Daily Archives: November 12, 2020

DK. HUSSEIN MWINYI KUIJENGA ZANZIBAR MPYA KUPITIA UCHUMI WA KISASA WA BULUU

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyiameahidi kuijenga Zanzibar mpya kwa kupitia uchumi wa kisasa wa Buluu (Blue Economy).

 Ahadi hiyo ameitoa leo katika hotuba yake ya uzinduzi wa Baraza la Kumi la Wawakilishi lililofanyika huko katika ukumbi wa Baraza hilo Chukwani, nje kidogo ya Jiji la Zanzibar, hafla ambayo ilihudhuriwa na viongozi kadhaa akiwemo Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ali hassan Mwinyi, Rais Mstaafu wa Zanzzibar Amani Abeid Karume, Dk. Ali Mohammed Shein, Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu, Mama Maryam Mwinyi, wake wa Marais wastaafu, Mabalozi na viongozi wengineo.

Katika hotuba yake hiyo, Rais Dk. Hussein alisema kuwa moja ya ahadi yake kubwa aliyoitoa kwa wananchi na ambayo imeelezwa na Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni kujenga uchumi wa kisasa wa Buluu(Blue Economy).

Alisema kuwa Uchumi wa Buluu ama uchumi wa bahari unafungamanisha kwa pamoja sekta za uvuvi, ufugaji samaki, ujenzi wa viwanda vya samaki, ukulima wa mwani, uchimbaji wa mafuta na gesi, matumizi bora ya rasilimali mbali mbali za bahari pamoja na shughuli za utalii wa fukwe na michezo ya baharini.

 Aliongeza kuwa uchumi wa Buluu haukamiliki bila ya kuwepo kwa Bandari za kisasa zenye ufanisi wa hali ya juu.

Katika hotuba yake hiyo, Rais Dk. Hussein Mwinyi alieleza kuwa miongoni mwa mambo yanayodhoofisha misingi ya utawala bora ni  vitendo vya rushwa, uzembe, kukosa uwajibikaji, kutofuata sheria na kukiukwa kwa maadili hivyo, alisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Nane itakabiliana ipasavyo na vitendo vyote vinavyoathiri utekelezaji wa misingi ya utawala bora.

Rais Dk. Hussein alirejea ahadi yake kwa wananchi  mbele ya Baraza hilo kwamba atapambana na rushwa na ufisadi bila kigugumizi wala kuoneana muhali na kuwaomba Wawakilishi na Wananchi wote wamuunge mkono wakati wa mapambano hayo.

“Tutashinda vita hii endapo wananchi pia watatuunga mkono. Sina shaka kuwa kwa vile wao, kwa wingi wao, wanachukia rushwa na ufisadi, watakuwa tayari kutoa ushirikiano wao katika mapambano haya. Ni matumaini yangu pia vyombo husika katika jambo hili vitatekeleza wajibu wao”,alisema Rais Mwinyi.

Katika hotuba hiyo pia, Rais Dk. Hussein alitumia fursa hiyo kutoa pole kwa Chama cha ACT Wazalendo, ndugu, jamaa na marafiki kufuatia kifo cha Marehemu Abubakar Khamis Bakari ambaye aliwahi kuwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi na Waziri wa Katiba na Sheria katika Serikali ya Awamu ya Saba kipindi cha kwanza.

Aliongeza kuwa uteuzi wa viongozi na watendaji katika Srtikali yake utazingatia uwezo wa mtu kitaaluma, uwajibikaji na uaminifu.

Akieleza kuhusu sekta ya mafuta na gesi, Rais Dk. Mwinyi alisema kwamba Serikali ya Awamu ya Nane itaziimarisha na kuzijengea uwezo wa kitaaluma na nguvukazi Kampuni ya Mafuta Zanzibar (ZPDC) na Mamlaka ya Usimamizi wa Mafuta na Gesi (ZPRA) ili ziweze kuiongoza sekta hiyo muhimu.

Vile vile, Rais Dk. Hussein alisema kwamba Serikali itaendelea kushirikiana na Kampuni mbali mbali zenye dhamira njema ya kuwekeza hapa nchini katika sekta hiyo.

Aidha, alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Nane ina malengo ya kujenga bandari kubwa ya kisasa katika maeneo ya Mangapwani itakayokuwa na sehemu kadhaa za kutolea huduma zikiwemo sehemu za kuhudumia meli zitakazobeba mafuta na gesi, chelezo kwa ajili ya matengenezo ya meli, eneo la kuhudumia meli zinazobeba mizigo na makontena, bandari ya uvuvi pamoja na bandari ya meli za kitalii.

