Daily Archives: August 14, 2020

DK. SHEIN AMEITAKA WIZARA YA ELIMU KUWATUMIA WANATAALUMA WAZALENDO WALIOBOBEA KWA MAENDELEO YA NCHI

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameupongeza Uongozi na Watendaji wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kwa kazi nzuri waliyofanya katika kipindi cha miaka kumi ya Uongozi wake.

Dk. Shein ametowa Pongezi hizo Ikulu Jijini Zanzibar, alipokutana na Uongozi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali wakati ilipowasilisha Taarifa ya utekelezaji ya mpango kazi kwa Mwaka 2019/2020 na mpango kazi wa Mwaka 2020/2021, ambapo pia Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd alishiriki.

Amesema Wizara hiyo yenye Idara na Taasisi kadhaa zinazotegemeana imepata mafanikio makubwa katika kuimarisha Sekta ya Elimu Nchini.

Katika Nasaha zake, Dk. Shein aliwataka Viongozi na Watendaji wa Wizara hiyo kuendeleza juhudi  zilizofanikisha mafanikio hayo, na kubainisha kuwa zimeleta sifa na Manufaa makubwa kwa Taifa na Wananchi wake.

Alisisitiza umuhimu wa kuendelea kushirikiana, kuwa wamoja na  kupendana, ili ujio wa Uongozi mpya uweze kuchochea kasi ya Maendeleo.

Dk. Shein aliutaka Uongozi wa Wizara hiyo kukaa na kufikiria njia ya kupata Fedha kupitia Mashirika mbali mbali ya kimataifa kama vile Benki ya Dunia na ADB  ili kuweza kuanzisha Jengo  jipya na la kisasa kwa ajili ya huduma za Maktaba litakaloweza kukidhi mahitaji ya wakati.

Aidha, aliiunga mkono azma ya Idara ya huduma za Maktaba ya kuwa na Maktaba katika kila Wilaya za Unguja na Pemba, kazi iliyoanza  utekelezaji wake katika Wilaya ya Kati Unguja.

Aliutaka Uongozi wa Wizara hiyo kuwatumia wana Taaluma Wazalendo waliobobea katika Masuala mbali mbali ya Kielimu yanayohitaji Ushauri, badala ya kazi za namna hiyo kuzitangaza kwa Wataalamu kutoka Nje ya Nchi.

Dk. Shein alitaka kufanyika juhudi za kuifanyia matengenezo Skuli ya Mkunazini kwa kufuata miongozo ya Mamlaka ya Mji Mkongwe, ili kuepuka athari zitakazojitokeza za kuanguka kwa Jengo hilo  na kuleta maafa.

Aliukumbusha Uongozi wa Wizara hiyo Umuhimu wa kuufufua Uwanja wa Michezo  uliopo Skuli ya Sekondari Lumumba kwa kupanda Majani ili uweze kutumika katika Mashindano mbali mbali ya Skuli za Sekondari, jambo ambalo zamani lilikuwa likifanyika.

Nae, Makamo wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Idd, alisema kumekuwepo Maktaba za aina mbali mbali, hivyo akautaka Uongozi wa Idara ya huduma za Maktaba kufanya juhudi za kuwahamasisha Wananchi na Wanafunzi kutumia Maktaba ziliopo ili kupanua wigo wa uwelewa.

Aidha, Katibu Mkuu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dkt. Abdulhamid Yahya Mzee aliipongeza Wizara hiyo kwa hatua kubwa za Maendeleo zilizofikiwa, na kuutaka Uongozi wa Wizara hiyo kuyalinda na kuyaendeleza Mafanikio hayo.

Vile vile aliutaka Uongozi wa Wizara hiyo kusimamia Utendaji bora wa kazi kwa Watumishi katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu, sambamba na kuondokana na Matumizi Mabaya ya Mali na Rasilimali za Serikali , ikiwemo uuzaji wa mali zake, hususan Magari.

