Monthly Archives: August 2020

DK.SHEIN AMEUTAKA UONGOZI WA WIZARA YA VIJANA KUONGEZA KASI KATIKA UTENDAJI WA MAJUKUMU YAO YA KAZI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameutaka Uongozi na watendaji wa Wizara ya Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo  kuongeza kasi katika kipindi hiki kifupi kilichobaki kuelekea uchaguzi mkuu kwa kuwajibika katika utekelezaji wa majukumu ya kazi.

Dk. Shein amesema hayo Ikulu mjini Zanzibar, alipokutana na Uongozi  wa Wizara Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo wakati ilipowasilisha taarifa ya utekelezaji wa Mpango kazi wa mwaka 2019/2020 na mpango kazi wa mwaka 2020/2021.

Alisema kuna umuhimu mkubwa kwa viongozi hao kuongeza kasi katika usimamizi na uwajibikaji wa majukumu ya kazi kwa kuzingatia kuwa  shughuli za Serikali zinapaswa kuendelezwa kama kawaida hadi pale awamu ijayo ya uongozi wa Serikali itakapochukua nafasi yake.

Aliwataka watendaji hao kuendeleza mashirikiano yaliopo na  kubainisha kuwa hatua hiyo italeta tija kubwa.

Aidha, Dk. Shein alisema Zanzibar inahitaji kuwa na uwanja mkubwa wa kisasa utakaowezesha kufanyika shughuli mbali mbali za Kitaifa.

Alisema kuna umuhimu wa kuwa na uwanja wa aina hiyo,utakaokuwa na uwezo wa kufanyika matukio mbali mbali ya kitaifa, kama vile gwaride pamoja na michezo ya aina tofauti, ikiwemo mpira wa miguu.

Alisema uwanja uliopo wa Amani hauwezi kukidhi mahitaji ya wakati na hivyo akautaka uongozi wa Wizara hiyo kuangalia maeneo ya nje ya mji, likiwemo eneo la Tunguu ambalo limekusanya taasisi mbali mbali na Wizara za Serikali na kuwa katika mpango huo.

Katika hatua nyengine, Dk. Shein alipokea salamu na kuupongeza uongozi wa Wizara hiyo kwa hatua yake ya kuwatembelea wasanii wakongwe na walioiletea sifa kubwa Zanzibar, ambapo hivi sasa wamepumzika kutokana na uzee au kukabiliwa na maradhi mbali mbali.

Alisema utaratibu wa kuwatembelea wasanii hao ni jambo jema na linalopasa kuendelezwa na kufanyika takriban mara mbili kwa mwaka ikiwa ni hatua ya kuunga mkono na kuthamin juhudi walizofanya, sambamba na kukubali wazo la kuanzisha mfuko wa kuwasaidia wasanii wa aina hiyo na hivyo akautaka uongozi huo kufikiria namna ya kuwa na chanzo cha mapato kitakacholeta ustawi bora wa maisha yao.

“Serikali itajitahidi kuona namna gani inaanzisha mfuko wa wasanii, haiwezekani mtu huyo alitumia muda mwingi kuimba………..watu kama hawa lazima tunatanabahi na tuwakumbuke waliipamba nchi yetu”, alisema.

Aidha, Dk. Shein aliutaka uongozi wa Wizara hiyo kulishughulikia na kulipatia ufumbuzi suala la matumizi ya muda wa ziada wa  Studio ya Muziki na Filamu iliopo Rahaleo, ili kuondokana na kilio cha wasanii.

Aliipongeza Wizara hiyo kwa kwa kufanya maandalizi mazuri na uwasilishaji bora wa taarifa ya Utekelezaji wa mpango kazi.

Nae, Katibu Mkuu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee aliwatanabahisha watendaji wa Wizara hiyo kuwa makini katika usimamizi wa mali na rasilimali za Serikali, wakati Taifa likielekea kwenye Uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu, na kubainisha kuwa shughuli zote za serikali  zinapaswa kuendelea kama kawaida, sambamba na kuwataka kukamilisha malengo waliyojiwekea.

Mapema Waziri wa Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Balozi Ali Abeid Karume alielezea baadhi ya mafanikio yaliopatikana na Wizara hiyo katika kipindi hicho, ikiwa pamoja na kutekelezwa kwa Programu ya Ajira kwa vijana, ambapo jumla ya vijana 3,490 wamenufaika na program hiyo.

Alisema Wizara hiyo inaendelea na uimarishaji wa kiwanja cha Amani kupitia bajeti yake ya 2019/2020 ambapo shughuli za ujenzi wa mkeka “base” inaendelea vizuri, huku kazi za uwekaji wa nyasi bandia zikitarajiwa kuanza  mara tu unafuata baada kukamilika kazi hiyo.

