Waziri wa Habari Utalii na Mambo ya Kale Mh. Mahmoud Thabit Kombo amesema Uchumi wa Zanzibar ulitetereka kwa asilimia 30 kufuatia kuzuiliwa kuingia kwa Watalii kutokana na Maambukizi ya CORONA na kudumaza Sekta ya Utalii.
Akizungumza katika kipindi cha moja kwa moja cha Alasiri yetu hapa ZBC amefahamisha kuwa katika muda huo mapato yanayotokana na Fedha za Nje yalipungua kwa asilimia 80 na kuathiri Nyanja zote za Kiuchumi .
Amesema Uamuzi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wa kufungua Milango ya Utalii ikiwemo Anga na Bandari na kuwa tayari kupokea wageni kunalenga kuurejesha Utalii katika kiwango chake na kwamba Serikali imechukua Hatua zote muhimu za kudhibiti Maambukizi mapya ya CORONA katika maeneo yote .
Mhe. Mahmoud amesema katika muda huo imegundulika kuwa upo umuhimu Mkubwa wa kuutangaza Utalii wa ndani kwani kutegemea wageni pekee kutoka mataifa ya Ulaya kunaweza kukaathiri Sekta hiyo pale Dunia inapopatwa na Majanga .
Amesisitiza kuwa Serikali imedhamiria kurejesha kiwango cha Idadi ya Watalii wanaoingia Nchini angalau kwa asilimia 30 kila mwezi ili kufikia Watalii 548 ,000 waloingia Nchini mwaka uliopita kabla ya kuripuka kwa Maambukizi ya CORONA.