Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein amesema Zanzibar imefanikiwa kupata mafanikio makubwa ya kiuchumi na kijamii kutokana na jitihada na uwezo wa viongozi na Wananchi wake.
Dk. Shein amesema hayo ikulu jijini Zanzibar, alipokutana na Uongozi wa Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na utawala bora ilipowasilisha taarifa ya utekelezaji wa mpango kazi kwa mwaka 2019/2020 na mpango kazi wa mwaka 2020/2021.
Alisema maendeleo makubwa ya kiuchumi yaliopatikana katika sekta mbali mbali, ikiwemo miundombinu na usafirishaji, upandishaji wa mishahara mara tano katika kipindi cha uongozi wake (miaka kumi), ongezeko la pencheni na mambo mengine kadhaa yanatokana na juhudi za serikali.
Alisema mafanikio hayo yamewezesha kupungua kwa utegemezi wa bajeti ya serikali kwa asilimia tano hivi sasa.
Dk. Shein aliutaka Uongozi wa ofisi hiyo kuandaa utaratibu wa kuwa na mipango ya mafunzo kwa Watumishi wa Serikali kwa kuzingatia mahitaji ya Wizara husika na Serikali kwa ujumla na kubainisha kuwa hiyo ndio kazi ya utumishi wa umma.
Aliwakumbusha viongozi na watendaji hao kuwa Ofisi hiyo ni ya heshima, hivyo ni vyema pale wanapohitaji kuwaandikia barua watumishi kwa dhamira ya kubainisha muda wao wa kustaafu, wakazingatia lugha nzuri ikiwa hatua ya kuthamin mchango waliotowa katika kipindi kirefu cha utumishi wao.
Aidha, aliuagiza uongozi wa ofisi hiyo kuweka kumbu kumbu za muhtasari wa ongezeko la mshahara na ulipaji wa posho katika mashirika ya serikali na kusisitiza wajibu wa waziri kuwa ndie mwenye mamlaka ya kuidhinisha kiwango cha malipo hayo baada ya kupendekezwa na bodi.
Alisema pamoja na mipango ya chuo cha Utumishi wa umma kuwa na azma ya kuendesha mafunzo ya uongozi , kinapaswa kuwa na mwelekeo wa mbali zaidi utakaolenga kukiimarisha na kukifanyia upanuzi, kama vile ujenzi wa hosteli kupitia mihula tofauti (robo mwaka, nusu mwaka au mwaka mzima).
Dk. Shein aliupongeza uongozi, watendaji na wafanyakazi wa wizara hiyo kwa utekelezaji mwema wa majukumu ya kazi zao pamoja na maandalizi na uwasilishaji mzuri wa taarifa ya utekelezaji wa mpango kazi, sambamba na kuwataka kuendelea kujitahidi katika kujenga uwezo ili kutekeleza vyema wajibu wao, akibainisha zanzibar inahitaji kujengwa na watu wote.
Aidha, makamu wa pili wa rais wa zanzibar, balozi seif ali idd alisema pamoja na mafanikio makubwa yaliopatikana na ofisi hiyo, kutokana na kuwepo kwa uongozi bora, kuna dhana iliyojengeka miongoni mwa jamii kuwa ni vigumu kwa mwananchi kupata ajira serikalini hadi apate msukumo, huku taarifa zaidi zikihusisha baadhi ya watendaji kuuza ajira hizo.
Aliitaka mamlaka ya kuzuia rushwa na kuhujumu uchumi zanzibar (zaeca) kuendleea kufanya kazi zake kwa umakini na weledi mkubwa ili kukabiliana na tatizo la rushwa, akibainisha serikali zote mbili (SMZ na SMT) zimekuwa zikipiga vita suala hilo.
Nae, katibu mkuu wa baraza la mapinduzi na katibu mkuu kiongozi, dk. Abdulhamid yahya mzee aliwapongeza vongozi, watendaji na wafanyakazi wa ofisi hiyo kwa mashirikiano yao yaliowawezesha kutekeleza vyema majukumu yao.
Alisema ni vyema ofisi hiyo ikaendeleza utaratibu wa kutayarishaji taarifa ya utekelezaji wa mpango kazi (bango kitita), kwani ni nyenzo muhimu katika kutathmin mafanikio na changamoto zinazojitokeza pamoja na kubadilishana mawazo.
“Kuelekea kipindi hiki cha uchaguzi mkuu, ni vyema kuhakikisha kunakuwepo udhibiti wa mali za serikali , serikali ipo na katika kipindi hiki inazuia kabisa uuzaji wa mali zake”, alisema.
Mapema, waziri ofisi ya rais, utumishi wa umma na utawala bora haroun ali suleiman alimpongeza rais dk. Shein kwa busara na uadilifu mkubwa katika uongozi wake, hivyo kujenga uwazi wa ofisi hiyo, na kusema pamoja na mambo mengine alifanikiwa kurekebisha mishahara ya wafanyakazi wa serikali mara kadhaa.
Alisema katika kipindi hicho ofisi hiyo ilifanikiwa kutekeleza kwa mafanikio makubwa mambo mbali mbali, ikiwemo kuratibu na kuendesha mafunzo ya maandalizi ya kustaafu kwa watumishi 550 wa wizara, mashirika ya umma pamoja na taasisi mbali mbali zinazojitegeemea.
Alisema ofisi hiyo ilikamilisha zoezi la uhakiki wa malipo ya mshahra na posho kwa wizara 13 za serikali ya mapinduzi ya zanzibar, idara pamoja na taasisi mbali mbali.
Aidha, alisema ofisi ilitangaza nafasi za ajira 5,083 katika utumishi wa umma unguja na pemba pamoja na kuanzisha wakala wa serikali mtandao.
