Daily Archives: September 16, 2020

DK.SHEIN AMEONGOZA MAZISHI YA MGOMBEA NAFASI YA UBUNGE JIMBO LA MPENDAE KUPITIA CCM SALIM TURKY

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein  leo ameongoza mazishi ya Mwanasiasa Mkongwe na Mgombea nafasi ya Ubunge jimbo la Mpendae Zanzibar kupitia Chama cha Mapinduzi CCM Salim Hassan Abdullah Turky yaliyofanyika katika makaburi ya Kijitoupele mkoa wa Mjini Magharibi.

Viongozi mbali mbali wa vyama vya Siasa, Dini, Serikali na  sekta binafsi pamoja na Wananchi, Wafanyabiashara, Ndugu na Jamaa walihudhuria  katika Mazishi hayo akiwemo makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Mungano wa Tanzania Ali hassan Mwinyi.

Wengine ni Makamo wa Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Mohamed Gharib Bilal, mgombea nafasi ya Urais wa Zanzibar kupitia CCM Dk. Hussein Ali hassan Mwinyi,  Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabih pamoja na Naibu  kadhi Mkuu wa Zanzibar sheikh Hassan Othman Ngwali.

Mapema Alhaj Dk. Shein aliungana na Viongozi, Ndugu, Jamaa, Marafiki na Wananchi mbali mbali katika dua na sala ya kumsalia mMrehemu  Salim Hassan Abdullah Turky (Mr. White) katika msikiti wa “Noor Muhammad” uliopo Mombasa  Mjini Unguja.

 

Akisoma Wasifu wa Marehemu huko Kijitoupele katika eneo la Makaburi alipozikwa Marehemu, Waziri ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mohammed Aboud Mohammed alisema kuwa Marehemu Salim Hassan Abdullah Turky (Mr. White), aliyezaliwa februari 11 mwaka 1963 amefariki dunia usiku wa kuamkia leo septemba 15, 2020 huko katika Hospitali ya Tasakhtaa Global jijini Zanzibar.

 

Waziri Aboud alieleza kuwa Marehemu Salim Turky alikuwa Mfanyabiashara maarufu Zanzibar na muda mrefu hapa Nchini ambapo ameanza shughuli zake za biashara tangu miaka ya 1980 kwa kujishughulisha na uagiziaji na uuzaji wa bidhaa mbali mbali.

 

Aliongeza kuwa katika mwaka 1990 alijiunga na kuwa Mjumbe wa Jumuiya ya wafanyabiashara na wakulima zanzibar (Zanzibar National Chamber of Commence) na mwaka 2006 aliteuliwa kuwa Mdhamini wa Jumuiya hiyo hadi kifo chake.

error: Content is protected !!