Aligusia kuwepo kwa malalamiko ya wafanyabiashara kuhusu kucheleweshwa mizigo yao bandarini na msongamano wa makontena katika Bandari ya Malindi, vitendo vya rushwa na kukosa uwajibikaji kwa baadhi ya watumishi wa bandarini.

Alielezadhamira ya Serikali ya kuimarisha bandari za Wete na Shumba Mjini na kuendelea na matayarisho ya ujenzi wa bandari ya mafuta na gesi huko Mangapwani na kuiimarisha bandari ya Mkoani ili iweze kuhudumia meli kubwa kutoka nje moja kwa moja kwa lengo la kunyanyua uchumi na biashara kwa kisiwa cha Pemba.

Alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Nane  itaongeza nguvu katika upanuzi wa wigo wa kodi na kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato na kuhakikisha kwamba kila mtu anayestahili kulipa kodi analipa kodi stahiki.

“Tutahakikisha kwamba kila senti inayoongezeka katika mapato ya Serikali inaelekezwa katika kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi. Tutaziba mianya ya upotevu wa fedha za Serikali ambayo inaipunguzia Serikali uwezo wake wa kuwahudumia wananchi”,alisema Rais Mwinyi.

 Aidha, alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Nane, itaweka mazingira mazuri ya uwekezaji na uendeshaji wa biashara ili sekta hizo ziwe na mchango mkubwa zaidi katika kukuza ajira na katika Pato la Taifa.

“Ushirikiano na umoja wetu ndio utakaotuwezesha kutekeleza  miradi yenye tija ikiwemo uendelezaji wa viwanda, utaliii na  uchumi wa buluu; ili kufanikisha azma hii, serikali itaweka mifumo rafiki kwa sekta binafsi kuweza kufanya kazi zao kwa ufanisi”,alisisitiza Dk. Hussein.

Aliongeza kuwa Serikali itaweka mazingira rafiki kwa Wanadiaspora kuja kuwekeza nyumbani kwa lengo la kuleta mapinduzi makubwa ya kiuchumi yanayokusudiwa kufanywa.

Kutokana na kuendelea kuimarika kwa sekta ya utalii, Rais Dk. Hussein alisema kuwa  kunampa matumaini kwamba malengo yaliyowekwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya kuongeza idadi ya wageni wanaoitembelea Zanzibar kutoka 538,264 mwaka 2019 hadi kufikia wageni 850,000 mwaka 2025 yatafikiwa.

Alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Naneitaendeleza dhamira njema ya kukuza sekta za Biashara na Viwanda hapa Zanzibar, ili kuwaletea wananchi wake maendeleo zaidi ya kiuchumi.

Alieleza kuwa hatokubaliana na visingizio vya aina yoyote na uzembe wa watendaji utakaozorotesha mipango  ya kukuza Sekta hizo na ndio maana, siku ya pili baada ya  kuapishwa na kuanza kazi rasmi alitembelea Bandari ya Malindi, ili kufahamu kwa kina malalamiko ya wafanyabiashara na wananchi kuhusiana na utendaji kazi na utoaji wa huduma usioridhisha unaofanywa na wafanyakazi Bandari hapo.

Rais Dk. Hussein aliwaeleza viongozi na wafanyakazi  wote katika  bandari kuu za  Unguja na Pemba pamoja na Viwanja vya ndege kwamba atakuwa akifuatilia kwa karibu utendaji wa taasisi hizo.

Alieleza bayana kwamba hajaridhishwa  na  uendeshaji wa shughuli za  bandari na viwanja vya ndege, katika maeneo yote, hasa  utoaji wa huduma, uendeshaji, ukusanyaji na  udhibiti wa mapato,  kiwango cha faida kinachopelekwa Serikalini kila mwaka  pamoja na mipango ya matumizi ya fedha za maendeleo

Alieleza kuwa atahakikisha kwamba  wafanyakazi wa bandarini  na viwanja vya ndege ni wale wanaopenda kazi kwa kuwatumikia umma, na sio wale wenye malengo binafsi ya kujinufaisha.

Rais Mwinyi alizitaja miongoni mwa barabara zitakazojengwa kwa Unguja ni Tunguu-Jumbi (km9.3), Jozani-Charawe-Ukongoroni-Bwejuu (km23.3), Fumba-Kisauni (km 12), Kizimbani-Kiboje (km 7.2) na Kichwele-Pangeni (km 4.8).

Nyengine alisema kuwa ni barabara ya Umbuji- Uroa ( km 6.9), Mkwajuni-Kijini (km 9.4) na Tunguu-Makunduchi (km48). Vile vile, kwa kuzingatia usumbufu wanaoupata wananchi wanaoishi vijiji vya Uzi na Ng’ambwa, Serikali itashughulikia ujenzi wa barabara na daraja kutoka Unguja ukuu hadi kisiwa cha Uzi.

