Recent Posts by TALHA FERUZ

UNDP YAIPONGEZA ZANZIBAR KWA KASI YA UKUAJI WA UCHUMI

Pongezi hizo zimetolewa leo na Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Miradi ya Maendeleo (UNDP) nchini Tanzania Christine Musisi wakati alipokuwa na mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein.

 

Katika mazungumzo hayo, Mwakilishi huyo Mkaazi wa (UNDP), alitoa pongezi hizo kwa Rais Dk. Shein na Serikali anayoiongoza kutokana na kasi kubwa ya ukuaji uchumi sambamba na hatua kubwa za maendeleo zilizofikiwa Zanzibar.

 

Mwakilishi huyo Mkaazi wa Umoja wa Mataifa alieleza kuwa Katika kipindi cha uongozi wa Rais Dk. Shein Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limeona mageuzi makubwa ya kiuchumi na kimaendeleo sambamba na kuimarika kwa utawala Bora.

 

Aliongeza kuwa Shirika la Umoja wa Maifa linaloshughulikia Miradi ya Maendeleo (UNDP) litaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuendeleza na kuimarisha miradi mbali mbali ya maendeleo ili Zanzibar izidi kupata mafanikio.

 

Aidha, Mwakilishi huyo Mkaazi wa (UNDP), alieleza kuwa katika uongozi wa Rais Dk. Shein Shirika hilo limeweza kushuhudia mafanikio makubwa ya kiimaendeleo ikiwa ni pamoja na juhudi za kupamba na umasikini na kukuza uchumi chini ya Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini Zanzibar (MKUZA) ukiwemo (MKUZA II) na kuahidi kuuunga mkono (MKUZAIII).

 

Alieleza kuwa huduma za kijamii zimezidi kuimarika zikiwemo huduma za afya, elimu, maji safi na salama pamoja na huduma nyenginezo sambamba na juhudi kubwa zilizofanyika katika kupambana na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI.

 

Hivyo, Kiongozi huyo alieleza kuwa (UNDP), iko tayari kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha na kuendeleza miradi ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kusaidia vipaumbele vyote vilivyowekwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

 

Nae Rais Dk. Shein kwa upande wake alieleza kuwa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Miradi ya Maendeleo (UNDP), ni miongoni mwa Mashirika ya Umoja wa Mataifa (UN) ambalo limekuwa na mashirikiano na kuweza kuiunga mkono Zanzibar kwa muda mrefu.

 

Hivyo, Rais Dk. Shein alitumia fursa hiyo kulipongeza Shirika hilo na kueleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na wananchi wake wanafarajika na juhudi kubwa inazozichukua Shirika hilo katika kuhakikisha Zanzibar inazidi kupata mafanikio ya kiuchumi, kijamii na kisiasa.

 

Rais Dk. Shein aliongeza kuwa uchumi wa Zanzibar umezidi kuimarika kutokana na mashirikiano makubwa kati ya uongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na wananchi wake bila ya kuwasahau washirika wa Maendeleo kama vile Shirika hilo la Umoja wa Mataifa (UNDP).

 

Aidha, Rais Dk. Shein alieleza juhudi na mikakati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha na kukuza uchumi wake ikiwa ni pamoja na kuiimarisha sekta ya uwekezaji, viwanda sambamba na kuiendeleza na kuiimarisha sekta ya utalii ambayo inachangia kwa asilimia 27 ya Pato la Taifa la Zanzibar na asilimia 80 ya fedha za kigeni.

 

Katika mazungumzo hayo, Rais Dk. Shein alieleza kuwa sekta ya utalii imeweza kuimarika kwa kiasi kikubwa ambapo pia, juhudi za makusudi zinaendelea kuchukuliwa katika kuiendeleza sekta hiyo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Hoteli kubwa za kitalii pamoja na kuviimarisha vivutio vlivyopo.

 

Kwa upande wa uwekezaji, Rais Dk. Shein alimueleza Mwakilsihi Mkaazi huyo wa (UNDP) kuwa Mamlaka ya Ukuzaji wa Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA), imekuwa ikifanya kazi kubwa katika kuhakikisha maeneo huru ya Uchumi yanaimarika na yanafikia yale malengo yaliyowekwa ambapo kwa upande wa Unguja alieleza kuwa eneo la Fumba tayari limeanza kutumika kiuwekezaji huku juhudi zikichukuliwa kwa upande wa eneo la Micheweni huko Pemba.

 

Pamoja na hayo, Rais Dk. Shein alieleza kuwa huduma za  kijamii zimezidi kuimarika na miradi yote ya maendeleo imeendelea kupata mafanikio na kueleza kuwa huduma za afya kwa upande wa kupunguza vifo vya akina mama na watoto vimepungua kwa kiasi kikubwa.

