Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema Wananchi Wazalendo wana haki ya kuwekeza miradi mikubwa ya Kiuchumi na Maendeleo ndani ya Taifa jambo linalotoa fursa za Ajira kwa kundi kubwa la Vijana na uhakika wa Soko la bidhaa zinazozalishwa.
Amesema zipo lawama za muda mrefu zinazotolewa na Wananchi pamoja na Wateja kuhusu baadhi ya bidhaa zinazotokea Nje ya Nchi kuwa zinapowafika kwa watumiaji zinakuwa zimeshapitwa na wakati na kuhatarisha Afya kwa Watumiaji.
Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati akipokea mchango wa vifaa mbali mbali vya mapambano dhidi ya Virusi vya Corona uliotolewa na Kampuni ya VIGO chini ya Kiongozi wake ambae pia ni Mbunge wa Jimbo la Mpendae Mh. Salum Turky vifaa ambavyo vimetengenezwa hapa hapa Nchini.
Alieleza inapendeza kuona kamba vifaa vinavyotengezwa kwa lengo la mapambano dhidi ya kupiga vita kuenea kwa Virusi vya Corona kwa sasa idadi kubwa inatengenezwa na Viwanda pamoja na Taasisi za Kizalendo hapa Nchini jambo linaloleta faraja kutokana na Wazalendo tofauti kuchangamkia fursa hiyo.
Balozi Seif Ali Iddi alitanabahisha kwamba Virusi vya Corona bado vipo Nchini licha ya kupunguwa kwa wagonjwa wa Maradhi hayo na kufikia Wagonjwa 10 hadi sasa ambapo juhudi zitapaswa kuchukuliwa ili Wananchi waendelee kuzingatia masharti yaliyowekwa na Wataalamu katika kukabiliana na janga hilo.
Alisisitiza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar bado inazingatia mambo ya kufanya kabla ya kuanza kwa harakati zake za kawaida ikiwemo masuala ya Mawasiliano ya usafiri unaogusa moja kwa moja Sekta ya Utalii inayojumuisha maingiliano wa safari za Mataifa mbali mbali Duniani.
Balozi Seif alisema uwepo wa Vifaa vya uhakika vya kupimia katika kufuatilia mienendo ya Virusi vya Corona ni muhimu ikiwa ni dawa kubwa ya kudhibiti kurejea tena kuenea kwake hapa Nchini.
Mapema Kiongozi wa Kampuni ya Vigo ambae pia ni Mbunge wa Jimbo la Mpendae Mh. Salum Turky alisema maradhi yanayosababishwa na Virusi vya Corona yameharibu kwa kiasi kikubwa Uchumi unaoliliwa na Kila Mwanaadamu hivi sasa.
Mh. Turky alisema kupungua kuenea kwa Virusi vya Corona ni hatua nzuri inayotokana na jitihada kubwa iliyochukuliwa na Serikali Kuu ambayo itatoa fursa kurejea kuimarika tena kwa uchumi katika Mataifa yote yaliyoathiriwa na mripuko wa Virusi hivyo.
Vifaa vilivyotolewa na Kampuni ya Vigo vina thamani ya Shilingi za Kitanzania Milioni 70,000,000/- ikiwa ni kukamilisha Ahadi ya Kampuni hiyo ya Mchango wa gharama ya vifaa vyenye thamani ya Shilingi Milioni 100,000,000/- ni pamoja na Maski 50,000, mashuka na foronya zake 100 na Nguo za kuhudumia Wagonjwa Mia 500.