Monthly Archives: October 2020

DKT SHEIN AMEAGANA NA WATENDAJI ALIOWATEUA SERIKALINI

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Ali Mohamed Shein ameagana na watendaji aliowateua katika nyadhifa mbali mbali Serikalini na kusema kwamba hafla hiyo ni kielelezo cha mafanikio katika kuendeleza na kudumisha Demokrasia na utawala bora Nchini.

 Dk. Shein aliyasema hayo leo huko katika viwanja vya Ikulu jijini Zanzibar katika hotuba ya kuagana na Watendaji aliowateua katika nyadhifa mbali mbali  katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Rais Dk. Shein alisema kuwa kuwepo kwa mfumo mzuri wa kisheria wa kubadilishana, kupokezana na kuacha madaraka ni miongoni mwa mambo yaliyoipatia sifa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar duniani kote.

Alisema kuwa viongozi wa Tanzania wamejijengea sifa ya kuacha, kukamilisha na kupokezana madaraka  kwa nafasi mbali mbali kwa hali ya salama na utulivu.

Aliongeza kuwa suala la kubadilishana madaraka au kuachia kwa hiari ili kutoa nafasi kwa wengine katika ngazi mbali mbali ni utamaduni uliojengeka hata kwa chama chake cha Mapinduzi (CCM).

Rais Dk. Shein alisema kuwa viongozi wote hao akiwemo yeye mwenyewe wanawajibika kwa wananchi wa Zanzibar kwani Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni yao hivyo alisisitiza haja ya kuwatumikia wananchi iapsavyo.

Alieleza kuwa jambo ambalo amekuwa akilisisitiza kwa kipindi chote cha miaka 10 ya uongozi wake ni kuwataka watumishi wa umma wafahamu jukumu lao kubwa la kutoa huduma kwa wananchi.

Alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutokana na mipango iliyopangwa ya Maendeleo ikiwa ni pamoja na mafanikio ya Dira ya Maendeleo 2020, Mipango ya Kimaendeleo ya Kimataifa.

Alisema kuwa kasi ya maendeleo iliyofanywa na Awamu ya Saba imetokana na kasi za Awamu zilizopita ambapo mafanikio yameweza kupatikana ikiwa ni pamoja na kuimarika kwa uchumi kwa asilimia 7.

Alieleza kuwa ndani ya miaka 10, Sheria 128 zimetungwa na kuwa Sheria za Zanzibar jambo ambalo ni mafanikio makubwa kwa Zanzibar ambapo katika Sheria hizo mbili miongoni mwao ni Sheria ya Kupambana na Rushwa na Uhujumu Uchumi na ile Sheria ya Maadili ya Uongozi wa Umma.

Rais Dk. Shein akinukuu Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kwenye Ibara ya 28 kifungu cha 3, ambacho kinasema kwamba “Bila ya kuathiri chochote kilichomo katika kifungu hiki cha Katiba hii hakutakuwa na mtu yoyote ataechaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar kwa zaidi ya vipindi viwili vya miaka mitano kila kimoja”.

Alitoa pongezi kwa Watendaji wote aliowateua kwa kufanya kazi vizuri na kuweza kuwasaidia wananchi na kusema kuwa anathamini juhudi zao hizo zilizopelekea Zanzibar kupata mafanikio.

Rais Dk. Shein alieleza kuwa mara nyingi inapofanywa safari jambo la kwanza linaloombwa ni  kujaalia safari ya salama na inapofikwa safari hiyo jambo linalofuata ni kutoa shukurani kwa kufika salama na kusema kuwa safari ya miaka 10 ni ndefu.

Alisema kuwa shughuli hiyo ya kuagana inatoa furaha kubwa akikumbuka kwamba anawaaga watendaji hao wakiwa wamefanya mambo mengi mazuri kwa pamoja kwa ajili ya kuwatumikia wananchi.

Aidha, alisema kuwa shughuli hiyo inatoa fursa ya kuyatathmini maisha yao pamoja na kazi mbali mbali walizozifanya pamoja kwa kipindi cha miaka 10 ya uongozi wa Rais Dk. Shein.

Rais Dk. Shein alisema kuwa baadhi ya wakati nyoyo hugubikwa na machungu, hasa kama watu wanaoagana waliishi vizuri na walipendana.

“Hali hii imeelezwa vizuri na Malenga wa Kiengereza, Bibi Mary Ann Evans, pale aliposema ‘Only in the agony of parting do we look into the depths of love’ akiwa na maana tunapokumbwa na machungu ya kuagana, ndipo hasa tunapofikiria ukubwa wa mapenzi yaliyokuwepo”,alisema Dk. Shein.

