Daily Archives: July 13, 2020

DK.SHEIN AMETOA MKONO WA POLE KWA FAMILIA YA MAREHEMU MZEE NYANYA

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, ametoa mkono wa pole kwa familia ya Marehemu Mzee Haji Nasibu Haji Nyanya aliyefariki dunia alfajiri ya kuamkia Jumamosi ya Julai 11, 2020 huko Jijini Dodoma. 

Rais Dk. Shein alifika nyumbani kwa marehemu haji Nasibu Nyanya mara tu baada ya kurejea Jijini Dodoma ambako alishiriki katika vikao mbali mbali vya Chama Cha Mapinduzi (CCM). 

Akiwa nyumbani kwa Marehemu Haji Nasibu Haji Nyanya huko Bububu, Rais Dk. Shein aliwapa mkono wa pole wanafamilia wote akiwemo mjane wa Marehemu Bi Zainab Nyanya na kuwataka kuwa na subira katika kipindi hichi kigumu cha msiba. 

Rais Dk. Shein akiwa amefuatana na Mama Mwanamwema Shein aliitaka familia hiyo kumuombea dua Marehemu Haji Nasibu Haji Nyanya ambaye alikuwa ni mwanasiasa mkongwe na mfanyabiashara wa muda mrefu. 

Katika salamu zake hizo za pole, Rais Dk. Shein alieleza jinsi alivyoguswa na kifo cha Mzee Nyanya ambacho kilitokea huko Jijini Dodoma na kueleza jinsi walivyokuwa pamoja na Marehemu kabla ya kumfika umauti. 

Nayo familia ya Mzee Nyanya ilitoa shukurani kwa Rais Dk. Shein kwa kushirikiana nao bega kwa bega katika msiba huo yeye pamoja na Mama Shein ikiwa ni pamoja na kwenda kuwapa mkono wa pole mara tu baada ya kurudi safari. 

 Marehemu Mzee Nyanya atakumbukwa katika harakati mbali mbali za kisiasa, kiuchumi na kijamii hapa nchini ambapo mnamo  Januari 8 mwaka huu 2020 Rais Dk. Shein alimtunuku Nishani ya Mapinduzi kwa Viongozi na Wananchi Wenye Sifa Maalum huko katika viwanja vya Ikulu Jijini Zanzibar. 

Marehemu ameacha mjane, mtoto mmoja na wajukuu wanne, MwenyeziMungu ailaze roho yake mahala pema peponi, Amin. 

MABALOZI I WAAHIDI KUSHIRIKIANA NA SERIKALI YA TANZANIA KATIKA SEKTA YA UCHUMI

Mabalozi wanaowakilisha Nchi zao Nchini wamesema wataendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania ili kuhakikisha inafanikisha malengo iliyojiwekea hasa katika Sekta ya Uchumi. 

Akizungumza kwa niaba ya Mabalozi saba wanaowakilisha Nchi za hapo Nchini mwenyeji wao ambae alifuata na ujumbe huo walipo tembelea Banda la Benki ya Nmb katika Maonyesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) Bwana Paul Koyi amesema Mabalozi hao wameamu kutembelea Taasisi hiyo ya Fedha kutokana na umuhimu wake katika kukuza Uchumi wa Nchini. 

Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Huduma za kifedha kwa Biashara za Kimataifa wa Benki ya Nmb Nd.Linda Teggisa amesema Nmb imekuwa na mchango mkubwa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Serikali ikiwamo Ujenzi wa reli ya kisasa  pamoja na Ujenzi wa Bwawa la kuzalisha Umeme la Mwalimu Nyerere lililopo Rufiji. 

Maonyesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) bado yanaendelea katika Uwanja wa MwlJulius Nyerere Barabara ya Kilwa Jijini Dar es salaam ya yanatarajiwa kuhitimisha Julai 13 Mwaka huu.