Monthly Archives: November 2020

WAWEKEZAJI KUTOKA JUMUIYA YA MADHEHEBU YA BOHORA KUWEKEZA ZANZIBAR

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dk. Hussein Ali Mwinyiamewakaribisha wawekezaji kutoka Jumuiya ya Madhehebu ya Bohora kuja kuekeza Zanzibar kutokana na fursa mbali mbali zilizopohapa nchini.

Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi aliyasema hayo leo Ikulu Jijini Zanzibar wakati alipokutana na Wajumbe wa Jumuiya ya Madhehebu ya Bohora kutoka Zanzibar na Tanzania Bara wakiongozwa na kiongozi wao Sheikh Tayabali Hamza Bhai Patanwalla ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya mwenye makao makuu yake Jijini Dar es Salaam.

 Rais Dk. Hussein aliueleza Ujumbe huo wa Jumuiya ya Madhehebu ya Bohora kutoka Zanzibar na Dar-es Salaam kwamba milango ya Zanzibar iko wazi hivyo, anawakaribisha kuja kuekeza Zanzibar hasa ikizingatiwa kwamba walio wengi katika Jumuiya hiyo ni wafanyabiashara.

Alisema kuwa Zanzibar ina fursa nyingi za kuekeza katika sekta mbali mbali za maendeleo zikiwemo viwanda hivyo, aliwataka kuitumia fursa hiyo na kusisitiza kwamba iwapo itazitumia fursa hiyo vyema itasaidia katika kutoa ajira kwa vijana.

Aliongeza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane itaendelea kushirikiana na Madhehebu hayo pamoja na yale mengine yote hapa nchini katika kuhakikisha kunakuwepo mashirikiano ya pamoja kwa azma ya kuendeleza na kuimarisha sekta mbali mbali za maendeleo.

Rais  Dk. Hussein Mwinyi aliipongeza Jumuiya hiyo kwa kuiunga mkono Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha na kuendeleza sekta mbali mbali za kijamii, kiuchumi na kimaendeleo zikiwemo huduma za afya, elimu na nyenginezo.

Aidha, Rais Dk. Hussein Mwinyi alitoa shukurani kwa Kiongozi wa Madhehebu ya Bohora duniani Dk. Syedna Mufaddal Saifuddin kutokana na salamu zake za pongezi alizomletea  ambazo ziliwasilishwa na viongozi hao katika mkutano wao huo hivi leo.

Akitoa shukurani kutokana na salamu hizo, Rais Dk. Mwinyi aliipongeza Jumuiya hiyo kwa kuendeleza uhusiano na ushirikiano uliopo na kuahidi kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na Jumuiya hiyo bega kwa bega.

 Mapema viongozi wa Jumuiya ya Madhehebu ya Bohora walimkabidhi Rais Dk. Hussein Mwinyi salamu za pongezi zilizotolewa na Kiongozi wa Madhehebu ya Bohora duniani Dk. Syedna Mufaddal Saifuddin kwa ushindi mkubwa alioupata na kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.

Akisoma salamu hizo kutoka kwa kiongozi huyo, Bwana Murtaza Zakirhussein AliBhai ambaye ni Mjumbe wa Jumuiya hiyo alieleza kuwa Kiongozi wa Madhehebu ya Bohora duniani Dk. Syedna Mufaddal Saifuddin anatoa pongezi kwa Rais Dk. Hussein na kusema kwamba wananchi wa Zanzibar wanamatumaini makubwa na uongozi wake.

Salamu hizo zilieleza kwamba kiongozi huyo ana matumaini makubwa kwamba Zanzibar itaendelea kupata mafanikio makubwa katika kuendeleza kujiletea maendeleo yake kiuchumi, kijamii na  kiutamaduni.

“Hongera kwa ushindi mkubwa ulioupata katika uchaguzi uliopita, watu wa Zanzibar wamekuchagua wewe wakiwa na matumaini makubwa ya maendeleo kwa kutambua kwamba wewe utaiongoza Zanzibar kwa amani, umoja na mshikamano utakaodumu leo na siku zijazo”,ilieleza sehemu ya salamu hizo za pongezi kutoka kwa Dk. Saifuddin.