Aidha, Rais Dk. Shein alisema kuwa Zanzibar inapendwa sana kwa sababu Zanzibar ni salama na watu wake ni wakarimu sana na jina lake linajiuza kwa kiasi kikubwa kwa watalii na kusisitiza haja ya kuongeza nguvu katika sekta hiyo.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein alitoa pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Pombe Joseph Magufuli kwa kushirikiana nae katika uongozi wake wote pamoja na kuyalinda na kuyadumisha Mapinduzi sambamba na kuudumisha Muungano.

Alisema kuwa katika Rais yeyote atakaetoka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania au Rais wa Zanzibar basi ataheshimu Mapinduzi na ataheshimu Muungano na kueleza imani yake kwamba Rais bora atatoka CCM.

Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuwashukuru viongozi wote wa SMZ na SMT pamoja na viongozi wastaafu wakiwemo Marais wa Wastaafu wa Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na  watendaji wengine wote akiwemo Makamo wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd na viongozi wengine.

Aliwapongeza viongozi wote wa CCM kwa kumpa heshima katika uongozi wake wote na kuwashukuru viongozi wote aliofanya kazi nao huku akimshukuru Marehemu Mzee Mkapa kwa kumteua kuwa Makamo wa Rais mara tu baada ya kutokea kifo cha Dk. Omar Ali Juma sambamba na kufanya kazi nae kwa mashirikiano makubwa.

Aidha, alimpongeza Mama Mwanamwema Shein kwa kumvumilia, kumliwaza na kumpa maneno mazuri  kwa kipindi chote cha takriban miaka 20 ya uongozi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Nae Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, alitoa shukurani kwa rais Dk. Shein kwa kushirikiana nae pamoja na imani kubwa aliyonayo kwake na kutoa shukurani kwa Mawaziri kwa kushirikiana katika kutatua changamoto mbali mbali.

Mapema Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee alitoa shukurani kwa Rais Dk. Shein kutokana na mambo mengi aliyowafanyia watendaji hao pamoja na wananchi kwa ujumla.

Alisema kuwa watumishi Serikalini wako wengi lakini ameweza kutoa nafasi kwa watendaji hao aliowateua hiyo ikionesha wazi kwamba anawaamini.

Alifahamisha kuwa katika kipindi chake cha uongozi Rais Dk. Shein amefanya mambo mengi yakiwemo kuimarisha miundombinu ya barabara, usafiri na usafirishaji, nyumba, ofisi, pencheni jamii kwa wazee, kuongeza mshahar kwa watumishi wa umma, sekta ya afya, elimu, kilimo, biashara uvuvi, ufugaji na nyenginezo.

Alimpongeza kwa kuimarisha utawala bora, na kupunguza manunguniko kwa wananchi sambamba na watendaji kujifunza has mfumo aliouanzisha wa “Bangokitita” na kuongeza mshahara kwa asilimia 100, kuanzisha taasisi mpya, wafanyakazi kupata nafasi za kusoma ndani na nje ya nchi, kujifunza staili yake ya kufanya kazi kwa utulivu, umakini, usikivu pamoja na kujifunza kutoka kwake kwamba kiongozi lazima ajiamini.

Alimpongeza Rais Dk. Shein kwa ujasiri wake hasa pale alipotangaza elimu bure pamoja na huduma zote za afya zitolewe bure kwa wananchi, kuongeza kiwango cha chini cha mshahara kutoka 150,000 hadi 300,000.

Alisema kuwa Rais Dk. Shein anamaliza uongozi wake akiwa anawaachia wananchi zawadi kubwa ya amani, utulivu, umoja na mshikamano na kuahidi kuwa tunu hiyo itaendelezwa na kutunzwa.

Nao Mawaziri wote wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar walipata fursa ya kueleza kwa ufupi mafanikio ya Wizara zao sambamba na kuwakabidhi zawadi mbali mbali Rais Dk. Shein pamoja na Mama Mwanamwema Shein.

Sambamba na hayo, Mawaziri wawili Wasiokuwa na Wizara Maalum ambao wanatoka kambi ya Upinzani walipata nafasi ya kutoa shukurani zao huku wakimpongeza Rais Dk. Shein kwa kuwateua kuwa Mawaziri jambo ambalo limemjengea sifa kubwa Dk. Shein sambamba kusisitiza haja ya kuilinda na kuidumisha amani iliyopo.