Alieleza kuwa ofisi hiyo pia ilifanya mapitio ya sheria ya utumishi wa umma ya mwaka 2011 na kuanda mapendekezo ya marekebisho ya sheria hiyo, sambamba na kukamilisha utafiti kuhusu tathmin juu ya uwajibikaji wa watumishi wa umma.“ofisi iliingiza taarifa za awali za viongozi katika mfumo wa kielektronik wa kusajili taarifa za mali na madeni ya viongozi”, alisema.
Nae, mshauri wa rais pemba, dk. Maua abeid daftar alimpongeza rais dk. Shein kwa kuanzisha sheria ya utawala bora,hatua iliyolifanya taifa kuwa na amani na utulivu, hususan katika kipindi kama hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.
Aliipongeza serikali kwa kusimamia vyema upatikanaji wa ajira kwa vijana, na kutoa rai kwa vyombo vya ulinzi na usalama kuchukua hatua za haraka pale litakapojitokea tukio la kiongozi wa serikali kuuza ajira.
Wakati huo huo,Dk shein alikutana na uongozi wa ofisi ya rais na mwenyekiti wa baraza la mapinduzi ameshukuru viongozi, watendaji na wafanyakazi wa ofisi ya rais na mwenyekiti wa baraza la mapinduzi kwa kazi nzuri waliyofanya katika kipindi chake cha uongozi, sambamba na kuandaa na kuwasilisha vyema taarifa ya utekelezaji wa mpango kazi (bango kitita).
Alisema kuna umuhimu wa kutumia uzoefu waliopata na kuendeleza kasi katika kulitumikia taifa katika kipindi kijacho cha uongozi wa serikali.
Aidha, aliwataka kuimarisha uhusiano na ushirikiano uliopo na kuepuka matabaka kwa kuzingatia kuwa wote ni wajiriwa wa Serikali.
Dk. Shein aliwataka watendaji hao kutumia vyema mafunzo wanayoyapa kazini na kuyatumia katika kukabiliana na changamoto mbali mbali katika maisha yao ya baadae.
Vile vile alisisitiza na kuwataka watendaji hao kujiendeleza kielimu ili kuwa na upeo wa kutekeleza vyema majukumu ya kazi, sambamba na kuzingatia ukweli na uwazi.
Dk. Shein alisema milango iko wazi pale atakapostaafu kwa kiongozi au mfanyakazi kwenda kuchota ushauri wenye lengo la kuendeleza maendeleo ya taifa.
Aliweka wazi kuwa hatokuwa tayari kupokea majungu au maneno ya fitna yatakolenga kuleta sintofahamu, hususan kwa serikali.
Aidha, dk. Shein aliahidi kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya viongozi wa taifa wastaafu (marais)ikiwa ni hatua ya kuleta ustawi bora wa taifa.
Nae, Katibu Mkuu wa Baraza la Mapinduzi na katibu mkuu kiongozi dk. Abdulhamid yahya mzee alimshukuru dk. Shein kwa kumuamini katika muda wote wa uongozi wake na hivyo kupata fursa ya kujifunza mambo mengi kutoka kwake.
Dk. Abdulhamid aliwataka watendaji na wafanyakazi wa ofisi hiyo kuyaendeleza yale yote mema na yalioiletea sifa ofisi hiyo, ikiwemo utunzaji wa siri za serikali, akibainisha kutokuwepo tukio lolote la uvujishaji wa siri za baraza la mapinduzi.
Alisistiza umuhimu wa viongozi, watendaji na wafanyakazi kuendelea kufanyakazi kwa umakini na utulivu sambamba na kutunza vyema mali za serikali.
Mapema, waziri ofisi ya rais na mwenyekiti wa baraza la mapinduzi issa haji ussi ‘gavu’ alimshukuru dk. Shein kwa kusimamia na kutekeleza kwa vitendo ilani ya ccm ya mwaka 2015 – 2020.
Alisema katika kipindi hicho ofisi hiyo imepata mafanikio makubwa ikiwemo kuratibu kwa ufanisi ziara ya kikazi iliofanyika nchi za umoja wa falme za kiarabu, iliokuwa na lengo la rais dk. Shein kushuhudia utiaji wa saini wa mkataba wa fedha za msaada wa dola milioni kumi kutoka mfuko wa khalifa fund.
Alisema katika kuendeleza utoaji wa motisha kwa wanafunzi, ofisi hiyo iliwaandalia chakula malum wanafunzi bora 375 waliopata daraja la kwanza katika mtihani wa kidato cha nne (f.iv) na wanafunzi bora 187 wa kidato cha sita (f.vi).
Aidha, alisema ofisi ilifanikiwa kuandaa kongamano la sita la wana diaspora wa tanzania katika ukumbi wa hoteli ya verde iliopo mtoni unguja.
Kwa upande wake, mshauri wa rais kisiwani pemba dk. Mauwa abeid daftari, alimpongeza dk. Shein kwa kuyafanyia ukarabati mkubwa majengo ya ofisi katika ikulu za chakechake na micheweni pamoja na kufanikisha ujenzi wa majengo na nyumba mpya.
Nao, wafanyakazi wa ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa baraza la mapinduzi, walimtakia kheri na maisha mema dk. Shein baada ya kuliongoza taifa kwa mafanikio katika kipindi cha miaka kumi.
Walisema juhudi kubwa alizofanya zimeliwezesha taifa kupiga hatua kubwa za maendeleo kupitia nyanja mbali mbali pamoja na kuleta ustawi bora wa wafanyakazi, hususan katika uimarishaji wa miundombinu ya kufanyia kazi na upatikanaji wa taaluma.