Mapema, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Riziki Pembe Juma,  alisema katika kipindi hicho Wizara hiyo imepata mafanikio makubwa ya kuimarisha  Sekta ya Elimu, hatua  iliyotokana na juhudi kubwa za Serikali ya Awamu ya Saba, Chini ya Uongozi wa Rais Dk. Ali Mohamed Shein.

Aliyataja baadhi ya mafanikio hayo kuwa ni pamoja na  Ongezeko la Ufaulu wa Watahiniwa  katika Mitihani ya Taifa ya Kidato cha Nne (f.iv) Mwaka 2019 kwa Daraja la Kwanza, la Pili na Daraja la Tatu.

Alisema Ufaulu kwa Watahiniwa wa Daraja la Kwanza uliongezeka kutoka Watahiniwa 185 Mwaka 2018 hadi Watahiniwa 299 Mwaka 2019, huku Ufaulu wa Watahiniwa wa Daraja la Pili ukiongeka kutoka 903 (2018) hadi Watahiniwa 1,509 (2019).

“Watahiniwa  2,205 Walifaulu  katika Daraja la Tatu kwa Mwaka 2018 na kuongezeka hadi Watahiniwa 2,915 Mwaka 2019”, alisema.

Alisema Wizara hiyo ilifanikiwa kuajiri Walimu 665, Wakiwemo Walimu 216 wa Sayansi, Mwalimu Mmoja wa Masomo ya Ufundi pamoja na Walimu 448 wa Masomo ya Sanaa na Mkutubi.

Aidha, Alisema pamoja na Mafanikio yaliopatikana, Wizara hiyo ilikabiliwa na Changamoto mbali mbali, ikiwemo Ongezeko kubwa la Wanafunzi Wanaoandikishwa kuanza Madarasa ya Maandalizi na Msingi, ikiwa hali tofauti na uwezo wa Miundombinu ya Skuli ziliopo.

Vile vile alisema Wizara inakabiliwa na Deni la Shilingi Bilioni 1.65 linalotokana na Ada na Posho la Wanafunzi wanaosoma Elimu ya juu kutoka Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, ambalo linapswa kulipwa katika Robo ya kwanza ya Mwaka 2020/2021.

Wakati huo huo, Rais Dk. Shein alikutana na Uongozi wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Ameipongeza Wizara hiyo kwa juhudi kubw aza kuleta Maendeleo.

Nae, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Sira Ubwa Mamboya Alisema katika kipindi hicho Wizara hiyo kupitia Programu ya Miundombinu na Huduma za Usafirishaji imepata Mafanikio Makubwa ikiwemo kukamilisha Ujenzi wa Barabara mbali mbali Unguja na Pemba kwa Kiwango cha Lami kwa Urefu wa Kilomita 63.6.

Alizitaja Barabara hizo kuwa ni pamoja na Bububu-Mahonda – Mkokotoni _Kilomita 31, Pale – Kiongele km (4.6), Matemwe – Muyuni (km 7.6), Koani – Jumbi (km 3.2), Ole – Kengeja (km 13) pamoja na Barabara ya Donge – Muwanda Kilomita 4.2.

Aidha, alisema kupitia Programu ya Tehama Wizara imefanikiwa kuimarisha Miundombinu katika Sekta ya Afya kwa kuzinganisha na Mkonga wa Mawasiliano na Masine za X-ray ziliopo Kivunge na Makunduchi.

DK. SHEIN AMEIPONGEZA WIZARA YA KILIMO KWA KAZI WANAZOZIFANYA

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein aliutaka uongozi wa Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi kuendelea kufanyakazi kwani Wizara hiyo imepata mafanikio makubwa.

 Hayo aliyasema leo, Ikulu Jijini Zanzibar alipokutana na uongozi wa Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi wakati ilipowasilisha Taarifa ya utekelezaji wa Mpango Kazi wa Mwaka 2019/2020 na Mpango Kazi wa mwaka 2020/2021.