MATENGENEZO NA UTANUZI WA VIWANJA VINNE VYA NDEGE

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imezindua Mradi wa Ujenzi, Matengenezo pamoja na Utanuzi wa Viwanja vinne vya Ndege vya Shinyanga, Tabora, Sumbawanga na Kigoma ili viwe na kiwango cha Kimataifa, utakaogharimu zaidi ya Shilingi Bilioni mia moja.

Akizindua Ujenzi wa mradi huo Jijini Dar es salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James, amesema kuwa Fedha hizo zimetolewa kama Mkopo wenye Masharti nafuu na Benki ya uwekezaji ya Ulaya kwa ajili ya kuboresha huduma za usafiri na usafirishaji wa Abiria katika maeneo hayo ya kimkakati.

Aidha Doto amewataka Wakandarasi wa Miradi hiyo kutekeleza kwa mujibu wa makubaliano huko akimuagiza Mtendaji mkuu wa wakala wa Barabara Tanzania-Tanroads, Mhandisi Patrick Mfugale, kusimamia kwa karibu Ujenzi wa Mradi hiyo.

Kwa upande wake Mtendaji mkuu wa wakala wa Barabara Tanzania-Tanroads, Mhandisi Patrick Mfugale, amesema Ujenzi wa Viwanja hivyo utahusisha upanuzi wa njia za kurukia Ndege, Majengo ya Abiria, Barabara za Lami za kuingia Uwanjani na Ujenzi wa Maegesho ya Magar

Akizungumza kwa niaba ya wakuu wa Mikoa ambako Miradi inaenda kutekelezwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma nd. Rashidi Mchata, amesema ukamilishaji wa Miradi hiyo utasaidia kuunganisha shughuli za Uchumi katika Mikoa ya pembezoni ya Nchi.

Utekelezaji wa Miradi hiyo ni mwendelezo wa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt John Pombe Magufuli na ile ya Awamu ya saba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Chini Rais Dr. Alli Mohed Shein ya kuboresha usafiri wa Anga Nchi.

 

DROO YA HATUA YA ROBO FAINALI YA MASHINDANO YA YAMLE YAMLE

Droo ya Hatua ya Robo Fainali ya Mashindano ya Yamle Yamle imepangwa leo katika studio ya Zbc TV ambapo hatua hiyo inatarajiwa kuanza ijumaaya wiki hii katika uwanja wa Mao Zedong’s jioni ya leo

Akiifungua droo hiyo Katibu Mkuu msaidizi wa kamati ya TOC amesema mashindano hayo yamekuwa sehemu ya kuinua vipaji na kuwaendeleza vijana katika fani yao hiyo ya mpira wa miguu.

Timu ya Manchester Camp kutoka Uroa ambao walikuwa wakijulikana kwa jina hilo kwa sasa wamebadilisha na kujulikanauroa Heroes watacheza dhidi ya Munduli Combin siku ya Ijumaa.

Wakati siku ya Jumamosi Mbirimbini watacheza na Mazombi Fc.

na siku ya jumapilitra watachuana na Mboriborini.

Wakati Robo Fainali ya mwisho Vijana wa Donge Heroes wakwaana na Meli Nne City ambao awali wakijulikana kwa jina la New Juver.

Mratib wa Michuano hiyo na Mwenyekiti wa Kamati ya Yamle Yamle wamesema michuano hiyo imeitikiwa kwa kiwango kikubwa.

 

USHIRIKIANO NI NYENZO MUHIMU KATIKA UTENDAJI KAZI AMBAYO INALIWEZESHA TAIFA KUWA NA MAENDELEO

Waziri wa Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati  Mhe. Salama Aboud Talib amesema umoja na Ushirikiano  ni  nyenzo muhimu katika utendaji kazi  ambayo inaliwezesha Taifa kuwa na maendeleo endelevu na kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Akizungumza na Wafanya kazi wa Wizara hiyo wakati wa kuagana Ofisini kwake Mhe. Salama amesema Wizara imefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika malengo iliyojiwekea pamoja na kutekeleza wajibu wa Serekali kutokana na ushirikiano uliokuwepo baina yao.

Kwa upande wao Wafanyakazi wa wizara hiyo wamempongeza Waziri Salama pamoja na Serekali ya Awamu ya 7 ya Dk Ali Mohd Shein kwa kutekeleza vyema ilani ya Chama cha Mapinduzi CCM katika sera mbalimbali.

Ghafla hiyo imeambatana na upokeaji wa zawadi zilizo tolewa na Wafanyakazi wa Wizara ya Ardhi, Nyumba, maji na Nishati ikiwa ni sehemu ya kuonyesha upendo wao na kumuaga baada ya kufanya nae kazi kwa kipindi cha miaka mitano.