Daily Archives: August 18, 2020

DK. SHEIN AMEITAKA MANISPAA YA MJI WA ZANZIBAR KUHAKIKISHA USAFI KATIKA MAENEO YAKE

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameueleza uongozi wa Mkoa wa Mijini Magharibi pamoja na Manispaa yake kuhakikisha mji wa Zanzibar unakuwa safi kwani tayari hivi sasa unahadhi ya Jiji.

Hayo aliyasema leo, Ikulu Jijini Zanzibar alipokutana na uongozi wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ wakati ilipowasilisha Taarifa ya utekelezaji wa Mpango Kazi wa Mwaka 2019/2020 na Mpango Kazi wa mwaka 2020/2021 ambapo Makamo wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd alihudhuria.

Alieleza kuwa kuna haja ya kuweka mikakati maalum katika kuhakikisha mji wa Zanzibar unaendelea kuvutia na kufikia malengo laye ya kuufanya kuwa Jiji kutokana na sifa zote ulizonazo.

Rais Dk. Shein alisema kuwa ipo haja kwa uongozi wa Mkoa kuangalia suala zima la usafi hasa katika masoko na barabarani kwani wengi ya wafanyabiasahra wamevamia maeneo hayo na hatimae kuufanya mji kutokuwa msafi sambamba na kuepuka ajali ambazo zinaweza kutokea kutokana na kufanya biashaara maeneo ya barabara.

Pia, Rais Dk. Shein alieleza haja ya uongozi wa Mkoa huo kufanya kazi kiserikali kwa kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizokuwepo katika kuhakikisha biashara zote zinafaywa kwa kufuata taratibu na sheria zilizopo.

Alieleza kuwa licha ya Serikali kubuni mpango wa masoko mapya lakini hata hivyo katika eneo la soko la Mwanakwerekwe bado pamekuwa na msongamano mkubwa wa wafanyabishara ambao hufanya shughuli zao hizo pembezoni mwa barabara.

Alieleza haja ya kuandaa utaratibu maalum wa kuwaweka wafanyabiashara katika mazingira mazuri pale wanapowaondoa kutoka eneo moja kwenda eneo jengine kwa ajili ya kufanya biashara zao.

Alipongeza hatua za kuanzisha mnada mkuu huko katika soko jipya la mnada la Jumbi hali ambayo imesaidia kwa kiasi kikubwa kuondoa msongamano wa wafanyabiashara masokoni.

Rais Dk. Shein alisema kuwa Ofisi hiyo ya Rais kupitia Idara zake Maalum za SMZ zimesaidia kwa kiasi kikubwa kulinda amani na utulivu hapa Zanzibar.

Alieleza kuwa utaratibu wa vikao hivyo vya kufanya tathmini na kuripoti (Bango Kitita), umekuwa ukitumika sehemu mbali mbali duniani na kwa upande wa Serikali ya Zanzibar tokea alipouanzisha umeweza kupata mafanikio makubwa.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein alisema kuwa Zanzibar imepiga hatua kubwa ambapo mafanikio yaliopatikana ni pamoja na kukua kwa uchumi wake na kufikia uchumi wa kati hatua ambayo imetokana na makusanyo mazuri ya mapato.

Aliongeza kuwa maafanikio hayo ndio yametoana na uendelezaji na uanzishwaji wa miradi kadhaa ya maendeleo ukiwemoujenzi wa nyumba za Kwahani, ununuzi wa meli, ujenzi wa maduka makubwa ya kisasa hapo Michenzani, uanzishwaji wa ukarbati wa uwanja wa Amaan, ujenzi wa barabara Unguja na Pemba, ujenzi wa daraja la Dk. Shein na mengineyo ambayo yote yanatokana na fedha za SMZ.

Rais Dk. Shein aliupongeza uongozi wa Ofisi hiyo pamoja na wafanyakazi wake huku akiwataka viongozi hao kuendelea kuchapa kazi na kuweka heshima ya nchi yao na Mapinduzi yao ya Januari 12, 1964 pamoja na Muungano uliopo kati ya Tanganyika na Zanzibar ambao umeasisiwa na Hayai Mzee Karume na Hayati Mwalimu Nyerere.

