Daily Archives: October 20, 2020

DK. SHEIN AMEWAAGA WANANCHI WA ZANZIBAR NA KUWAAMBIA KUWA AWAMU YA SABA IMEFANYA MAMBO MENGI

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amewaaga Wananchi wa Zanzibar na kuwaambia kuwa Awamu ya Saba imefanya mambo mengi huku akisema kuwa anawaachia zawadi ya Amani na Utulivu.

Dk. Shein aliyasema hayo leo huko katika viwanja vya Mao Dze Dong, Jijini Zanzibar katika hotuba yake ya kuwaaga wananchi wa Mikoa Mitano ya Zanzibar pamoja na kuzindua Dira ya Maendeleo ya Zanzibar ya mwaka 2050.

Hafla ambayo imehudhuriwa na viongozi mbali mbali akiwemo Makamo wa Rais wa  Jamahuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan, Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, Mama Mwanawema Shein, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ambaye pia ni mgombea kwa tiketi ya CCM Dk. Hussein Ali Hassan Mwinyi, Mawaziri, na viongozi wengine wa vyama vya siasa, dini na serikali.

Katika maelezo yake, Rais Dk. Shein alisema kuwa mbali ya jitihada alizozichukua za kuwaachia wananchi mifumo na vitu ambavyo vitarahisisha mwenendo wao wa kujipatia huduma za maisha vile vile anawaachia zawadi ya amani na utulivu.

Rais Dk. Shein aliwasishi wananchi kuzidisha upendo, umoja na mshikamano miongoni mwao ili zawadi hiyo anayowaachia iweze kudumu na kung’ara zaidi.

“Zawadi hii ya amani na utulivu mtaweza kuitumia nyinyi na vizazi vitakavyokuja baadae kwa hivyo itunzeni sana na muilinde kwa nguvu zenu nyote”,alisema Rais Dk. Shein.

Aidha, Rais Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba bila ya kutetereka kinyume na matarajia ya wale waliokuwa hawaitakii mema imefanya mambo mengi kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.

Alisema kuwa Serikali imefanikiwa kuyatekeleza mambo ya maendeleo kwa kuzingatia shida na kero kadhaa zilizokuwa zikiwakabili wananchi kwenye huduma za msingi za amii.

Aliongeza kuwa wananchi wamekuwa wasikivu katika kufuata taratibu na sheria za nchi mambo ambayo taasisi zilizopewa majukumu ya ukusanyaji wa mapato zimeweza kufanya vizuri sana.

Dk. Shein aliwapongeza wananchi kwa usikivu wao hasa pale lilipotokea janga la COVID 19 ambapo waliweza kufuata maelekezo yote ya Serikali na yeye pamoja na Serikali anayoiongoza kwa mashirikiano na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Magufuli walikuwa makini katika kuwapa maelekezo wananchi.

Alisema kuwa wananchi wa Zanzibar kila pembe wanathamini jitihada zilizochukuliwa na Serikali yao katika kuleta maendeleo yenye manufaa kwao na kuziunga mkono jitihada za Serikali katika kuleta maendeleo yenye ufanisi ambayo wanajivunia.

Rais Dk. Shein alitoa shukurani kwa zawadi alizotunukiwa na wananchi na kueleza kuwa hicho ni kielelezo cha jinsi wanavyomjali na yeye kwa upande wake anawajali, anawathamini na anawapenda wote wananchi wake.

Katika hotuba yake hiyo aliwapongeza viongozi wote wakuu wa SMZ na SMT pamoja na uongozi wa Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na wataalamu wote wa Tume ya Mipango kwa kuiwasilisha Dira ya Zanzibar 2015 kwa wananchi pamoja na kuwapongeza wakuu wa vikosi vya SMZ na SMT.

Aliwapongeza viongozi wote wa Chama na Serikali pamoja na Wakuu wa Mikoa Mitano ya Zanzibar na Wilaya, watendaji wengine wote, masheha na Madiwani pamoja na Wazee wa CCM kwa busara, hekima na maendeleo yao ambayo kwa wakati wote yalikuwa na manufaa kwa ustawi wa nchi.

Kwa upande wa Dira ya Maendeleo ya Zanzibar ya mwaka 2050 imetengenezwa kwa utaalamu wa hali ya juu kutokana na uzoefu ambao wataalamu wazalendo wamekwishaupata kwenye shughuli ya namna hiyo.

Alisema kuwa maandalizi ya Dira ya 2050 yamezingatia mabadiliko ya haraka ya sayansi na teknolojia duniani fursa  zinazojitokeza katika sekta zinazoibua zikiwemo uchumi wa kutumia rasilimali za bahari (uchumi wa Buluu), mtehama, mafuta na gesi asilia.

Aliongeza kuwa katika Awamu ya Saba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, imepata mafanikio mengi kupitia utekelezaji wa Dira ya 2020 na mafanikio makubwa yamepatikana hiyo ni kutokana na kuwa yako wazi.

