Daily Archives: November 11, 2020

WAJUMBE WA BARAZA LA WAWAKILISHI WAMEMCHAGUA NAIBU SPIKA MH MGENI HASSAN JUMA KWA ASILIMIA MIA MOJA

Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wamemchagua Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Mh Mgeni Hassan Juma kwa Asilimia mia moja

Akitoa Matokeo ya Kura hizo Nd Raya Issa Mselem amesema kura zilizomkubali Mh Mgeni ni kura 67 za Wajumbe ambao wa walioingia  Barazani Jumanne..

Akitoa Shukrani kwa Wajumbe  hao Mh Mgeni amesema Demokrasia ya Chama Cha Mapinduzi ni ushirikiano umoja na upendo na kuhakikisha wanatekeleza Majukumu yote ya Chama cha Mapinduzi kama Katiba inavyoeleza.

Amesema atatenda haki na uwaminifu na kushirikiana na wajumbe wote wa Baraza la Wawakilishi kwa kutekeleza Majukumu yao ya kazi.

Mh Anna Athanas amesema atahakikisha anatetea maslahi ya Wanawake na watu wenye ulemavu.

 

 

NGOZI NA WATUMISHI WA UMMA WAJITAMBUE NA KUJITATHMINI KATIKA UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU YAO

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh Hemed Suleiman Abdalla amewataka Viongozi na Watumishi wa Umma wajitambue na kujitathmini katika utekelezaji wa Majukumu yao waliopewa  na Taifa  ili ile kiu ya kuwatumikia Wananchi ifanikiwe vyema.

Amesema baadhi ya Viongozi ama watendaji watakaojihisi kwamba hawaendani na kasi ya Serikali iliyoanza kazi zake muda mfupi uliopita baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu ni vyema wakaondoka kwa heshima katika maeneo yao ya Kazi waliyokabidhiwa.

Mhe. Hemed Suleiman Abdalla alitoa kauli hiyo muda mfupi baada ya kupokewa ndani ya Ofisi yake mpya kama Mtendaji Mkuu wa Serikali wakati akizungumza na Viongozi wa idara na Taasisi zilizo Chini ya ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar hapo Vuga mjini Zanzibar.

Amesema hapendezi kuona baadhi ya Viongozi wa Taasisi na Wakuu wa Vitengo wanajifikiria maslahi yao binafsi hasa fursa za masomo hata zile Safari za Nje ya Zanzibar zinazoambatana na masurufu bila ya kujali haki za watendaji wao wa ngazi ya Chini.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitanabahisha wazi kwamba yeye akiwa mtendaji Mkuu wa shughuli za Serikali hatakuwa tayari kumbeba Kiongozi au Mtumishi ye yote aliyepewa dhamana na akashindwa kuitekeleza katika eneo lake la Kazi.

Alionya kwamba akimgundua Kiongozi anayetumia vibaya Rasilmali za Umma aelewe kwamba atakwenda na maji kwa vile hatasita kumchukulia hatua za kinidhamu mara moja kutokana na tabia hiyo mbaya isiyokubalika katika utumishi wa Umma

Aliwataka watendaji hao wa Utumishi wa Umma wajisafishe  kwa vile wao ndio wanaosimamia utendaji wa Serikali na kuacha malalamiko yasiyo na msingi kwani pale vinapojitokeza kikwazo katika uwajibikaji wao taratibu ziko wazi za kuwasilisha changamoto zao zinazowakabili katika ngazi ya juu.

Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdalla aliwashukuru Viongozi wakuu  Waliostaafu wa Serikali ya Awamu ya Saba Dr. Ali Mohamed Sheni na Balozi Seif Ali Iddi kwa ulezi wao mwema uliopelekea kumwajengea daraja ya pale walipofikia Viongozi Wapya.

Mapema akimkabidhi Ofisi pamoja na nyenzo za kazi Mtendaji Mkuu huyo mpya wa shughuli za Serikali Mh. Hemed Suleiman Abdalla, Makamu wa Pili wa Rais Mstaafu wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema uteuzi wa rais wa Zanzibar kumpa dhamana Mh. Hemed unatokana na ujemedari wake katika kusimamia maslahi ya wananchi.

Balozi Seif alisema kwa umahiri wake Mheshimiwa Hemed Suleiman hana shaka na jukumu alilokabidhiwa la umakamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar na kuwaomba viongozi na watendaji wa ofisi hiyo waendelee kumpa ushirikiano kama aliyopewa yeye wakati wa utumishi wake.

Akitoa Taarifa ya makaribisho hayo ya Ofisi Katibu Kuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd.Shaaban seif Mohamed alisema kwa Niaba ya Wafanyakazi wa Ofisi hiyo alimpongeza Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdalla kwa kuteuliwa kuwa makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

Nd. Shaaban alisema makaribisho ya Wafanyakazi hao kwake Mheshimiwa  Hemed ni ishara ya kumkubali kufanya kazi pamoja katika kuona usimamizi wa Serikali unaendelea kutoa huduma kwa Umma.

Akitoa shukrani kwa niaba ya Viongozi na Wafanyakazi wote wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo Nd. Abdallah Hassan Mitawi alimuahidi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kupewa ushirikiano ili jukumu walilokabidhiwa na taifa lifanikiwe vyema.

Ndugu Mitawi alitumia nafasi hiyo kumshukuru na kumpongeza Makamu wa Pili wa Rais mstaafu wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kwa busara zake zilizochangia kuwapa msukumo Viongozi na watendaji na hatimae kufanikiwa katika utekelezaji wa Majukumu yao ya kila siku.

Mapema Asubuhi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdalla alipokewa kwa shangwe na vigere gere na viongozi waandamizi pamoja na watendaji wa ofisi hiyo wakati alipoingia kwenye majengo hayo kuanza jukumu lake alilopatiwa na taifa.

Mapokezi hayo ya aina yake yaliambatana na kuvishwa shada la maua kama ishara ya kumpokea ramsi mtendaji mkuu huyo wa shughuli za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ofisini vuga Mjini Zanzibar.