Monthly Archives: April 2021

TANZANIA INAUNGANA NA MATAIFA MENGINE KATIKA KUKUZA MASHINDANO YA KUSOMA NA KUHIFADHI QUR-AN

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa inapendeza kuona Jamhuri ya Muungano wa Tanzania sasa inaungana na Mataifa mengine duniani katika kukuza na kuimarisha mashindano ya kusoma na kuhifadhi Qurani.

 Alhaj Dk. Mwinyi ameyasema hayo leo katika hafla ya mashindano ya 21 ya Qurani ya juu 30, yaliyofanyika katika uwanja wa Benjamin William Mkapa Jijini Dar-es-Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali pamoja na maelfu ya wananchi.

Katika hotuba yake, Rais Dk. Mwinyi aliwataka Watanzania kuona kuwa ushiriki wao katika mashindano hayo ni fursa adhimu ya kuitangaza Tanzania kama inavyofanya katika mashindano mengine ya Kitaifa inayoshiriki.

Alisema kuwa ni jambo jema na la kheri kushuhudia kwamba mashindano ya Kuhifadhi Qurani, kitabu kitukufu cha Mwenyezi Mungu yanazidi kupata nguvu na umaarufu duniani hivi sasa.

Aliongeza kuwa nchi mbali mbali zinaendelea kuandaa mashindano hayo kwa ngazi ya Kitaifa na Kimataifa huku akitumia fursa hiyo kuipongeza Taasisi ya Al-Hikma kwa kuandaa mashindano hayo.

Alhaj Dk. Mwinyi alisema kuwa Watanzania wa rika mbali mbali wamekuwa wakionesha umahiri mkubwa katika mashindano na kupeperusha bendera ya nchi yao Kimataifa, katika mataifa kadhaa ikiwemo Saud Arabia, Iran,Oman, Malaysia na nchi nyenginezo.

Hivyo, Alhaj Dk. Mwinyi alisisitiza kwamba ni vyema kwa madrasa za hapa nchini pamoja na taasisi nyengine za dini ya Kiislamu zikahakikisha kwamba zinawaandaa vizuri vijana wenye vipaji vya kuhifadhi Quarani ili pale wanaposhiriki waiwakilishe vyema Tanzania na warejee nyumbani wakiwa na zawadi na tunzo mbali mbali.

Aidha, Alhaj Dk. Mwinyi aliwapongeza washiriki wote wa mashindano hayo kwa kufikia hatua hiyo lakini aliwapongeza zaidi walimu na Masheikh waliowaandaa vijana hao waliofikia kiwango hicho.

Alhaj Dk. Mwinyi alotumia fursa hiyo kumuomba Mwenyezi Mungu awape fadhila nyingi na kheri walimu na Masheikh wote waliotoa mafunzo ya kitabu kitukufu cha Qurani hadi mafundisho yake yakaweza kufahamika.

Alisisitiza kwamba ni wajibu kwa Waumini wa Dini ya Kiislamu kuendelea kuisoma Qurani kwa hukumu zake na kuzingatia zaidi yale yanayoelekezwa ndani yake kwani inapatikana elimu kamili ya maisha yote ya mwanaadamu.

Pamoja na hayo, Alhaj Dk. Miwnyi aliwahimiza Waumin wa Dini ya Kiislamu kuzingatia mafunzo, maamrisho na makatazo yaliyomo katika kitabu Kitukufu cha Qurani ili kukuza ucha Mungu wao.

Alhaj Dk. Mwinyi alisema kwamba pamoja na kuwa washiriki wa mashindano hayo ni Waislamu shughuli hiyo ilihudhuriwa pia, na baadhi ya wasio kuwa waislamu jambo ambalo linaifanya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa tofauti na mataifa mengine.

“Huundio utamaduni mzuri ambao waasisi wa Taifa letu, wametujengea  na tumelelewa nao, watu wa dini na madhehebu tofauti tunaweza kuishi na kwua pamoja kwa kustahamiliana, kuvumiliana na kushirikiana hata katika masuala yanayohusu dini mbali mbali zinazofuatwa na Watanzania”,alisema Alhaj Dk. Mwinyi.

Katika hotuba yake hiyo, Alhaj Dk. Mwinyi alisema kuwa Marehemu Dk. John Pombe Magufuli alionesha njia kwa mifano katika kujenga ustahamilivu na kuwataka Watazania kuishi kwa upendo na umoja bila ya kujali tofauti zao ambapo katika mashindano ya mwaka 2019 yeye mwenyewe alikuwa mgeni rasmi.

Mapema Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa alitoa salamu za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan kwa wale wote walioshiriki katika mashindano hayo makubwa barani Afrika.

Nae Rais wa Taasisi ya Al- Hikma Foundation Sheikh Sharif Abdulqadir akimkaribisha Alhaj Dk. Mwinyi alieleza jinsi taasisi hiyo inavyojishughulisha na shughuli hizokwa muda mrefu na kuwapongeza Watanzania kwa kuunga mkono.

Mufti Mkuu wa Tanzania Shekh Abubakar Bin Zubeir Bin Ally alisema kwamba mashindano hayo ya Qurani yameifanya Tanzania izidi kutajika duniani kote na kuwapongeza washiriki wote wa mashindano hayo.