Sambamba na hayo, kiongozi huyo wa Mabohora duniani alimuombea dua Rais Dk. Mwinyi kwa Mwenyezi Mungu yeye na familia yake pamoja na wananchi wote wa Zanzibar ili wazidi kupata maendeleo zaidi na Allah aendelee kuwa mlinzi wao.

Kwa upande wao viongozi hao waliofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa pamoja waliipongeza  hotuba aliyoitoa Rais Dk. Hussein Mwinyi siku aliyowaapisha Mawaziri katika viwanja vya Ikulu na kusema kwamba imewatia moyo na kuwapa matumaini makubwa ya mafanikio na maendeleo kwa Zanzibar na kuamini kwamba yajayo ni neema tupu.

Viongozi hao walimuahidi Rais Dk. Hussein Mwinyi kwamba watahakikisha Jumuiya yao inalichukua kwa mikono miwili suala la uwekezaji katika sekta mbali mbali za maendeleo ikiwemo viwanda na sekta nyenginezo na kuahidi kulifanyia kazi kwani limo ndani ya uwezo wao, huku wakiahidi kiongozi wao kufika Zanzibar pale atakapofanya ziara tena hapa nchini kwani mnamo Agosti 17,2020 alifanya ziara nchini  Tanzania.

 

DK. HUSSEIN ALI MWINYI AMEKUTANA NA WAFANYA BIASHARA WA ENEO LA KIJANGWANI

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameliagiza Baraza la Manispaa Mjini na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi kutafuta eneo jengine la muda kwa ajili ya Wafanya biashara wa eneo la Kijangwani

Rais Mwinyi ametoa Agizo hilo kufuatia malalamiko ya Wafanyabiashara hao kutakiwa kuondoka eneo hilo na kuhamia eneo la Jitimai ambapo kwa sasa amewaagiza wafanyabiashara hao kuendelea na biashara zao kwa muda katika eneo la Kijangwani

Aidha Rais Mwinyi amewataka Ofisi hizo kuzungumza pamoja na Wafanyabiashara hao ili kutafuta sehemu nyengine ambayo wataikubali  wenyewe kwa ajili ya kufanya kazi zao

Ameeleza kuwa Ahadi yake ya kuweka mazingira bora kwa Wafanyabiashara hao iko pale pale na ameahidi kuwa wataandaliwa vitambulisho maalumuili kuepuka kutoa kodi za kila siku.

Amewataka ndani ya muda mfupi kupewa Ripoti juu ya eneo litakalopatikana kwa ajili ya wafanyabiashara na ujenzi wake uzingatie miundombinu yote muhimu inayohitajika.

Aidha Rais Mwinyi amewaomba Wananchi kutoa ushirikiano kwa miradi inayoanzishwa na Serikali kwani ina Malengo mazuri ya kuhakikisha Uchumi wa Zanzibar unaimarika na kuhimiza suala la usafi wa mji ikizingatiwa kuwa Mji wa Zanzibar ni kitovu kikuu kwa ajili ya shughuli za Utalii.

Akitoa maelezo kwa Rais wa Zanzibar, Mkuu wa mkoa wa Mjini Magharibi Mh. Hassan Khatib amesema eneo la Kijwangwani lilikubaliwa kuwa ni eneo la muda kwa kufanyia Biashara kutokana na mripuko wa korona ili kupunguza msongamano katika Maeneo mengine ya Biashara.

UTAFITI WA WHO WA MWAKA 2011 UNAONESHA ATHARI ZA UVUTAJI WA SIGARA HUCHANGIA MARADHI YASIIOAMBUKIZA

Uvutajj wa Sigara kwa Zanzibar uko kwa Asilimia 7.3  nani Miongonu mwa vichocheo vya vikubwa vya uwepo wa Maradhi yasioambukiza.

Akizungumza  na Waandishi wa Habari katika Shamra shamra za kuadhimisha siku ya kisukari, meneja kitengo cha maradhi yasioambukiza katika Wizara ya Afya Omar Abdullah ali amesema utafiti wa who wa Mwaka 2011 unaonesha kuwa Athari za uvutaji wa Sigara huchangia kwa kiasi kikubwa Maradhi yasiioambukiza ikiwemo Sukari kensa moyo na shinikizo la Damu.