Aidha, alisema vifaa vya matangazo ‘scoreboard’ vimewashawili na shughuli za uwekaji wa ubao huo unatarajiwa kuanza kipindi kifupi kijacho.

Alieleza kuwa kazi za ujenzi wa viwanja katika Wilaya  za Unguja  ikiwemo kiwanja cha Mkokotoni (Wilaya Kaskazini “A”), kinachojengwa  na Wizara Ujenzi, Mawasilianio na Usafirishaji kupitia Wakala wa Barabara Zanzibar zimeanza.

Alieleza kuwa Wizara hiyo tayari imepokea makisio ya Ujenzi wa kiwanja kiliopo Kama (Wilaya Magharibi A), huku hatua za kuomba Fedha Wizara ya Fedha na Mipango ikiwa tayari zimechukuliwa.

Waziri Karume alibainisha kuwa Wizara hiyo imeanza kukisaidia kituo cha michezo cha JKU (JKU Sports Academy) kwa kukipatia vifaa mbali mbali vya michezo, vitanda, magorodo pamoja na kugharamia huduma mbali mbali za vijana waliopo kituoni hapo, ambapo vijana 130 wananufaika na programu hiyo wakiwemo wachezaji wa mpira miguu na waamuzi wadogo.

Wakati huo huo; Dk. Shein alikutana na Uongozi wa Wizara ya Fedha na Mipango na kuupongeza uongozi na wafanyakazi wa Wizara hiyo waliopo Unguja na Pemba kwa utekelezaji mzuri wa majukumu yao, sambamba na kuwasilisha vyema taarifa ya Utekelezaji ya Mpango kazi.

Nae, Waziri wa Wizara hiyo Balozi Mohamed Ramia, alisiisitiza umuhimu wa jamii kulipa kodi na kusema kutokana na athari za Ugonjwa wa Corona zilizolikabili Taifa na Dunia, Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) Tawi la Zanzibar ilikusanya shilingi Bilioni 279.70  sawa na asilimia 80 ya matarajio ya kukusanya shilingi Bilioni 350.20 kwa mwaka.

Alisema shilingi Bilioni 21, ikiwa sawa na asilimia 100 ya makadirio ya kipindi hicho yalitokana na chanzo cha kodi ya wafanyakazi wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, katika ofisi ziliopo Zanzibar.

Serikali imejiwekea mpango  maalum wa miaka miwili ili kuhuisha mapato baada ya  athari za ugonjwa wa Corona, kwa lengo la kuimarisha uchumi wake.

Katika vikao vyake vya leo, pia Rais Dk. Shein alikutana na Uongozi wa Wizara ya Habari, Utalii na Mambo ya Kale……………………..

Mapema, Waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale, Mahamoud Thabit Kombo alisema katika kipindi cha miaka kumi ya uongozi wa Dk. Ali Mohamed Shein, Wizara hiyo imepata mafanikio makubwa katika sekta za habari, utalii pamoja na mambo ya kale.

Alisema katika kipindi hicho, Wizara kupitia Shirika la Magazeti ya serikali Zanzibar  mnamo mwaka 2016 lilianza kuchapisha gazeti la Zanzibar leo lenye rangi katika kiwanda cha Wakala wa Uchapaji Zanzibar, hatua iliyorahisisha usambazaji wa gazeti hilo katika maeneo mbali mbali ya Zanzibar, mijini na vijijini.

Alieleza kuwa Wizara imefanikiwa kuyafanyia matengenezo makubwa maeneo ya kihistoria ya Kwa  Bihole, Mwinyi Mkuu, Fukuchani , Mkamandume na Mvuleni kwa gharama  ya shilingi Bilioni 14, na hivyo kuongeza idadi ya wageni wanaotembelea maeneo hayo sambamba na kuongeza mapato.

Aidha,  alisema katika kipindi hicho Kamisheni ya Utalii iliendelea kuandaa na kudhamini matukio mbali mbali yaliofanyika nchini, kama vile Stone town marathon,Tamasha la chakula cha asili Makunduchi, Mbio za Baiskeli za Afrika Mashariki, Tamasha la Utalii la Pemba, Sauti za Busara, Tamasha la nchi za Jahazi pamoja na maonyesho ya Utalii Zanzibar na kusema matamasha hayo yamesaidia sana kupunguza msimu mdogo wa utalii pamoja na kuongeza  siku za ukaazi kwa wageni wanaotembelea nchini.

Waziri Kombo aliipongeza Serikali chini ya Uongzi wa Dk. Shein kwa hatua ilizozichukua katika kukabiliana na ugonjwa wa Covid-19.

 

error: Content is protected !!