Sheikh Alhad Mussa Salum, Sheikh Mkuu wa Dar-es-Salaam aliwataka Watanzania wampende Rais wa Jamhuri ya Muunganowa Tanzania Samia Suluhu Hassan kama walivyokuwa wakimpenda Hayati Rais Magufuli.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Al-Hikma Sheikh Nurdin Kishki alitoa pongezi kwa Serikali zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuunga mkono mashindano hayo huku akiipongeza Benki ya PBZ Islamic kwa kuwa mdhanini Mkuu wa mashindano hayo pamoja na wadhamini wengine.

Katika mashindano hayo, mshindi niJibrilaOmar Hassan kutoka Niger ambaye amejinyakulia TZS Milioni 20, Cheti cha ushiriki pamoja na vocha ya TZS milioni moja na mshindi wa Pili ni Hassan Ibrahim kutoka Sudan aliyepata milioni 12 na mshindi wa tatu ni Sangare Halid kutoa Ivory cost  aliyepata milioni 7.5 na mshindi wa nne ni Omar Abdallah Salim kutoka Tanzania Bara aliyepata zawadi ya TZS milioni 5 na wa tano ni Mustafa Ali kutoka Nigeria aliyepata TZS milioni tatu.

Viongozi mbali mbali walihudhuria katika mashindano hayo aliwemo Rais Mstaafu Alhaj Ali Hassan Mwinyi, Mawaziri, Mkuu wa Mkoa wa Dar-es-Salaam pamoja na viongozi wengine wa dini na Serikali wa ndani na nje ya Tanzania ambapo mashindano hayo yamezishirikisha nchi 21 za Afrika na kuwashirikisha washindanaji 23 kutoka nchi mbali bali za Afrika isipokuwa mshindanaji mmoja kutoka Senegal hakuweza kufika.

MASHINDANO MAKUU YA KUHIFADHI QUR-AN YA KITAIFA ZANZIBAR JUZUU 30

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla, amewataka Wazee na Walimu wa Madrasa Nchini, kuwaendeleza kielimu katika fani mbali mbali za dini na dunia, Wanafunzi waliohifadhi Qurani, ili kupata radhi zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu.

Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla ameyasema hayo katika hafla ya Mashindano Makuu ya kuhifadhi Quran ya Kitaifa Zanzibar ya juzuu 30 yaliyohitimishwa katika Masjid Jaamiu Zinjibaar, Mazizini Zanzibar.

Amesema kuwa wanafunzi waliopata fursa ya kuhifadhi Quran ni vyema kuandaliwa mazingira mazuri ya kielimu, ili wasiishie kushiriki mashindanoni na kupata zawadi, bali waandaliwe mfumo mzuri wa kuendelea na masomo akitolea mfano kujua tafsiri ya kile walichokihifadhi.

Akigusia suala la umuhimu wa kitabu cha Quran Mheshimiwa Hemed amesema ipo haja ya kuendelea kuisoma zaidi Quran hasa katika mwezi huu Mtukufu wa Ramadhan, ili kupata ujira mkubwa, akitolea mfano kuwa, mwenye kusoma quran, aajihakikishia uombezi siku ya kiama.

Amewausia  Wana Jumuiya na Walimu wa Vyuo vya Quran kwamba wasikate tamaa na mazingira magumu wanayofanyia Kazi kwani jukumu wanalolisimamia lina ujira mkubwa kwa Muumba wao ambaye hashindwi kuwashushia Rehema zake.

Mapema akitoa Taarifa ya Jumuiya ya kuhifadhi Quran Zanzibar Mwenyekiti wa Taasisi hiyo ya Kiislamu Mwanazuoni Sheikh Suleiman Omar {Maalim Sule} alisema Jumuiya hiyo iliyoasisiwa Mnamo Mwaka 1992 hivi sasa imeshatimiza miaka 28.

Maalim Suleiman alisema lengo la Jumuiya hiyo ni kusimamia ujenzi wa Maadili mema katika Kizazi cha Kiislamu katika kujikita zaidi kwenye Uhifadhi ya Kitabu Kitakatifu cha Quran ambapo kwa sasa zaidi ya Wanafunzi 300 wameshafanikiwa kukihifadhi moyoni Kitabu hicho.

Akitoa salamu Mmoja wa Waumini wanaoiunga mkono Jumuiya hiyo kwa kiwango kikubwa Mfanyabiashara Maarufu Nchini Sheikh Said Nasser Bopar alisema Waumini lazima washindane kwa nguvu na mali zao katika kuisimamia njia sahihi ya mwenyezi Mungu.

Matokeo ya Mashindano hayo ya kuhifadhi Quran yamemuwezesha Mwanafunzi Fahad Haji kushika nafasi ya kwanza kwa kupata alama 99 akizawadiwa shilingi Milioni 5,000,000/- na zawadi maalum.

Mshindi wa Pili alikuwa Mwanafunzi Abdull Nassir aliyepata alama 98 akikabidhiwa shilingi Milioni 4,000,000/- taslim wakati mshindi wa Tatu Shamis Maalim aliyepata alama 98 na kuzawadiwa shilingi Milioni 3,000,000/-.

Kwa upande wa Tashjii Tahqiq Mshindi wa kwanza alikuwa Mwanafunzi Rashid Hemed Rashid aliyeibuka na alama 100 na kuzawadiwa shilingi Milioni 2,500,000/-.