Amefahamisha kuwa hali hiyo imeonekana hadi kwa Wanafunzi kuanzia umri wa Miaka 9 kuanza matumizi ya sigara kitu ambacho ni kinaweza kumpotezea mwelekeo mzima wa maisha yake kutokana na kuathirika zaidi kiafya .

Meneja wa Jumuiya ya Muungano wa watu wanaoishi na Maradhi yasioambukiza Zanzibar Nd Haji Khamis Fundi amesema wamejipanga kutoa Elimu ipasavyo kuanzia kwa watoa huduma pamoja na kutaka Sheria ya kuzuiya uvutajiwa Sigara kwenye mikusanyiko ya watukufanya kazi ili kuepuka Athati kwa Jamii.

 

DK. HUSSEIN MWINYI KUIJENGA ZANZIBAR MPYA KUPITIA UCHUMI WA KISASA WA BULUU

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyiameahidi kuijenga Zanzibar mpya kwa kupitia uchumi wa kisasa wa Buluu (Blue Economy).

 Ahadi hiyo ameitoa leo katika hotuba yake ya uzinduzi wa Baraza la Kumi la Wawakilishi lililofanyika huko katika ukumbi wa Baraza hilo Chukwani, nje kidogo ya Jiji la Zanzibar, hafla ambayo ilihudhuriwa na viongozi kadhaa akiwemo Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ali hassan Mwinyi, Rais Mstaafu wa Zanzzibar Amani Abeid Karume, Dk. Ali Mohammed Shein, Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu, Mama Maryam Mwinyi, wake wa Marais wastaafu, Mabalozi na viongozi wengineo.

Katika hotuba yake hiyo, Rais Dk. Hussein alisema kuwa moja ya ahadi yake kubwa aliyoitoa kwa wananchi na ambayo imeelezwa na Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni kujenga uchumi wa kisasa wa Buluu(Blue Economy).

Alisema kuwa Uchumi wa Buluu ama uchumi wa bahari unafungamanisha kwa pamoja sekta za uvuvi, ufugaji samaki, ujenzi wa viwanda vya samaki, ukulima wa mwani, uchimbaji wa mafuta na gesi, matumizi bora ya rasilimali mbali mbali za bahari pamoja na shughuli za utalii wa fukwe na michezo ya baharini.

 Aliongeza kuwa uchumi wa Buluu haukamiliki bila ya kuwepo kwa Bandari za kisasa zenye ufanisi wa hali ya juu.

Katika hotuba yake hiyo, Rais Dk. Hussein Mwinyi alieleza kuwa miongoni mwa mambo yanayodhoofisha misingi ya utawala bora ni  vitendo vya rushwa, uzembe, kukosa uwajibikaji, kutofuata sheria na kukiukwa kwa maadili hivyo, alisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Nane itakabiliana ipasavyo na vitendo vyote vinavyoathiri utekelezaji wa misingi ya utawala bora.

Rais Dk. Hussein alirejea ahadi yake kwa wananchi  mbele ya Baraza hilo kwamba atapambana na rushwa na ufisadi bila kigugumizi wala kuoneana muhali na kuwaomba Wawakilishi na Wananchi wote wamuunge mkono wakati wa mapambano hayo.

“Tutashinda vita hii endapo wananchi pia watatuunga mkono. Sina shaka kuwa kwa vile wao, kwa wingi wao, wanachukia rushwa na ufisadi, watakuwa tayari kutoa ushirikiano wao katika mapambano haya. Ni matumaini yangu pia vyombo husika katika jambo hili vitatekeleza wajibu wao”,alisema Rais Mwinyi.

Katika hotuba hiyo pia, Rais Dk. Hussein alitumia fursa hiyo kutoa pole kwa Chama cha ACT Wazalendo, ndugu, jamaa na marafiki kufuatia kifo cha Marehemu Abubakar Khamis Bakari ambaye aliwahi kuwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi na Waziri wa Katiba na Sheria katika Serikali ya Awamu ya Saba kipindi cha kwanza.

Aliongeza kuwa uteuzi wa viongozi na watendaji katika Srtikali yake utazingatia uwezo wa mtu kitaaluma, uwajibikaji na uaminifu.

