Daily Archives: March 20, 2020

JAJI MKUU WA ZANZIBAR AMEMUAPISHA JAJI MWAMPASHI NA MAKADHI WATATU WA MAHAKAMA ZA KADHI ZA WILAYA.

Jaji Mkuu wa Zanzibar Mh. Omar Othman Makungu amemuapisha Jaji Abraham Mwampashi na Makadhi watatu wa Mahakama za Kadhi za Wilaya.

Jaji Mwampashi ameapishwa kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama na Makadhi wa Wilaya ni Sheikh Omar Sheikh Khamis, Ali Sharif Maalim na Masoud Saleh Abdulla.

Akizungumza katika hafla hiyo Jaji Makungu  amewataka Makadhi  hao kufanya kazi kwa uadilifu   na  kuzingatia Sheria ili waweze kufanya  kazi  zao  kwa ufanisi  katika Majukumu  yao.

Akizungumzia uchache  wa  Mahakimu  Kisiwani  Pemba  amesema  Mahakama  ina  mpango  wa  kuweka hakimu  mkaazi  ili  kuondoa  jukumu  la  kupeleka  Mahakimu  mara  kwa  mara  Kisiwani  humo .

Jaji Abraham Mwampashi akizungumza kwa niaba ya Makadhi  walioapishwa ameahidi  kufanya kazi kulingana na miongozo na Sheria za Mahakama katika utekelezaji wa Majukumu yao.

Hatua hiyo imekuja kufuatia vifo vya  Marehem Sheikh Shamim Khamis na Marehemu Mkusa Isaack Sepetu aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama.

OFISI YA MUFTI MKUU WA ZANZIBAR IMEWATAKA MAIMAMU KUFUPISHA SALA NA DUA KATIKA NYUMBA ZA IBADA

Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar imeziongeza Tahadhari kwa Waumini wa Dini ya Kiislamu na kuwataka Maimamu kufupisha Sala na Dua katika nyumba za ibada ili kuwa ni Tahadhari ya Ugonjwa wa Korona.

Akitoa Taarifa kwa Vyombo vya Habari katika wa Mufti Zanzibar Sheikh Khalid Ali Mfaume amesema ni vyema kwa  Maimamu  kufupisha  kusoma Sura kubwa wakati wa Sala ili kupunguza muda katika Sala za jamaa ikiwemo Sala ya Ijumaa.

Sheikh Khalid katika taarifa yake  ameyataja mambo kadhaa  ambayo yanapaswa kuchukuliwa ikiwemo kuzuiya semina za Kidini, Mihadhara , Sherehe za Harusi na pamoja na  Msiba kuhudhuriwa na Watu wachache.

Amesema kwa wale ambao wanasafirisha Mahujaji kwa  kufanya ibada ya hija  ameshauri watafute njia itakayofaa ambayo haito leta Mikusanyiko wakati wa kutoa Mafunzo.

Aidha amewataka Wazazi kutowaacha Watoto wao katika kipindi hiki kwa kuwacha kudhurura ovyo na kutumia fursa ya kuwasomesha wenyewe Nyumbani kwao.

Kuhusu Wafanyabiashara Shehe Khalid amekumbusha ubaya wa kupandisha bei bidhaa katika wakati huu wa janga la Ugonjwa ulioingia katika Nchi.

error: Content is protected !!