kwa Unguja na Ole-Kengeja kwa Pemba ”alisema Dk. Shein.

Rais Dk. Shein alitumia fursa hiyo kwa kusema kuwa ujenzi wa barabara ya Ole-Kengeja nao umeshamaliza na imani yake atakapokwenda Pemba wiki ijayo ataizindua ambayo ina urefu wa kilomita 35 huku akieleza kuwa kipande cha barabara cha kutoka Bububu hadi kwa Nyanya nacho tayari kimeshakamilika.

Aidha, Rais Dk. Shein alisema kuwa faida zinazopatikana katika uendelezeji wa miundombinu ya barabara zinatokana na uamuzi uliochukuliwa na Serikali wa kununua vifaa vipya vya ujenzi wa barabara vilivyogharimu jumla ya TZS bilioni 14.

Rais Dk. Shein pia, alitumia fursa hiyo kuihimiza Wakala wa Barabara kuwa na mipango imara ya kuzifanyia ukarabati barabara huku akiwataka wafanyakazi wa Wakala wa Barabara kutofanya kazi kwa mazoea na badala yake wabadilike kwa kwenda na wakati uliopo kwani tayari Serikali imo katika mchakato wa kuwaongezea mishahara ili walipwe vizuri.

Hivyo, Rais Dk. Shein alieleza kuwa Serikali itaendelea kujenga barabara mpya katika maeneo yanayohitajika ili kuimarisha shughuli za kiuchumi na kijamii.

Alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuzifanyia matengenezo barabara za ndani ya miji kwa kuzipanua na kujenga barabara mpya ambapo mipango hiyo ni muhimu katika juhudi za kupambana na tatizo la msongamano wa gari ndani ya miji.

Nae Waziri wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Dk. Sira Ubwa Mamboya alisema kuwa uzinduzi wa barabara hizo ni mafanikio makubwa chini ya uongozi wa Rais Dk. Shein.

Alisema kuwa hiyo ni hatua kubwa ya maendeleo iliyofikiwa katika uongozi wa Rais Dk. Shein wa Awamu ya Saba ambapo zaidi ya kilomita 300 za barabara  zimejengwa katika maeneo mbali mbali ya Unguja na Pemba.

Alifahamisha kuwa ujenzi wa barabara hizo ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha miundombinu ya barabara kwa ajili ya kuimarisha huduma za usafiri na usafirishaji mjini na vijijini kwa lengo la kuwaondoshea wananchi shida ya usafiri ambapo Wizara yake imepata mafanikio makubwa katika kuimarisha miundombinu ya barabara Unguja na Pemba.

Mapema Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji, Mustafa Aboud Jumbe alisema kuwa ujenzi wa barabara ya Kombeni hadi Fuoni yenye urefu wa kilomita 8.5 na Koani Jumbi kilomita 6.3 iliyopo Wilaya ya Kati Unguja.

Alisema kuwa hizo ni miongoni mwa jitihada zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tokea Mapinduzi matukufu ya mwaka 1964 ya kujenga ustawi wa wananchi wake kwa kuimarisha na kuendeleza miundombinu ya barabara za mjini na vijijini Unguja na Pemba.

Aidha, alisema kuwa ujenzi huo ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020 kama ilivyoelezwa kwenye ukurasa wa 138 kifungu cha 83, kifungu kidogo cha b na c, Dira ya Maendeleo (Vision 2020), MKUZA III, Sera ya Taifa ya Usafiri pamoja na Mpango Mkuu wa Usafiri Zanzibar.

Mradi wa ujenzi wa barabara hio ya Kombeni hadi Fuoni  yenye urefu wa kilomita 8.5 ni miongoni mwa barabara nne ikiwemo ile ya Bububu, Chuini kuelekea Mahonda hadi Mkokotoni yenye urefu wa kilomita 31, Pale-Kiongele yenye kilomita 4.61, Matemwe-Muyuni Kilomita 7.58 Bububu Polisi hadi Chuini yenye  urefu wa kilomita 2.8.

Aliongeza kuwa barabara zote hizo zimekamilika kwa kiwango cha lami na kazi zinazoendelea ni ujenzi wa misingi ya maji ya mvua pembezoni mwa barabara pamoja na kuweka alama za usalama za barabarani pamoja na kujengwa kwa vizuizi kwenye baadhi ya sehemu ya miinuko..

Alisema kuwa ujenzi wa barabara hizo umetekelezwa kwa kutumia fedha za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Mkopo wa fedha kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika ADB.

Alisema kuwa ujenzi wa barabara ya Fuoni hadi Kombeni ulianza tarehe 17 Agosti 2019 na ulitarajiwa kukamilika tarehe 30 mwezi Septemba mwaka huu ambapo mradi huo ulitiliana saini tarehe 8 Novemba mwaka 2017 baina ya Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji na Mjenzi ambaye ni Kampuni ya ‘China Civil Engineering Construction Corporation’ (CCECC), kwa thamani ya TZS Bilioni 71.9 kwa barabara zote 4 ambapo kwa barabara ya Fuoni – Kombeni iligharimu TZS Bilioni 9.1 na mchango wa SMZ ulikuwa ni TZS Bilioni 3.120.

Aliongeza kuwa Msimamizi wa Mradi ni Kampuni ya H.P Gauff Ingenieure GmbH ya Ujerumani ambae alifungiana Mkataba na Wizara hiyo tarehe 15 Julai 2017 kwa thamani ya Euro Milioni 1.5. ikiwa ni sehemu ya mkopo wa Benki ya Maendeleo ya Afrika ADB.

Kwa upande wa barabara ya Jumbi hadi Koani yenye urefu wa kilomita 6.3 Katibu Mkuu huyo alisema kuwa ujenzi huo umegharamiwa kwa pamoja kati ya SMZ pamoja na mkopo wa Benki ya BADEA kwa gharama ya TZS bilioni 5. 690 ambapo SMZ imechangia TZS bilioni 1.95 ambapo kazi ya ujenzi imefanywa na Kampuni ya MECCO ya Dar-es-Salaam na kusimamiwa na Wakala wa Barabara huku akisema kuwa barabara ya Kizimbani hadi kiboje matayarisho yake tayari yameanza.

Katibu Mkuu huyo alitumia fursa hiyo kumshukuru na kumpongeza Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ambaye pia ni Mgombea wa Urais wa Zanzibar kupitia (CCM) Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa kusaidia kuruhusu kujenga barabara hiyo iliyopita sehemu ya Jeshi bila ya fidia na malipo yoyote  pamoja na kutoa shukurani kwa  uongozi na wafanyakazi wote wa Wizara hiyo.

Viongozi mbali mbali walihudhuria akiwemo Makamu wa Pili wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeid Ali Maulid, Mawaziri na viongozi mbali mbali wa Serikali pamoja na viongozi wa vyama vya siasa pamoja na wananchi wa maeneo zilimopita barabara hizo.

Rais Dk. Shein akiwa ameambatana na viongozi pamoja na wananchi waliohudhuria katika hafla hiyo walipata fursa ya kuzitembelea barabara hizo zote mbili ambapo pia, aliifungua kwa kuweka jiwe la msingi na kukata utepe barabara ya Jumbi hadi Koani hapo katika eneo la Jumbi bango la Mkoa.

Recent Comments by Wardat Mohd

No comments by Wardat Mohd yet.