Akieleza kuhusu sekta ya mafuta na gesi, Rais Dk. Mwinyi alisema kwamba Serikali ya Awamu ya Nane itaziimarisha na kuzijengea uwezo wa kitaaluma na nguvukazi Kampuni ya Mafuta Zanzibar (ZPDC) na Mamlaka ya Usimamizi wa Mafuta na Gesi (ZPRA) ili ziweze kuiongoza sekta hiyo muhimu.

Vile vile, Rais Dk. Hussein alisema kwamba Serikali itaendelea kushirikiana na Kampuni mbali mbali zenye dhamira njema ya kuwekeza hapa nchini katika sekta hiyo.

Aidha, alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Nane ina malengo ya kujenga bandari kubwa ya kisasa katika maeneo ya Mangapwani itakayokuwa na sehemu kadhaa za kutolea huduma zikiwemo sehemu za kuhudumia meli zitakazobeba mafuta na gesi, chelezo kwa ajili ya matengenezo ya meli, eneo la kuhudumia meli zinazobeba mizigo na makontena, bandari ya uvuvi pamoja na bandari ya meli za kitalii.

Aligusia kuwepo kwa malalamiko ya wafanyabiashara kuhusu kucheleweshwa mizigo yao bandarini na msongamano wa makontena katika Bandari ya Malindi, vitendo vya rushwa na kukosa uwajibikaji kwa baadhi ya watumishi wa bandarini.

Alielezadhamira ya Serikali ya kuimarisha bandari za Wete na Shumba Mjini na kuendelea na matayarisho ya ujenzi wa bandari ya mafuta na gesi huko Mangapwani na kuiimarisha bandari ya Mkoani ili iweze kuhudumia meli kubwa kutoka nje moja kwa moja kwa lengo la kunyanyua uchumi na biashara kwa kisiwa cha Pemba.

Alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Nane  itaongeza nguvu katika upanuzi wa wigo wa kodi na kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato na kuhakikisha kwamba kila mtu anayestahili kulipa kodi analipa kodi stahiki.

“Tutahakikisha kwamba kila senti inayoongezeka katika mapato ya Serikali inaelekezwa katika kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi. Tutaziba mianya ya upotevu wa fedha za Serikali ambayo inaipunguzia Serikali uwezo wake wa kuwahudumia wananchi”,alisema Rais Mwinyi.

 Aidha, alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Nane, itaweka mazingira mazuri ya uwekezaji na uendeshaji wa biashara ili sekta hizo ziwe na mchango mkubwa zaidi katika kukuza ajira na katika Pato la Taifa.

“Ushirikiano na umoja wetu ndio utakaotuwezesha kutekeleza  miradi yenye tija ikiwemo uendelezaji wa viwanda, utaliii na  uchumi wa buluu; ili kufanikisha azma hii, serikali itaweka mifumo rafiki kwa sekta binafsi kuweza kufanya kazi zao kwa ufanisi”,alisisitiza Dk. Hussein.

Aliongeza kuwa Serikali itaweka mazingira rafiki kwa Wanadiaspora kuja kuwekeza nyumbani kwa lengo la kuleta mapinduzi makubwa ya kiuchumi yanayokusudiwa kufanywa.

Kutokana na kuendelea kuimarika kwa sekta ya utalii, Rais Dk. Hussein alisema kuwa  kunampa matumaini kwamba malengo yaliyowekwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya kuongeza idadi ya wageni wanaoitembelea Zanzibar kutoka 538,264 mwaka 2019 hadi kufikia wageni 850,000 mwaka 2025 yatafikiwa.

Alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Naneitaendeleza dhamira njema ya kukuza sekta za Biashara na Viwanda hapa Zanzibar, ili kuwaletea wananchi wake maendeleo zaidi ya kiuchumi.

Alieleza kuwa hatokubaliana na visingizio vya aina yoyote na uzembe wa watendaji utakaozorotesha mipango  ya kukuza Sekta hizo na ndio maana, siku ya pili baada ya  kuapishwa na kuanza kazi rasmi alitembelea Bandari ya Malindi, ili kufahamu kwa kina malalamiko ya wafanyabiashara na wananchi kuhusiana na utendaji kazi na utoaji wa huduma usioridhisha unaofanywa na wafanyakazi Bandari hapo.