Nae Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd alimpogeza Rais Dk. Shein kwa utaratibu wake huopamoja na kuupongeza uongozi wa Ofisi hiyo kwa juhudi kubwa walizozichukua huku akiwasasitiza kuimarisha miundombinu ya elimu, afya pamoja na kilimo katika kuwahudumia wananchi.

Mapema Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ Haji Omar Kheri alisema kuwa Ofisi imeendelea kuhudumia skuli 327 za maandalizi na msingi kwa kuhakikisha zinatoa huduma ya ufundishaji na kujenga mazingira mazuri ya kujifundishia.

Alisema kuwa ununuzi wa madaftari 4,624,846 ya kuandikia kwa wanafunzi 325,009, madaftari 5,500 ya mahudhurio na kadi 50,000 za maendeleo ya wanafunzi umefanyika na kusambazwa kila Wilaya za Unguja na Pemba na kuwawezesha wanafunzi wote kuwa na mabuku ya kuandikia bila ya gharama za wazazi.

Huduma za tiba na kinga ya afya ya msingi pamoja na huduma za afya ya mama na mtoto zimetolewa katika vituo 154 vya afya Unguja na Pemba chini ya usimamizi imara wa Serikali za Mitaa.

Upatikanaji wa dawa muhimu, vitendanishi na vifaa tiba umekuwa mzuri unaotokana na jitihada za Rais Dk. Shein za kuimarisha sekta ya afya nchini na kuenzi tamko jengine la Serikali ya Mapinduzi la matibabu bure lililotolewa mwaka 1964.

Alieleza kuwa uwajibikaji wa Serikali za Mitaa katika kusaidia miradi inayoibuliwa na wananchi umeogezeka ambapo kwa mwaka 2019/2020 miradi ya maendeleo 59 yenye thamani ya TZS Bilioni 1.7 imetekelezwa kwa upande wa Unguja na miradi 17 yenye thamani ya TZS milioni 521.9 imetekelezwa Pemba.

Waziri Kheri alieleza historia aliyoandika Rais Dk. Shein ya kuanzisha rasmi Jiji la Zanzibar baada ya kufanya uteuzi wa Mkurugenzi wa Jiji kwa kumteua Ali Khamis Juma ambapo pia, Ofisi kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mji Magharibi iliratibu uchaguzi wa  Meya na Naibu Meya na kuapishwa Madiwani wa Baraza la Jiji.

Aidha, alipongeza hatua za Rais Dk. Shein za kuridhia na kuzipandisha hadhi Halmashauri za Wilaya ya Kaskazini A, Kaskazini B na Halmashauri ya Wilaya ya Kati kuwa Mabaraza ya Miji.

Alisema Ofisi kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais imeshiriki kikamilifu katika kupambana na maradhi ya Corona (COVID 19), mikakati mbali mbali imetekelezwa ikiwemo kuanzisha kambi za karantini kwa kila Wilaya ambapo jumla ya wananchi 715 walioingia kupitia bandari zisizo rasmi waliwekwa karantini na vyombo 7 vilivyobeba abiria kinyume na utaratibu vilikamatwa.

Aliongeza kuwa barabara ya Fuoni Mambosasa hadi Mwera Wilayani yenye urefu wa kilomita 3.4 na barabara ya Gombani hadi Pagali yenye urefu wa kilomita 1.8 zipo hatua za mwisho za uwekaji wa lami.

Sambamba na hayo, Waziri Kheir alisema kuwa usalama wa Jiji la Zanzibar, Mji wa Mkoani, Chake Chake na Wete umeendelea kuimarika kupitia utekelezaji wa mradi wa Mji Salama ambapo kwa mwaka 2019/2020 kazi ya uwekaji wa vizuizi vya kiusalama katika barabara kuu imefanyika kwa upande wa Unguja pamoja na kufuatilia matukio 256 yaliyoonekana katika kamera za kiusalama (CCTV).

Waziri Kheir pia, alieleza mchango mkubwa unaotolewa na timu za Idara Maalum za SMZ ambazo zimekuwa washindi wakubwa wa michezo na matamasha kadhaa nchini.

Nae Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee alisema kuwa mikutano hiyo ya (Bango Kitita) imekuwa na msaada mkubwa katika kujitathmini na kujipima na kueleza haja ya kuendelezwa huku akiwataka viongozi na wafanyakazi wa Wizara hiyo kuendelea kuchapa kazi hasa katika kipindi hichi cha kuelekea uchaguzi mkuu.

