KIKAO cha Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi kilichokaa leo chini ya Mwenyekiti wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli kimezipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa mafanikio makubwa yaliopatikana.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambaye pia, ni Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein naye alihudhuria katika kikao hicho ambacho kimefanyika leo mjini Dodoma.
Katika taarifa ya Umma kuhusu kikao cha Kamati Kuu Maalum ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) iliyotolewa na Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi Humphrey Polepole ilieleza kuwa miongoni mwa mafanikio hayo ni utekelezaji mzuri wa Dira ya Taifa ya mwaka 2020/2025, Mwelekeo wa Sera za CCM kwa miaka ya 2010-2020, Ilani ya CCM ya 2015-2020 pamoja na usimamizi madhubuti wa Sera za kiuchumi nchini.
Kufuatia mafanikio hayo kwa kauli moja Kamati Kuu imeipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa mafanikio hayo makubwa yaliopatikana.
Aidha, taarifa hiyo ilieleza kuwa kikao cha Kamati Kuu ya CCM kilikaa leo kikiwa na lengo la kuandaa agenda ya Kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM.
Kwa maelezo ya Polepole Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM itakutana kesho tarehe 20 Agosti 2020 katika Makao Makuu ya CCM Mjini Dodoma.
Sambamba na hayo, taarifa hiyo ilieleza kwamba pamoja na kujali na kupitisha agenda za Kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa Kikao hicho cha Kamati Kuu kinakuwa cha kwanza baada ya Tanzania kuvuka na kuingia katika kundi la nchi zenye uchumi wa Kati.