 

Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein alisema kuwa juhudi za makusudi zinaendelea kuchukuliwa katika kuhakikisha Zanzibar inatekeleza azma ya Uchumi Bahari (Blue Economy), ikiwa ni pamoja na kuimarisha viwanda vidogo vidogo, kukuza sekta ya utalii, uvuvi pamoja na sekta nyenginezo.

COSOZA KUSADIA KUPATIKANA TAKWIMU SAHIHI ZA WASANII

 

Wasanii wanaweza kufanikiwa katika kazi zao kwa kuzisajili katika ofisi ya hatimiliki Zanzibar Cosoza hali itakayoisadia kupatikana takwimu sahihi za wasanii na kufuatilia utetezi wa kazi zao.

Kauli hiyo imetolewa na mkuu wa kitengo cha leseni  cosoza Muumini Mwinyi Mzee katika mkutano na viongozi wa   wasanii na wabunifu wa mkoa wa kaskazini unguja wa kujadili umuhimu wa kusajili kazi wasanii.

Amesema kazi ya msanii ikisajiliwa itaweza kusimamiwa na msanii kupata haki zake ikiwa kazi hiyo itatumika ndani au nje ya nchi.

Afisa usajili na kumbukumbu kutoka Cosoza ndg Iddi Makame Simai na mwanasheria kutoka kosoza Mwanaisha Mrisho Mwinyi wamesema usajili huo ni muhimu kwa vile ni mkombozi wa wasanii

Mwenyekiti wa umoja wa wasanii wilaya kaskazini "A" Unguja Hafidh Saleh amesema  mkutano huo umewasaidia kufahamu njia za kuimarisha sanaa zao ili ziwe sehemu ya ajira katika maisha yao.

 

 

WAGONJWA WA SUKARI WATAKIWA KUFUATA UTARATIBU WA VYAKULA WANAOPEWA NA WATAALAMU WA AFYA.

Mwakilishi wa Jimbo la Kiembe Samaki Mhe. Mahmoud Thabit Kombo amewaka wagonjwa wasukari kufuata utaratibu wa vyakula wanaopewa na wataamu wa afya ili kulinda afya zao.

Akizungumaza katika maadhimisho ya siku ya ugonjwa sukari Mhe. Mahmoud  amesema serikali kupitia wizara ya afya imeweka utaratibu wa kuwapatia huduma ya afya wagonjwa wa maradhi hayo ikiwemo kuwapatia dawa na maelekezo ya utumiaji wa vyakula jambo litasaidia kuimarisha afya zao.

Mratibu wa umoja wa wagonjwa wa sukari Bi Mkasi Mohamed amesema umefika wakati kwa Wananchi hasa Wazee kuitikia wito katika kupata huduma za matibabu zinazotolewa bure katika shehia zao.

Wananchi Mzee Juma Ali na Bi Asya Shaban wameiomba Serikali kuendelea kuwasaidia Wazee kwa kuwapa huduma mbali mbali huku wakiwashauri wananchi kuwa na tabia ya kuchunguza afya zao ili kupata matibabu mapema.

 

ZBS KUANZISHA UKAGUZI NA UTOAJI WA ALAMA ZA UBORA WA VIWANGO KWA VIFAA VYA UJENZI.

Naibu Mwenyekiti wa Bodi ya taasisi ya viwango Zanzibar ZBS Bi Khamisa Mmanga Makame amesema taasisi hiyo itaanzisha ukaguzi na utoaji wa alama za ubora wa viwango kwa vifaa vya ujenzi vinavyoingia na vinavyotengenezwa Visiwani  humu ili  kuimarisha sekta ya ujenzi

Akizungumza katika Semina ya mafunzo ya utengenezaji wa Matofali kwa Wakandarasi na Wamiliki wa Viwanda Bi Khamisa amesema kutokana na kukua kwa sekta ya ujenzi  taasisi hiyo imeamua kuelekeza nguvu zake katika sekta hiyo ili kuwa na Majengo imara.

Mkurugenzi wa ZBS amesema wameanza kuimarisha mifumo yao ya ukaguzi na utoaji wa viwango kwa bidhaa zinazozalishwa ndani ya Zanzibar ili ziweze kushindana katika soko la Kimataifa.

Washiriki wa semina hiyo wameitaka ZBS kushirikiana na Idara ya Misitu, Mazingira na wadau wa ujenzi katika kutatua matatizo katika sekta ya ujenzi ikiwemo upatikanaji wa Mchanga.

Muezeshaji katika semina hiyo Mhandisi Danford Semwenda amewataka wamiliki wa Viwanda vya matofali kuchukua tahadhari kwa wafanyakazi wao kwa kuwapa vifaa vya kinga kuepusha majanga.

 

Recent Comments by TALHA FERUZ

No comments by TALHA FERUZ yet.