Daily Archives: November 10, 2020

DK. HUSSEIN MWINYI AMEMUAPISHA MH. HEMED SULEIMAN ABDALLA KUWA MAKAMO WA PILI WA RAIS WA ZANZIBAR

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dk. Hussein Ali Mwinyiamemuapisha Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla kuwa Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

 Hafla hiyo ya kiapo imefanyika Ikulu Jijini Zanzibar ambayo ilihudhuriwa na  viongozi mbali mbali akiwemo Spika wa Baraza la Wawakilishi Mhe. Zubeir Ali Maulid, Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee.

Wengine ni Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Dk. Mwinyi Talib Haji, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Hassan KhatibMufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabih,  Naibu Kadhi Mkuuwa ZanzibarSheikh  Hassan Othman Ngwali, Naibu Mufti Mkuu Sheikh Mussa Wadi, Mkuu wa  Mkoa wa Mjini Magharibi Hassan Khatib Hassan, Mstahiki Meya wa Jiji la Zanzibar Saleh Juma Kinana , Wakuu wa vikosi vya Ulinzi na Usalama, viongozi wengine wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na wanafamilia.

Akizungumza mara baada ya kiapo hicho Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla alitoa pongezi kwa Mhe. Rais Dk. Hussein Mwinyi kwa kumuamini na  kumteua kuwa Msaidizi wake namba moja na kuahidi kwamba atamsaidia kwa asilimia mia moja.

Alieleza kwamba uteuzi huo ameupokea vizuri na kwa sababu Rais kamteua akiamini kwamba anaweza kumsaidia hivyo, aliwaahidi wananchi wote wa Zanzibar na Tanzania nzima kwa jumla kwamba atafanya kazi hiyo kwa uaminifu na uadilifu mkubwa na kuhakikisha yale malengo ya Serikali yaliyowekwa yanafikiwa kwa mujibu wa sheria.

Alisema kwamba katika hilo yapo mambo ambayo yatajitokeza hapo baadae ambapo watatokeabaadhi ya watu ambao watakuwa hawako tayari kuyatekeleza hivyo,alisema kwamba akiwa Msimamizi Mkuu wa shughuli za Serikali hatokuwa na muhali wa aina yoyote na kwamba hatua stahiki zitachukuliwa ili kuweza kupata watu watakaoendana na kasi ya Mhe. Rais.

Alisema kwamba wananchi wanamategemeo makubwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na hasa baada ya Rais wa Zanzibar kushinda uchaguzi mkuu kwa kishindo kikubwa.

Aliongeza kwambamalengo ndani ya Serikali ni kuhakikisha matumaini yanarejeshwa kama vile Rais alivyoahidi kuyatekeleza katika kampeni zake kipindi ambacho anaomba fursa ya kuchaguliwa kuwa Rais.

Aidha, alisema kwamba atasimamia na kumsaidia Rais kwa asilimia mia na atatumia nguvu zake zote na hekima na busara zake zote katika kuhakikisha malengo hayo yanatimia.

Makamo  wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla aliteuliwa jana na Rais Dk. Hussein Mwinyi kwa mujibu wa uwezo aliopewa chini ya Kifungu Namba 39 (1) na 39 (2) cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.

Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla ni miongoni mwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi walioteuliwa na Rais Dk. Hussein Mwinyi mnamo tarehe 07 Novemba 2020 kwa mujibu wa uwezo aliopewa chini ya Kifungu Namba 66 cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.

Kabla ya Uteuzi huo Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba.

 

WIZARA YA AFYA ZANZIBAR IMESEMA IMEANDAA UPIMAJI WA MARADHI YASIOAMBUKIZA KWA WAUGUZI

Wizara ya Afya Zanzibar imesema imeandaa Upimaji wa Maradhi yasioambukiza kwa Wauguzi ikiwa ni maandalizi ya siku ya Kisukari duniani utakayofanyika Novemba 14 mwaka  huu.

Akizungumza na ZBC Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi  Dk Haji Nyonje Pandu  na   Muuguzi Mkunga wa Watoto Dk Zuhura Saleh wamefahamisha kuwa katika maandalizi hayo wanatarajia kuwapima zaidi ya wauguzi mia tano ili kujua Afya zao kwa lengo la kutoa huduma bora kwa Wagonjwa.

Msaidizi Mkurugenzi Uuguzi wa Hospitali ya Mnazi mmoja Dk Tatu Khamis Hussein na Katibu wa Jumuiiya ya watu wanaoishi na Maradhi ya Kisukari Zanzibar Ali Zubeir Juma wamesema Upimaji wa Afya kwa Wauguzi hao kunatoa fursa muhimuza kujua Afya zao hivyo amewahimiza kutodharau huduma hiyo.

Upimaji huo unafanywa kwa ushirikianowa kitengo cha Maradhi yasioambukiza cha Wizara ya Afya, jumuiya ya Watu wanaoishi na Maradhi ya Kisukari Zanzibar pamoja na Muungano wa Jumuiya za Maradhi yasioambukiza Zanizbar na utafanyika katika Hospitali ya Mnazi Mmoja, Mwembeladu na Kidongo Chekundu.