Tume ya Haki za Binaadamu Tanzania ina wajibu wa kufanya kazi kwa karibu zaidi na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa lengo la kuwatumikia Wananchi wa pande zote mbili za Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kufanya hivyo kutaisaidia Serikali kutatua changamoto zinazowakabili Wananchi hususani Wanawake, Watoto na wenye mahitaji maalum.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo wakati wa mazugumzo yake na Uongozi wa juu wa Tume ya haki za binaadamu Tanzania ukiongozwa na Mwenyekiti wake Jaji Mstaafu Mathew Pauwa Mhina ulipofika Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar kujitambulisha Rasmi.
Balozi Seif alisema Tume ya haki za binaadamu ina kazi kubwa katika kutekeleza Majukumu yake kwa upande wa Zanzibar kutokana na Migogoro na Changamoto nyingi zinazowakabili Wananchi hali inayosababisha mitafaruki na mifarakano miongoni mwa Jamii yenyewe.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliueleza Uongozi huo wa Tume ya Haki za Binaadamu kwamba yapo matatizo mengi yanayowakabili Wananchi hasa Wanawake ya kupewa ovyo Talaka na matokeo yake kutelekezwa kunakokwenda sambamba na kuachiliwa Watoto bila ya Huduma.
Katika kuimarisha Utendaji wa Tume ya haki za Binaadamu Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliuomba Uongozi huo kuandaa mpango Maalum wa kujenga majengo ya kudumu ya Ofisi zake Visiwani Zanzibar wakati Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ipo tayari kutoa maeneo ya Ujenzi huo wakati wowote pale itapohitajika kutekelezwa Mpango huo.
Mapema Mwenyekiti wa Tume ya haki za Binaadamu Tanzania Jaji Mstaafu Mathew Pauwa Mhina alisema Taasisi hiyo ni Chombo cha Umma kilichoundwa kusimamia upatikanaji wa haki za binaadamu ili kusimamia utawala bora hapa Nchini.
Hata hivyo, Jaji Mathew alisema watendaji wa Tume hiyo ni binaadamu wanaoweza kuteleza katika utekelezaji wa Majukumu yao . Hivyo viongozi Wakuu wanapaswa kushauri pale watendaji hao wanapoteleza katika maeneo yao ya kazi.
Mwenyekiti huyo wa Tume ya haki za Binaadamu Tanzania aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kazi kubwa na ngumu inayofanya ya kuhudumia Wananchi jambo ambalo Uongozi wa Tume hiyo unaliunga Mkono.
Wajumbe wa Tume ya Haki za Binaadamu Tanzania waliteuliwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli mnamo tarehe 19 Septemba Mwaka 2019.