Rais Dk. Shein alieleza Imani yake kwamba zoezi hilo limesaidia kwa kiasi kikubwa katika kutathmini shughuli za Wizara za Serikali.

Alisema kuwa Serikali imeweka mkazo katika kufanya tafiti hatua ambayo imepelelekea kuanzisha Taasisi mbali mbali hapa nchini na kueleza kuwa kituo cha Utafiti cha Kizimbami ndio cha mwanzo katika nchi za Afika Mashariki hiyo ni kuonesha wazi kuwa Zanzibar imepiga hatua muda mrefu.

Aidha, alieleza kuwa Taasisi za utafiti zilizopo zikiwemo za Mifugo pia, ipo hapa Zanzibar hivi sasa ambayo imekuwa ikienda kwa kasi sambamba na Taasisi ya utafiti ya uvuvi na rasilimali za bahari.

Alisema kuwa taasisi hizo zimeundwa kwa ajili ya kuendeleza kilimo, uvuvi na afya kwa lengo la kuleta tija.

Pamoja na hayo, Rais Dk. Shein aliipongeza Wizara hiyo kwa juhudi zake za kudhibiti mali zisizorejesheka ukiwemo mchanga hali ambayo imepelekea kuongezeka kwa mapato ya Serikali kwa kiasi kikubwa.

Alieleza matumaini yake makubwa kuwa Zanzibar itakwenda mbele katika sekta ya kilimo kutokana na programu mbali mbali zinazotekelezwa na Wizara hiyo.

Nae Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi, Mmanga Mjengo Mjawiri alisema kuwa Wizara hiyo imelenga kuendeleza mageuzi katika sekta ya kilimo kwa kuifanya ya kisasa, jumuishi na chenye ushindani ambacho kinachangia sekta ya viwanda na utalii ili kuleta tija na maisha bora ya wananchi wa Zanzibar na maendeleo ya uchumi.

Alisema kuwa sekta ya kilimo ikijumuisha mazao, mifugo, uvuvi, misitu na rasilimali zisizorejesheka bado inaendelea kuwa ni muhimili mkuu wa uchumi wa Zanzibar.

Aliongeza kuwa sekta hiyo inatoa mchango wa moja kwa moja kwa wananchi katika kujikimu kimaisha ambapo asilimia 40 wameajiriwa na sekta hiyo na inakadiriwa kuwa zaidi ya asilimia 70 ya wananchi wanategemea sekta hiyo ambapo kwa mwaka 2019 imechangia asilimia 21.2 ya Pato la Taifa.

Akieleza kuhusu wizi  na uchimbaji holela wa rasilimali ya mchanga, Waziri Mjawiri alisema kuwa Wizara kwa kushirikiana na vikosi vya SMZ imeunda kikosi shirikishi cha doria ambacho kinaendelea kupambana na wizi na uchimbaji wa mchanga kiholela pamoja na udhibiti wa ukataji ovyo wa miti.

Alieleza Mpango Kazi wa mwaka 2020/2021 ambao umelenga kuleta Mapinduzi ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kutoka Kilimo duni cha kujikimu kuelekea kilimo endelevu cha kibiashara na chenye tija pamoja na uhifadhi na matumizi.

Aidha, alieleza kuwa jumla ya wafanyakazi 263 wameajiriwa ikiwemo wahudumu shambani, maafisa katika ngazi tafauti na wataalamu 68 kuanzia Digriihadi PhD,

Alieleza dhamira ya Wizara hiyo ya kuibadilisha sekta ya kilimo kuwa ya kibiashara kwa kushajiisha ukuaji wa viwanda vidogo vidogo, miradi ya kilimo, mifugo, uvuvi, misitu, utumiaji wa teknolojia za kisasa za uzalishaji na usindikizaji wa mazao ya kilimo, kuongeza uzalishaji pamoja na kuweka mazingira bora katika sekta hiyo.

