Daily Archives: June 15, 2020

CCM YATAFAKARI KIONGOZI ATAKAYEFAA KWA MIAKA MITANO IJAYO

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema wakati muda wa kuelekea katika uchaguzi Mkuu unakaribia Wana CCM na Wananchi wana fursa nzuri ya kutafakari Kiongozi  atakayefaa kuwaongoza katika kipindi kijacho cha Miaka Mitano.
Alisema Viongozi wanaofaa kushika hatamu ya kuwaongoza vyema ni wale wenye uwezo kamili wa kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM inayokwenda kisasa katika mazingira ya Karne ya sasa ya Sayansi na Teknolojia Ulimwenguni.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa Kauli hiyo akimuwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduziu Dr. Ali Mohamed Shein katika uzinduzi wa Tangi kubwa la Kuhifadhia Maji safi na salama pamoja na uzinduzi wa Ofisi ya Jimbo la Kikwajuni iliyofanyiwa matengenezo makubwa ikiwa ni umaliziaji wa Utekelzaji wa Ilani ya Uchaguzi ndani ya Jimbo hilo.
Alisema Wananchi wanapaswa kufanya tathmini ya kina itakayoweza kuwaibulia mchapakazi imara  atakayejitolea kusimamia kwa wakati wote masuala yao ya Maendeleo na Uchumi  katika maeneo yao.
Alibainisha kwamba kumchagua Kiongozi kabla ya kumfanyia uhakiki wa kina huleta hatari kwani matokeo yake ni majuto yasiyokuwa na suluhu na hata kama uchaguzi wenyewe ukiambatana na rushwa inayokuwa kaa la moto ndani ya Miaka Mitano ya yule aliyechaguliwa.

Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif aliwakumbusha Wanachama wenye nia ya kuchukuwa Fomu kwa ajili ya kuomba Uongozi ndani ya CCM wazingatie Sheria, Muongozo na Taratibu zilizowekwa.
Aliupongeza Uongozi wa Jimbo la Kikwajuni kwa kazi kubwa ya kuwaletea Maendeleo Wananchi wake wakiwemo wale wa Mitaa ya jirani kazi iliyoleta Mafanikio Makubwa na ya kupigiwa mfano ndani ya Utekelezaji wa Ilani ya Chama ikienda sambamba na utekelezaji wa Ahadi uliyotoa wakati wa Kampeni.
Wakiwasilisha Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2015 – 2020 Mwakilishi wa Jimbo la Kikwajuni Mh. Nassor Salum Jazira na Mbunge wa Jimbo hilo Mhandisi Hamad Yussuf Masauni wamesema CCM kwenye uchaguzi ujao haitapata shida kuwanadi Wagombea wake watakaopata fursa ya kuteuliwa kugombea Jimbo hilo.
Walisema hiyo inatokana na Utekelezaji mkubwa wa Ilani ya Uchaguzi  ndani ya Jimbo la Kikwajuni Wilaya ya Mjini ambayo imepindukia kwa asilimia 100%.
Mh. Nassor Jazira na Mhandisi Masauni  walieleza kwamba uimarishaji wa Sekta ya Maji uliosimamiwa na Uongozi wa Jimbo kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maji Zanzibar {ZAWA} umelea Ukombozi mkubwa kwa Wananchi  waliowengi ndani ya Jimbo hilo ambao sasa utabakia kuwa Historia kutokana na kuondoka kwa changamoto ya huduma ya Maji.
Mapema Katibu wa Chama cha Mapinduzi Jimbo la Kikwajuni Nd. Farid Abdullah Hamad alisema kwa Niaba ya Wanachama na Wananchi wa Jimbo hilo wanaishukuru Serikali Kuu kwa nguvu kubwa iliyochukuwa ya kuimarisha Miundombinu mingi ya Maendeleo ndani ya Jimbo hilo.
Nd. Farid alisema Wananchi wa Jimbo la Kikwajuni na maeneo jirani wana haki ya kujivunia kutokana na neema ya Maendeleo hayo ambayo wameiomba Serikali kupitia Taasisi yake kutoa upendeleo wa fursa za Ajira kwa ile Miradi ya Uwekezaji iliyoanzishwa katika Jimbo hilo.
Katika shughuli hiyo Balozi Seif Ali Iddi amekabidhi Kadi za C.C.M kwa Wanachama 31 Waliohama Vyama tofauti vya Upinzani na kuhamia Chama cha Mapinduzi.
Halkadhalika akakabidhi  mchango wa Computer na Printer Zake, Garil Moja ya Jimbo, Basi Moja na Seti za Jazi kwa Chuo cha kuwafundishia Vijana masuala mbali mbali ya Michezo na ushoni.

error: Content is protected !!