Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema Wahandisi wa Ujenzi Wazalendo kujenga heshima na Uaminifu katika kutekeleza Miradi wanayokabidhiwa ili kujijengea sifa na kuaminika zaidi.
Amesema kuna baadhi ya Wataalamu Wazalendo wasio waaminifu ambao huwadanganya Viongozi na Taasisi zilizowakabidhi miradi ya Ujenzi bila ya kujali muda waliokubaliana wa kukamilisha kazi yenyewe.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo alipofanya ziara fupi ya kukagua maendeleo ya mradi wa Ujenzi wa tangi kubwa la kuhifadhia maji safi na salama katika Kijiji cha Kitope Mbaleni ambao ulichelewa kukamilika katika muda uliopangwa ambapo alilazimika kumuagiza Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini “b” kuchukuwa hatua zinazostahiki dhidi ya Wahandisi wa Ujenzi wa Mradi huo.
Alisema Wahandisi Wazalendo ni vyema wakazingatia umuhimu na fursa wanazopewa na Serikali pamoja na Taasisi za Kijamii za kusimamia miradi ya Maendeleo na Kiuchumi kwa vile Taifa limeshaanza kuridhika na taalum zao badala ya ile tabia ya kuwakumbatia Wahandisi wa Kigeni
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimpongeza na kumshukuru Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini “b” kwa usimamizi mzuri wa mradi huo uliokuwa ukisuasua katika Utekelezaji wake.
Akitoa Taarifa ya Mradi huo Katibu Mtendaji wa Taasisi ya Tanzania Youth Icon inayosimamia Ujenzi huo kwa ufadhili wa Taasisi moja ya Umoja wa Mataifa Bwana Abdullah Suleiman alisema Jumla ya Shilingi Milioni 10,000,000 tayari zimeshalipwa katika Awamu ya pili ya Mradi huo.
Nd. Abdullah Suleiman alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba salio lililobaki litamalizwa mara tu pale Mradi huo muhimu kwa maisha ya Wananchi utakapokamilika na kukabidhiwa rasmi kwa Wahusika ambao ni Serikali.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini “b” Ndugu Rajab Ali Rajab alisema alilazimika kumpa agizo la kuripoti kwa Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kaskazini “b” Asubuhi ya Ijumaa ya tarehe17 Aprili Mwaka huu Mkurugenzi wa Kampuni ya Grative Tanzania Limited yenye Makao Makuu yake Dar es salaam kutoa maelezo ya kina kuhusiana na kuchelewa kumalizika kwa wakati Mradi huo.
Nd. Rajab alisema Makubaliano ya kukamilika kwa mradi huo kati ya Uongozi wa Serikali ya Wilaya hiyo na Uongozi wa Kampuni ya Grative Tanzania Limited yamefikiwa ambapo ifikapo tarehe 25 Juni mradi huo utakabidhiwa Rasmi.
Mapema Asubuhi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alizindua rasmi Kisima cha Maji safi na Salama kilichojengwa na Uongozi wa Jimbo la Mahonda kwa ufadhili wa Taasisi ya Misaada ya Hayrat Yardin kilichopo Magharibi ya Skuli ya Mahonda.
Kisima hicho kilichoanza kujengwa Mnamo tarehe 9 Disemba 2019 hadi Tarehe 7 Januari 2020 kwa kuhudumia zaidi ya Wananchi Mia tatu wanaokizunguuka kimegharimu Jumla ya Dola za kimarekani Elfu Nne sawa na Shilingi za Kitanzania zaidi ya Milioni Tisa.
Akizungumza na Wananchi wa Eneo hilo Balozi Seif ambae pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda aliwashukuru na kuwapongeza Viongozi na Watendaji wa Taasisi ya Misaada ya Hayrat Yarnid kwa kuguswa na changamoto iliyokuwa ikiwakabili Wananchi wa Mahonda ya ukosefu wa huduma hiyo muhimu.
Balozi Seif alifahamisha kwamba Maji ni huduma muhimu anayolazimika kiumbe kuipata katika Mazingira yake ya kawaida yoyote hasa Mwanaadamu ili kustawisha Uhai na Afya yake.