Pia, alieleza kuwa Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2020/2021 inalengo la kujenga miundombinu ya umwagiliaji maji katika eneo la hekta 65 na kukarabati hekta 87 kupitia mradi wa ERPP pamoja na kukarabati hekta 87.

Kuongeza uzalishaji wa Mpunga kufikia wastani wa tani 50,000 pamoja na kuendelea kutoa huduma za matrekta na zana zake kwa wakulima na kufuatilia ukulima wa zao la mpunga katika eneo la ekari 33,800 pamoja na mazao mengine ya kilimo.

Wizara hiyo pia, ilieleza lengo la kufanya tafiti 26 za kisayansi ambapo 16 ni za kilimo, 5 za mifugo na 5 za uvuvi, kufanya tafiti za kiuchumi na kijamii kwa mujibu wa ‘Zanzibar Research Agenda’, kuwajengea uwezo watafiti wa kilimo, mifugo na uvuvi na kuimarisha miundombinu ya utafiti.

Nae Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee alisema kuwa mikutano hiyo ya (Bango Kitita) imekuwa na msaada mkubwa katika kujitathmini na kujipima na kueleza haja ya kuendelezwa huku akisisitiza haja kwa viongozi na wafanyakazi wa Wizara hiyo kuendelea kuchapa kazi hasa katika kipindi hichi cha kuelekea uchaguzi mkuu.

Nae Mshauri wa Rais Pemba Dk. Mauwa Abeid Daftari akichangia katika kikao hicho alieleza haja kwa Wizara hiyo kufanya tafiti za kutosha ili kuwasaidia wakulima katika kuendeleza sekta ya kilimo.

Nao viongozi wa Wizara hiyo walitoa pongezi kwa Rais Dk. Shein kwa kuwafanya kuwa makini na kujitathmini katika utendaji wa kazi zao na kueleza jinsi ya vikao hivyo vilivyoaza katika uongozi wa Rais Dk. Shein na vilivyowasaidia kwa kuwa na nidhamu na ubunifu katika utendaji wa kazi zao.

 

MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA IMESEMA HAKUNA MADHARA YALIYOTOKEA KUTOKANA NA TETEMEKO LA ARDHI

Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka  ya Hali ya Hewa TanzaniaTMA   Tawi la Zanzibar  Nd. Said Khamis Said Amethibitisha kutokea kwa Tetemeko la Ardhi hapo Jana Majira ya Saa Mbili Usiku  Lenye Ukubwa wa Kipimo cha  Richta  Tano Nukta Tisa katika Eneo la Mashariki la Mkoa wa Pwani katika Bahari ya Hindi.

Akizungumza na ZBC  Ofisini kwake amesema kwa upande wa Zanzibar hakukua na madhara makubwa yalioathiri maeneo ya Makaazi ya Watu kutokana na Tetemeko hilo kutokea kutokea katika Eneo la Chini ya Bahari ambapo Kiwango cha Tetemeko hilo halikufika Tsunami.

Ameeleza kuwa TMA  inaendelea kufuatilia Mifumo ya Hewa Baharini na kutoa taarifa endapo  kutajitokeza mwendelezo    wa matetemeko katika Eneo la Bahari.

Aidha Kaimu Mkurugenzi huyo Amewashauri Wananchi Kuachana na Ujenzi holela ambao utasaidia kuharibu Miundombinu na kuwaomba linapotokea Janga kama hilo kukaa katika Maeneo ya Wazi .

Kwa upande wa Wananchi wa Maeneo mbalimbali wa Mji wa Zanzibar wamesema Tetemeko hilo ni Mipango  ya Mwenyezi Mungu na kuwaomba Wananchi wenzao  kutotaharuki ili kuepusha Madhara yanayoweza kujitokeza.

 

error: Content is protected !!