Daily Archives: August 13, 2020

DK. SHEIN AMEKUTANA NA UONGOZI WA WIZARA YA HABARI, UTALII NA MAMBO YA KALE

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein amesema Serikali imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuliimarisha Shirika la Utangazaji Zanzibar ZBC jambo lililoiwezesha kuwa na wasikilizaji wengi hivi sasa na  kusikika hadi nje ya Tanzania

Dk. Shein amesema hayo leo Ikulu jijini Zanzibar, alipokutana na Uongozi wa Wizara ya Habari, Utalii na Mambo ya Kale wakati ilipowasilisha taarifa za utekelezaji wa Mpango kazi wa mwaka 2019/2020 na Mpango kazi wa mwaka 2020/2021.

Alisema vyombo vya Shirika hilo vya Redio na Televisheni hivi sasa vina wasikilizaji na watazamaji wengi hadi nje ya Tanzania, jambo ambalo hapo kabla halikuwepo.

Alisema kuna umuhimu kwa viongozi wa Shirika hilo kujikita katika kuwapatia mafunzo watendaji wake, ili waweze kwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia sambamba  na kujenga uwezo wa kuandaa programu bora zitakazovutia watazamaji wake.

Aidha, alisema serikali itaendeea na juhudi za kuliimarisha Shirika hilo ili liweze kupata mafanikio makubwa zaidi.

Rais Dk. Shein aliutaka uongozi wa Tume ya Utangazaji Zanzibar kuendelea kusimamia sheria na kanuni zilizopo katika uendeshaji wa vyombo vya habari nchini, ikiwemo Redio na Televisheni.

Kuelekea uchaguzi mkuu ujao, Dk. Shein aliwataka watendaji wa vyombo vya habari  kuzingatia wajibu walionao wa kuwakumbusha wananchi umuhimu wa kudumisha amani na utulivu nchini kupitia programu na makala mbali mbali.

Alisema habari zinapoandaliwa na kuandikwa vizuri zinaiweka nchi katika mazingira mazuri na kuutaka uongozi wa gazeti la Zanzibar kufanya kazi hiyo kwa umakini kupitia matumizii sahihi ya Kiswahili, sambamba na kusisitiza umuhimu wa kutafuta zaidi elimu.

 

Aliwapongeza Uongozi, watendaji na wafanyakazi wa Wizara hiyo kwa juhudi kubwa wanazofanya kuimarisha utendaji wao wa kazi pamoja na kuandaa na kuwasilisha vyema taarifa ya utekelezaji wa mpango kazi.

 

Mapema, Waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale, Mahamoud Thabit Kombo alisema katika kipindi cha miaka kumi ya uongozi wa Dk. Ali Mohamed Shein, Wizara hiyo imepata mafanikio makubwa katika sekta za habari, utalii pamoja na mambo ya kale.

 

Alisema katika kipindi hicho, Wizara kupitia Shirika la Magazeti ya serikali Zanzibar  mnamo mwaka 2016 lilianza kuchapisha gazeti la Zanzibar leo lenye rangi katika kiwanda cha Wakala wa Uchapaji Zanzibar, hatua iliyorahisisha usambazaji wa gazeti hilo katika maeneo mbali mbali ya Zanzibar, mijini na vijijini.

 

Alieleza kuwa Wizara imefanikiwa kuyafanyia matengenezo makubwa maeneo ya kihistoria ya Kwa  Bihole, Mwinyi Mkuu, Fukuchani , Mkamandume na Mvuleni kwa gharama  ya shilingi Bilioni 14, na hivyo kuongeza idadi ya wageni wanaotembelea maeneo hayo sambamba na kuongeza mapato.

 

Aidha,  alisema katika kipindi hicho Kamisheni ya Utalii iliendelea kuandaa na kudhamini matukio mbali mbali yaliofanyika nchini, kama vile Stone town marathon,Tamasha la chakula cha asili Makunduchi, Mbio za Baiskeli za Afrika Mashariki, Tamasha la Utalii la Pemba, Sauti za Busara, Tamasha la nchi za Jahazi pamoja na maonyesho ya Utalii Zanzibar na kusema matamasha hayo yamesaidia sana kupunguza msimu mdogo wa utalii pamoja na kuongeza  siku za ukaazi kwa wageni wanaotembelea nchini.

 

Waziri Kombo aliipongeza Serikali chini ya Uongzi wa Dk. Shein kwa hatua ilizozichukua katika kukabiliana na ugonjwa wa Covid-19.

 

Nae, Mshauri wa Waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale, Maalim Abdalla Mwinyi  alisema viongozi, watendaji na wafanyakazi wa Wizara hiyo wanajivunia utendaji bora wa Dk. Shein, jambo lilosababisha sekta zote ziliomo ndani ya Wizara hiyo kupiga hatua kubwa ya maendeleo.

 

Katika kikao hicho, Uongozi wa Wizara ya Habari, Utalii na Mambo ya Kale, ulimkabidhi zawadi maalum Rais Dk. Shein pamoja na Mama Mwanamwema ikiwa ni kumbu kumbu ya kipindi chake cha Uongozi.

 

 

error: Content is protected !!