 

Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein aliwahimiza wananchi kwa kila aliyetimiza masharti yaliyowekwa na Tume kujitokeza kwa wingi siku ya tarehe 28 Oktoba, 2020 kwenda kupiga kura ili wasipoteze haki yao ya demokrasia.

Aliwataka wananchi kuchagua viongozi wakweli na wenye nia njema ya kuwaletea wananchi maendeleo yanye manufaa na wala wasichague viongozi wanaotaka kuielekeza nchi katika shari na mfarakano.

Aliwataka kuangalia maslahi ya nchi yao ambayo ndiyo yatakayowawezesha kuishi vizuri wakiwa nchini mwao “Wahenga wanasema mtu kwao ndio ngao na anayebomoa kwao ni mtumwa”, alisisitiza Dk. Shein.

Nae Waziri wa Fedha na Mipango Balozi Muhammed Ramia Abdiwawa  alieleza kuwa Dira hiyo ni ya watu wote na Dira ya 2020 Rais Dk. Shein aliisimamia na hiyo mpya inatokana na miongozo yake huku akisema kuwa Dira ya 2050 ni ya vijana zaidi.

Alisema kuwa Dira hiyo itajikita zaidi katika mageuzi ya Kiuchumi na kusisitiza kuwa Dira hiyo itakuwa ndio muongozo wa miaka 30 ijayo ambayo imefanywa na wataalamu wa ndani kwa mara ya kwanza na kuwashikirisha wananchi hadi vijijini na ambayo itapekekea kufikia uchumi wa juu ifiapo 2025 ambapo kila mwananchi anatarajiwa kuwa na kipato cha Dola za Marekani 4400 kwa mwaka.

Mapema Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango Mwita Mgeni alitoa historia ya kuundwa Dira hapa nchini na kusema kuwa utayarishaji wa Dira ya Maendeleo ya 2050 ilipitia kwa wadau mbali mbali ikiwa ni pamoja na Kamati ya Makatibu Wakuu, wajumbe wa Tume ya Mipango na hatimae ridhaa ya Baraza la Mapinduzi.

Alisema kuwa Dira hiyo ina muundo na lengo ni kuifikisha Zanzibar katika uchumi wa kati wa kiwango cha juu ifikapo mwaka 2050, pamoja na vipaumbele kadhaa.

Alisema kuwa Dira hiyo itakuwa ni msingi imara wa kutoa mashirikiano ya pamoja katika maendeleo yatakayosukuma utendaji thabiti wa sekta binafsi katika kuendeleza uchumi

Nae Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Hemed Suleiman akisoma hotuba kwa niaba ya wananchi wa mikoa mitano ya Zanzibar alimpongeza Rais Dk. Shein kwa kuiwacha Zanzibar ikiwa na amani na utulivu sambamba na uongozi wake imara wenye hekima na busara.

Alisema kuwa Zanzibar inaendelea kuwa na amani na ndio maana imekuwa kivutio kikubwa cha watalii ambapo pia, katika uongozi wa Rais Dk. Shein kumepatikana mafanikio makubwa ikiwemo kuimarika kwa sekta za maendeleo ikiwemo kilimo, elimu, biashara,afya, maji safi na salama, kuimarika kwa sekta ya utalii, ujenzi wa barabara, majengo ya ofisi za Serikali, biashara na huduma nyengine.

Aidha, alieleza hatua alizozichukua za ujenzi wa misingi mikubwa ya maji ya mvua, pamoja na ujenzi wa madaraja, eneo la Mwanakwerekwe ambalo lilikuwa likituama maji huku akieleza historia aliyoandika kwa kuongeza mishahara kwa sekta ya umma na sekta binafsi.

Alisema kuwa wananchi wameridhika na uongozi wa Rais Dk. Shein pamoja na maendeleo aliyowaletea wananchi wa Zanzibar na kuahidi kuyadumisha na kuyaimarisha yale yote aliyowaachia.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ Haji Omar Kheri alizitaja zawadi alizotunukiwa Rais Dk. Shein pamoja na Mama Mwanamwema Shein kutoka kwa Mikoa yote Mitano ya Zanzibar.

Katika hafla hiyo burudani mbali mbali zilitumbuiza zikiwemo zile za asili pamoja na zile za kizazi kipya ambapo ngoma ya Tukulanga, Kibati zilitumbuiza pamoja na wasanii wa kizazi kipya akiwemo IT na ZUCHU.

 

DK. SHEIN AMEWAONGOZA WAUMINI WA DINI YA KIISLAMU KATIKA MAULIDI YA KUZALIWA MTUME MUHAMMAD (SAW)

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein jana aliwaongoza Waumini wa Dini ya kiislamu pamoja na Wananchi mbali mbali katika Maulidi ya kuadhimisha kuzaliwa Mtume Muhammad (saw) kitaifa yaliofanyika katika Viwanja vya Maisara Mjini Zanzibar.