Kwa upande wa Pemba,  alizitaja barabara zitakazojengwa kwa kiwango cha lami kuwa ni barabara ya Chake chake – Wete (km 22.1), Mkoani-Chake chake kupitia Chanjaani (km 29) na barabara ya Finya – Kicha (km 8.8) pamoja na kuzitengeneza  barabara za ndani za Unguja na Pemba ili zipitike kwa urahisi wakati wote.

Sambamba na miongozo ya Ilani ya Uchaguzi, alieleza kwamba Serikali ya Awamu ya Nane, itaweka mkazo katika kuimarisha Sekta ya Huduma za Fedha kwa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji na uendeshaji wa shughuli za benki, mashirika ya bima na taasisi nyengine za fedha.

Alisema kuwa Serikali itasimamia utendaji wa mashirika yake kwa lengo la kuhakikisha taasisi hizo zinatoa huduma bora zenye kuaminika kwa wateja wote.

Rais Dk. Mwinyi alieleza kwamba serikali  itaimarisha  mitaala ya masomo ya sayansi katika skuli, vituo na taasisi za ufundi pamoja na vyuo vikuu  ili kuwaandaa vizuri vijana wetu na hatimae  kuweza kwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia katika sekta zote.

Alieleza kwamba Serikali ya Awamu ya Nane itaendeleza juhudi zilizopo za kuliimarisha zao la karafuukwa kutoa mikopo na kuwatafutia masoko wakulima.

Kadhalika, kutokana na tatizo kubwa la uhaba wa nazi unaopelekea kupanda bei ya zao hilo kila uchao, alisema kuwa Serikali itaimarisha upandaji wa miche ya minazi ili kuongeza uzalishaji wa zao hilo pamoja na kuendeleza program ya kukuza zao la minazi iliyoanzishwa mwaka 2019.

Alisema kuwaSerikali yake itaweka mkazo katika kuendeleza shughuli za ufugaji wa njia za kisasa, ili sekta hiyo iwe na tija zaidi kwa wakulima na kuongeza mchango wake katika upatikanaji wa chakula na kuimarisha Pato la Taifa. Serikali itabuni na kutekeleza mikakati madhubuti ya kukomesha wizi wa mifugo na mazao.

Mapema mara baada ya kufika katika viunga vya Baraza la Wawakilishi,  Dk. Mwinyi alikagua Gwaride la Heshima lililoandaliwa kwa ajili ya hafla hiyo  huko katika viwanja vya Baraza hilo la Wawakilishi, Chukwani Jijini  Zanzibar.

MAONI YA WAJUMBE WA BARAZA LA WAWAKILISHI KUHUSU HOTUBA YA RAIS DK. HUSSEIN MWINYI

Balozi Mdogo wa Heshima wa Brazil Nchini Zanzibar Mh Abdulsamad Abdulrahim amesema hutuba ya Mh Rais imetoa fursa katika mambo mengi ukizingatia Zanzibar inarasilimali nyingi.

Akizungumza na ZBC baada ya kuhairika kwa kikao cha baraza la wawakilishi Abdul Swamad amesema atahakikisha anashirikiana na Serikali katika kufikia malengo yake.

Amesema kwa upande wa sekta ya mafuta na gesi asilia atasimamamia ipasavyo ili kuhakikisha taifa linafaidika na sekta hiyo.

Nao baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wamesema Hotuba ya Mh Rais inamatumaini mema kwa Wananchi na wamewaomba wale wote watakaopata Uongozi kusimamia vyema majukumu yao nakumpa ushirikiano Mh: Raisi katika kusimamia Jukumu la kuwaletea Maendeleo Wananchi.

 

YAMLE YAMLE CUP

Mashabiki wa Meli Nne City na Mbirimbirini wameendelea na tambo na majigambo kuelekea nusu Fainali ya michuano ya Yamle Yamle Cup inayotarajiwa kufanyika katika uwanja wa Mao Zedong’s siku ya Jumamosi na Jumapili.

Wiki hii.

Wakizungumza na ZBC michezo shabiki wa Timu zote mbili wamejigamba kuhakikisha wanashinda na kuweza kuingia Fainali na kulichukuwa Kombe hilo.

Aidha Wazee na Mashabiki wameiomba kamati ya  Michuano hiyo kuendelea kufanyika kwa Michuano hiyo katika kiwanja cha Magirisi Arena kwa hatua za Awali ili Wakaazi wa maeneo hayo wanufaike.

Nusu Fainali ya kwanza ya Michuano hiyo inatarajiwa kuchezwa siku ya Jumamosi katika Uwanja wa  Mao Zedong's.