Rais Dk. Hussein aliwaeleza viongozi na wafanyakazi  wote katika  bandari kuu za  Unguja na Pemba pamoja na Viwanja vya ndege kwamba atakuwa akifuatilia kwa karibu utendaji wa taasisi hizo.

Alieleza bayana kwamba hajaridhishwa  na  uendeshaji wa shughuli za  bandari na viwanja vya ndege, katika maeneo yote, hasa  utoaji wa huduma, uendeshaji, ukusanyaji na  udhibiti wa mapato,  kiwango cha faida kinachopelekwa Serikalini kila mwaka  pamoja na mipango ya matumizi ya fedha za maendeleo

Alieleza kuwa atahakikisha kwamba  wafanyakazi wa bandarini  na viwanja vya ndege ni wale wanaopenda kazi kwa kuwatumikia umma, na sio wale wenye malengo binafsi ya kujinufaisha.

Rais Mwinyi alizitaja miongoni mwa barabara zitakazojengwa kwa Unguja ni Tunguu-Jumbi (km9.3), Jozani-Charawe-Ukongoroni-Bwejuu (km23.3), Fumba-Kisauni (km 12), Kizimbani-Kiboje (km 7.2) na Kichwele-Pangeni (km 4.8).

Nyengine alisema kuwa ni barabara ya Umbuji- Uroa ( km 6.9), Mkwajuni-Kijini (km 9.4) na Tunguu-Makunduchi (km48). Vile vile, kwa kuzingatia usumbufu wanaoupata wananchi wanaoishi vijiji vya Uzi na Ng’ambwa, Serikali itashughulikia ujenzi wa barabara na daraja kutoka Unguja ukuu hadi kisiwa cha Uzi.

Kwa upande wa Pemba,  alizitaja barabara zitakazojengwa kwa kiwango cha lami kuwa ni barabara ya Chake chake – Wete (km 22.1), Mkoani-Chake chake kupitia Chanjaani (km 29) na barabara ya Finya – Kicha (km 8.8) pamoja na kuzitengeneza  barabara za ndani za Unguja na Pemba ili zipitike kwa urahisi wakati wote.

Sambamba na miongozo ya Ilani ya Uchaguzi, alieleza kwamba Serikali ya Awamu ya Nane, itaweka mkazo katika kuimarisha Sekta ya Huduma za Fedha kwa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji na uendeshaji wa shughuli za benki, mashirika ya bima na taasisi nyengine za fedha.

Alisema kuwa Serikali itasimamia utendaji wa mashirika yake kwa lengo la kuhakikisha taasisi hizo zinatoa huduma bora zenye kuaminika kwa wateja wote.

Rais Dk. Mwinyi alieleza kwamba serikali  itaimarisha  mitaala ya masomo ya sayansi katika skuli, vituo na taasisi za ufundi pamoja na vyuo vikuu  ili kuwaandaa vizuri vijana wetu na hatimae  kuweza kwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia katika sekta zote.

Alieleza kwamba Serikali ya Awamu ya Nane itaendeleza juhudi zilizopo za kuliimarisha zao la karafuukwa kutoa mikopo na kuwatafutia masoko wakulima.

Kadhalika, kutokana na tatizo kubwa la uhaba wa nazi unaopelekea kupanda bei ya zao hilo kila uchao, alisema kuwa Serikali itaimarisha upandaji wa miche ya minazi ili kuongeza uzalishaji wa zao hilo pamoja na kuendeleza program ya kukuza zao la minazi iliyoanzishwa mwaka 2019.

Alisema kuwaSerikali yake itaweka mkazo katika kuendeleza shughuli za ufugaji wa njia za kisasa, ili sekta hiyo iwe na tija zaidi kwa wakulima na kuongeza mchango wake katika upatikanaji wa chakula na kuimarisha Pato la Taifa. Serikali itabuni na kutekeleza mikakati madhubuti ya kukomesha wizi wa mifugo na mazao.

Mapema mara baada ya kufika katika viunga vya Baraza la Wawakilishi,  Dk. Mwinyi alikagua Gwaride la Heshima lililoandaliwa kwa ajili ya hafla hiyo  huko katika viwanja vya Baraza hilo la Wawakilishi, Chukwani Jijini  Zanzibar.