Monthly Archives: July 2020

DK.SHEIN AMETOA MKONO WA POLE KWA FAMILIA YA MAREHEMU MZEE NYANYA

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, ametoa mkono wa pole kwa familia ya Marehemu Mzee Haji Nasibu Haji Nyanya aliyefariki dunia alfajiri ya kuamkia Jumamosi ya Julai 11, 2020 huko Jijini Dodoma. 

Rais Dk. Shein alifika nyumbani kwa marehemu haji Nasibu Nyanya mara tu baada ya kurejea Jijini Dodoma ambako alishiriki katika vikao mbali mbali vya Chama Cha Mapinduzi (CCM). 

Akiwa nyumbani kwa Marehemu Haji Nasibu Haji Nyanya huko Bububu, Rais Dk. Shein aliwapa mkono wa pole wanafamilia wote akiwemo mjane wa Marehemu Bi Zainab Nyanya na kuwataka kuwa na subira katika kipindi hichi kigumu cha msiba. 

Rais Dk. Shein akiwa amefuatana na Mama Mwanamwema Shein aliitaka familia hiyo kumuombea dua Marehemu Haji Nasibu Haji Nyanya ambaye alikuwa ni mwanasiasa mkongwe na mfanyabiashara wa muda mrefu. 

Katika salamu zake hizo za pole, Rais Dk. Shein alieleza jinsi alivyoguswa na kifo cha Mzee Nyanya ambacho kilitokea huko Jijini Dodoma na kueleza jinsi walivyokuwa pamoja na Marehemu kabla ya kumfika umauti. 

Nayo familia ya Mzee Nyanya ilitoa shukurani kwa Rais Dk. Shein kwa kushirikiana nao bega kwa bega katika msiba huo yeye pamoja na Mama Shein ikiwa ni pamoja na kwenda kuwapa mkono wa pole mara tu baada ya kurudi safari. 

 Marehemu Mzee Nyanya atakumbukwa katika harakati mbali mbali za kisiasa, kiuchumi na kijamii hapa nchini ambapo mnamo  Januari 8 mwaka huu 2020 Rais Dk. Shein alimtunuku Nishani ya Mapinduzi kwa Viongozi na Wananchi Wenye Sifa Maalum huko katika viwanja vya Ikulu Jijini Zanzibar. 

Marehemu ameacha mjane, mtoto mmoja na wajukuu wanne, MwenyeziMungu ailaze roho yake mahala pema peponi, Amin. 

MABALOZI I WAAHIDI KUSHIRIKIANA NA SERIKALI YA TANZANIA KATIKA SEKTA YA UCHUMI

Mabalozi wanaowakilisha Nchi zao Nchini wamesema wataendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania ili kuhakikisha inafanikisha malengo iliyojiwekea hasa katika Sekta ya Uchumi. 

Akizungumza kwa niaba ya Mabalozi saba wanaowakilisha Nchi za hapo Nchini mwenyeji wao ambae alifuata na ujumbe huo walipo tembelea Banda la Benki ya Nmb katika Maonyesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) Bwana Paul Koyi amesema Mabalozi hao wameamu kutembelea Taasisi hiyo ya Fedha kutokana na umuhimu wake katika kukuza Uchumi wa Nchini. 

Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Huduma za kifedha kwa Biashara za Kimataifa wa Benki ya Nmb Nd.Linda Teggisa amesema Nmb imekuwa na mchango mkubwa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Serikali ikiwamo Ujenzi wa reli ya kisasa  pamoja na Ujenzi wa Bwawa la kuzalisha Umeme la Mwalimu Nyerere lililopo Rufiji. 

Maonyesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) bado yanaendelea katika Uwanja wa MwlJulius Nyerere Barabara ya Kilwa Jijini Dar es salaam ya yanatarajiwa kuhitimisha Julai 13 Mwaka huu. 

DK.MWINYI KUFUATA NYAYO ZA MAGUFULI KUPIGA KAZI

Mgombea wa Nafasi ya Urais wa Zanzibar kupitia CCM Dk. Hussein Mwinyi ameahidi kufuata Utendaji kazi wa Dk. Magufuli ili Zanzibar ipate Maendeleo zaidi.

Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa CCM  Mjini Dodoma Amesema katika kufikia hatua kubwa ya maendeleo hayo atapaswa kupiga vita Rushwa ili Zanzibar inufaike na Rasilimali zilizopo.

Hivyo amewataka Wazanzibari kumuamini kwa kumpa ridhaa ya kuongoza kwa manufaa ya Zanzibar.

Dk.Shein amewashukuru Viongozi waliomtangulia kwa kumpa msaada mkubwa katika utekelezaji wa kazi zake na kuwasihi wana CCM kumpa ushirikiano Dk.Mwinyi ili   kuinyanyua Zanzibar Kiuchumi.

 

 

IDADI YA WATALII YAENDELEA KUONGEZEKA KUWASILI ZANZIBAR

Jumla ya Watalii thamanini wamewasili katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Abeid Karume  na Ndege ya  Qatar air   wakitokea Nchi za Bara la Ulaya kwa ajili ya kutembelea maeneo ya kihistoria Nchini.

Idadi hiyo ni kubwa kwa Wageni wa Kitalii kuwasili Nchini tokea Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuruhusu Ngede hizo kuingia kutokana na kupungua kwa Maambukizi ya Maradhi ya Corona.

Mwenyekiti wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar Nd.Sabahi Seleh Ali amesema Kamisheni hiyo imejipanga kuhakikisha Wageni wanaoingia Nchini wanapimwa ili kuepuka Maambukizi ya Maradhi mbali mbali ikiwemo Corona.

Afisa Uhamiaji Muandamizi Nd.Bakari Mohamed na Afisa Dhamana Huduma za Afya Uwanja wa Ndege Nd.Nassor Hamad wamesema wamejipanga vizuri kuhakikisha Mgeni anaeingia Nchini yupo salama pamoja na Wafanyakazi.

Nao Wageni waliowasili na Ndege hiyo ya Qatar air wameipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuweka Mazingira mazuri ndani ya Viwanjwa hivyo na kuishauri Jamii kuzidi kuchukua tahadhari zilizotolewa na Wataalamu ili kujikinga na Maradhi hayo.

 

error: Content is protected !!