Sherehe hizo za kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (S.A.W) ambazo hufanyika kila mwaka Kitaifa hapa Zanzibar ni miongoni mwa kawaida na mila ya Waislamu wa Zanzibar ambazo hapa nchini zilianzishwa mapema mnamo mwaka 1926.

Alhaj Dk. Shein aliungana na Waislamu pamoja na viongozi mbali mbali wa Serikali na viongozi wa Dini na wananchi akiwemo Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhaj Balozi Seif Ali Idd, Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Alhaj Ali Hassan Mwinyi, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Alhaj Dk. Hussein Ali Hassan Mwinyi, Mawaziri, Masheikh na viongozi wengine wa Serikali nao walihudhuria.

Nae, Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan aliungana na viongozi wengine wanawake wa Kitaifa akiwemo Mama Mwanamwema Shein, Mama Asha Balozi, Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Mgeni Hassan Juma na wengineo.

Naibu Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Hassan Othman Ngwali alitumia fursa hiyo kuwakaribisha wananchi pamoja na waliohudhuria katika Maulid hayo akiwemo Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein ambaye ndio mlezi wa Maulid hayo huku akimpongeza kwa wazo lake la Maulid hayo kusomwa mapema ili kuepuka kuingiliana na uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

Katika Sherehe  hizo, Waislamu walisisitizwa suala zima la kudumisha amani, umoja na mshikamano miongoni mwao na kutakiwa kufuata nyayo za Mtume Muhammad (S.A.W) ili wapate kuongoka hapa duniani na kesho akhera.

Akisoma khutba ya Maulid hayo, Sheikh Abdulaziz Saleh Juma kutoka Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana aliwataka  Waislamu kuwa kitu kimoja huku akiwasisitiza umuhimu wa  kusaidiana na kuvumiliana kwa lengo la kupata rehema za Allah.

Sheikh Hassan  pia, alitumia fursa hiyo kumpongeza Alhaj Dk. Shein kwa kuiongoza Zanzibar kwa muda wa miaka kumi na kufanya mambo mengi mazuri aliyoyafanya na kusisitiza kuwa kwa vile hakuna cha kumlipa ni vyema akaombewa dua.

Akisisitiza umuhimu wa amani na utulivu hasa katika kipindi hichi cha kuelekea uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika tarehe 28 mwezi huu, Sheikh Abdulaziz Juma alieleza haja ya kudumisha amani na utulivu ili heri zaidi izidi kupatikana hapa nchini. “Uchaguzi sio vita wala kuhatarisha amani na utulivu bali uchaguzi ni sehemu ya demokrasia hivyo wananachi tunapaswa kuwa kitu kimoja”, alisema Sheikh Abdulaziz.

Sherehe hizo za Maulid ambazo husherehekewa duniani kote, zilianza kufunguliwa na Qur-an tukufu iliyosomwa na  Ustadhi Idd Ussi Haji kutoka Tazari Mkoa wa Kaskazi ni Unguja, ambapo tafsiri yake ilitolewa na Sheikh Abdullah Hamid kutoka Chuo cha Kislamu Mazizini Unguja.

Milango  ya Maulid Barzanji iliyoenda sambamba na Qasweeda ilisomwa na Maustadhi kutoka vyuo mbali mbali vya Qur-an kutoka Unguja na Pemba yakiwemo Maulid ya Hom kutoka Jumuiya ya Maulid ya Hom Mtendeni, Mkoa wa Mjini Magharibi ambayo nayo yalikuwa kivutio kikubwa katika sherehe hizo adhimu.

Katika sherehe hizo za Maulid ya kuzaliwa Mtume Muhammad (S.A.W) Madrassa Noor El Islamiya ya Mji Mkongwe, Mjini Unguja walisoma Qiyaam Talaa, kilichotanguliwa na Mlango wa nne uliosomwa na Ustadhi Hassan Mdungi kutoka Tumbatu Jongowe, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Qasweeda ya mwaka 1442 Al Hijra, ilisomwa na wanafunzi kutoka Madrassa Nassur Iman ya Mtoni Kijundu, Wilaya ya Magharibi ‘A’ Mkoa wa Mjini Magharibi  ambapo  Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Maulid  Sheikh Sherali Chapsi alitumia fursa hiyo kama ilivyo kawaida kwa kila mwaka kumkabidhi Rais, Qasweeda hiyo maalum.

Maulid hayo yalimalizika kwa Mlango wa dua uliosomwa na Sheikh Abubaker Said Abubaker, kutoka Mji Mkongwe Unguja na hatimae kufungwa kwa fat-ha iliyosomwa na Naibu Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Mahmoud Mussa Wadi chini ya mshereheshaji Sheikh Hamza Zubeir Rijal.