Daily Archives: April 3, 2020

MAMIA YA WANANCHI WAMESHIRIKI KATIKA MAZISHI YA MWANDISHI MWANDAMIZI WA TBC MARIN HASSAN MARIN

Mamia ya Wananchi  wameshiriki katika Mazishi ya Mwandishi Mwandamizi wa TBC Marin Hassan Marin katika Makaburi ya Mwanakwerekwe yakiongozwa na Waziri wa Habari Utalii na Mambo ya Kale Mhe. Mahamoud Thabit Kombo na Waziri wa Harisson Mwakiembe.

Maiti ilisaliwa katika Msikiti wa Ijumaa Kibweni na kuhudhuriwa na Mamia  ya Wananchi.

Katika Makaburi ya Mwanakwerekwe baadhi  ya viongozi  na  watu waliowahi kufanya  nae kazi wakitoa Wasfu wa Marehemu Marin wamesifu kazi, uweledi na kuwa  mtu aliyejali kazi yake na kuinua Waandishi wa Chipukizi.

Marehemu Marin alizaliwa mwaka 1972 katika mtaa wa Kikwajuni na kupata elimu yake ya Msingi na Sekondari hapa Zanzibar, Marehemu alipitia kada ya Ualimu kabla ya kujiunga katika tasnia ya  Habari hadi mauti yanamkuta.

Mwenyekiti wa Bodi ya ZBC kwa niaba ya Wafanyakazi anatoa Mkono wa Rambi rambi kwa Wafiwa na Wafanyakazi wa TBC kwa msiba huo mzito.

MH. HAROUN ALI AMEWATAKA MASHEHA KUWAHIMIZA WANANCHI WAO KUEPUKA MIKUSANYIKO ISIYOKUWA YA LAZIMA

Mwakilishi wa Jimbo la Makunduchi  Mh.Haroun Ali Suleiman amewataka Masheha wa Wilaya hiyo na Makatibu wa Vyama vya Siasa kuhimiza Wananchi wao kujinusuru na Mikusanyiko isiyokuwa ya lazima ili kupunguza ueneaji wa Maradhi ya CORONA katika sehemu zao.

Ameyasema hayo wakati akikabidhi Vifaa vya kujikinga na CORONA huko katika Afisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kusini Unguja.

Amesema endapo Tahadhari ikichukuliwa mapema uenezaji wa Maradhi hayo unaweza ukapungua,siku hadi siku.

Ameshauri vifaa hivyo vitumike kwa matumizi yaliyokusudiwa, pamoja na kuwasihi Wafanya Biashara kuwa waangalifu wanapo fanya Biashara zao, ili kuweza kupunguza tatizo hilo lisienee kwa haraka.

Mapema Mkuu wa Wilaya ya Kusini  Nd.Idrissa Kitwana Mustafa amesema lengo hasa la msaada huo ni kutumia kwa maslah ya wananchi wa Wilaya hiyo bila ya kujali itikadi zao za Kisiasa.

Aidha ametoa Tahadhari kwa Masheha kuzidisha  uangalifu  kwa Maradhi ya CORONA lakini pia kufata maelekezo yote yaliyotolewa na  Serikali na badala yake  kuondoa mzaha juu ya Maradhi hayo hatari kwa Jamii nzima .

Akitoa shukrani Mwenyekiti wa Jimbo  hilo Nd. Nassor Rajab Mwalim amewashukuru Viongozi kwa kushirikiana pamoja  katika  kupunguza  janga la Maradhi ya CORONA  na wameahidi vifaa hivyo vilivyotolewa kwa msaada na Mbunge na Mwakilishi  kuvitumia kwa uangalifu.

error: Content is protected !!