Nao viongozi wa Wizara hiyo walitoa pongezi kwa Rais Dk. Shein kwa kuwafanya kuwa makini na kujitathmini katika utendaji wa kazi zao na kueleza jinsi ya vikao hivyo vilivyowasaidia katika utendaji wa kazi zao.

Walieleza mafanikio yaliopatikana katika uongozi wa Rais Dk. Shein kutokana na maendeleo makubwa yaliopatikana Unguja na Pemba hali ambayo imepelekea vijiji vilivyokuwa havijulikani kujulikana huku wakieleza jinsi wananchi walivyofurahishwa na utaratibu aliouanzisha wa kusherehekea skukuu za Idd katika ngazi za Wilaya.

Viongozi hao walieleza mafanikio yaliopatikana kutokana na uwepo wa mradi wa Uimarishaji wa Huduma za Jamii Mijini (ZUSP) Unguja na Pemba.

DK. SHEIN AMETUMA SALAMU ZA PONGEZI KWA RAIS WA JAMHURI YA WATU WA INDIA

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein amemtumia salamu za pongezi Rais wa Jamhuri ya Watu wa India Shri Ram Kovind kwa kuadhimisha miaka 74 tokea Taifa hilo kupata huru wake.

Salamu hizo zilieleza kuwa wananchi wa Zanzibar wanaungana na ndugu zao wa Jamhuri ya India katika kusherehekea sikukuu hiyo adhimu ya uhuru wa Taifa hilo ambayo ni ya kihistoria.

Katika salamu hizo, Dk. Shein alimuhakikishia Rais Ram Nath Kovind kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendeleza uhusiano na ushirikiano wa kihistori uliopo kati yake na India sambamba na kuvumbua maeneo mapya ya mashirikiano kwa maslahi ya pande zote mbili.

Dk. Shein alimtakia kiongozi huyo na familia yake pamoja na wananchi wote wa India afya njema na sherehe njema katika kuadhimisha siku hiyo adhimu kwa Taifa hilo na kumtakia mafanikio zaidi ya kiuchumi kwa madhumuni ya kulinufaisha Taifa hilo na wananchi wake kwa amani na utulivu mkubwa.

Jamhuri ya India inasherehekea siku ya uhuru wa Taifa hilo kila ifikapo Agosti 15 ya kila mwaka ambapo nchi hiyo ilipata uhuru wake kutoka kwa Wakoloni wa Kiengereza mnamo mwaka 1947 chini ya uongozi wa muasisi na Baba wa Taifa hilo Hayati Mahtma Gandhi.

Wakati huo huo, Rais Dk. Shein alimtumia salamu za pongezi Rais wa Jamhuri ya Watu wa Indonesia Joko Widodo kwa kuadhimisha miaka 75 ya uhuru wa Taifa hilo.

Salamu hizo za Rais Dk. Shein alizozituma kwa Rais Widodo zilieleza kuwa uhusiano uliopo kati ya Zanzibar na Indonesia umekuwa ukiimarika kila siku na kusisitiza kuwa Zanzibar itaendeleza uhusiano na ushirikiano huo kwa ajili ya kuimarisha uchumi sambamba na kupambana na changamoto zilizopo.

“Bado kumekuwa na mahusiano mazuri kati ya Serikali zetu pamoja na watu wake ambao nao wamekuwa na mashirikiano na mahusiano mema kwa ajili ya kujiletea maendeleo hatua ambayo pia, imesaidia kuleta mafanikio”,alisisitiza Rais Dk. Shein.

Pamoja na hayo, Rais Dk. Shein alimtakia kiongozi huyo sherehe njema na mafanikio katika kuadhimisha siku hii adhimu ya Uhuru wa Taifa hilo huku akimtakia afya njema, maisha marefu yeye, familia pamoja na wananchi wake sambamba na  kumtakia maendeleo  endelevu ya uchumi katika Taifa lake.

Jamhuri ya Indonesia inasherehekea siku ya uhuru wa Taifa hilo kila ifikapo Agosti 17 ya kila mwaka ambapo nchi hiyo ilipata uhuru wake kutoka kwa Wakoloni wa Uholanzi mnamo mwaka 1945 chini ya uongozi wa muasisi wake Hayati Sukarno Raden Sukami Sosrodihardjo.

error: Content is protected !!