Daily Archives: March 11, 2020

WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI KUENDELEA KUSIMAMIA AMANI NA USALAMA WA WANANCHI NA MALI ZAO

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameeleza haja kwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuendelea  kusimamia amani na usalama wa wananchi pamoja na mali zao wakati wote.

Hayo aliyasema leo wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi George Boniface Simbachawene Ikulu Jijini Zanzibar alipofika kwa ajili ya kujitambulisha kufuatia kuteuliwa kushika wadhifa huo hivi karibuni.

Katika maelezo yake Rais Dk. Shein alimueleza Waziri huyo kuwa ipo haja kwa Wizarahiyo ya kuendeleza kasi katika kushughulikia suala zima la kulinda amani na usalama kwa wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Rais Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Vikosi vyake vyote vya ulinzi ili kuhakikisha amani, usalama na utulivu unaendelea kudumu hapa nchini.

Alieleza kuwa Serikali ya Mapnduzi ya Zanzibar kwa upande wake imekuwa ikiendelea kuhakikisha amani, usalama na utulivu unakuwepo kwa wananchi pamoja na mali zao na ndio maana imeanzisha mradi wa Mji Salama katika maeneo yote ya Jiji la Zanzibar ukiwemo Mji Mkongwe ambao umepata umaarufu sana kwa utalii.

Rais Dk. Shein  alieleza kuwa Mradi huo wa Mji Salama mbali ya kuhakikisha usalama kwa wananchi wa Zanzibar pia una lengo la kuhakikisha wageni wote wakiwemo watalii wanaotembelea Jiji la Zanzibar wako salama.

Hivyo, Rais Dk. Shein alisisitiza haja kwa vikosi vya ulinzi vya Jeshi la Polisi kuhakikisha linaendelea na utaratibu wake wa kuwalinda wananchi pamoja na mali zao kwa maeneo ya mjini na mashamba hasa zile sehemu za ukanda wa Utalii.

Aidha, Rais Dk. Shein ameeleza juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Jeshi hilo la Polisi katika kusimamia ulinzi na usalama wa wananchi na mali zao pamoja na kusifu juhudi za Jeshi la Uhamiaji kwa kuendelea kudhibiti na kupambana na wahamiaji haramu hapa Zanzibar.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein ameendelea kulisisitiza Jeshi la Polisi kuendelea kusimamia vyema usalama wa barabarani kwa lengo la kuepuka ajali zisizo za lazima pamoja na kuhakikisha sheria na kanuni elekezi za barabarani zinafuatwa.

Aliongeza kuwa kutokana na juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar za kuimarisha  miundombinu ya barabara hatua hiyo imepelekea madereva wengi kuvunja sheria kwa kwenda mwendo wa kasi na hatimae kuhatarisha maisha kwa wananchi.

Dk. Shein pia, alitumia fursa hiyo kumpongeza Waziri Simbachawene kwa kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli kushika wadhifa huo na kumuahidi kuwa yeye pamoja na Serikali anayoiongoza wataendelea kumsaidia na kuipa mashirikiano Wizara anayoiongoza hasa ikizingatiwa kuwa ni  Wizara ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili iendelee kufanya kazi zake vyema.

Nae Waziri George Boniface Simbachawene, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi alimuhakikishia Rais Dk. Shein kuwa atahakikisha amani na  usalama vyote kwa pamoja vinaendelea kudumishwa hapa nchini ili Tanzania iendelee kusifika ndani na nje ya Bara la Afrika.

Waziri Simbachawene alimueleza Rais Dk. Shein kuwa ni jukumu la Wizara hiyo la kuhakikisha usalama na amani kwa wananchi pamoja na mali zao unakuwepo wakati wote na kusisitiza kuwa kwa mashirikiano ya pamoja ya vikosi vya ulinzi na usalama jambo hilo litaendelea kutekelezwa.

Waziri huyo alitoa pongezi zake kwa mashirikiano makubwa kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoendelea kuyapata Wizara anayoiongoza pamoja na vikosi vyote vya ulinzi na usalama vilivyomo katika Wizara hiyo.

Aidha, Waziri Simbachawene alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein kwa kupatiwa eneo la kujenga Ofisi za Idara ya Uhamiaji hapa Zanzibar.

Pamoja na hayo, Waziri huyo alimuhakikishia Rais Dk. Shein kuwa juhudi za makusudi zitaendelea kuchukuliwa na Jeshi la Polisi katika kuhakikisha sheria na kanuni zinafuatwa hasa zile za usalama barabarani.

DK.SHEIN AMEITAKA TAASISI YA MWANAHARAKATI YA BIBI SITI BINT SAAD KUZIDI KUMTANGAZA

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameitaka Taasisi ya Mwanaharakati  Bibi Siti Bint Saad kumtangaza Mwanaharakati huyo pamoja na kuzitangaza kazi zake ili zifahamikeNdani na Nje ya Zanzibar.

 Hayo ameyasema Leo, Ikulu Jijini Zanzibar alipokutana na Uongozi wa Taasisi ya Mwanaharakati Bibi Siti Bint Saad ukiongozwa na Mwenyekiti wa Taasisi hiyo Bi Nasra Mohamed Hilal pamoja naMshauri wa Taasisi hiyo Bwana Abdalla Mwinyi Khamis.

Katika maelezo yake, Rais Dk. Shein aliueleza Uongozi huo kuwa Mwanaharakati Bibi Siti Bint Saad amefanya mambo mengi ambayo yanapaswa Jamii iyafahamu na hilo litafanikiwa iwapo Taasisi hiyo itachukua Jukumu lake hilo na kulifanyia kazi ipasavyo.

Rais Dk. Shein alieleza kuwa mengi aliyoyafanya Bibi Siti Bint Saad hayaonekani hivi sasa na mengine yamebakia kwenye Picha za kubuni pamoja na kuandikwa vitabuni tu, hivyo, ni jambo jema Taasisi hiyo ikafanya juhudi za makusudi katika kuhakikisha Mwanaharakati huyo anatambulikana Ndani na Nje ya Zanzibar.

Aliongeza kuwa Taasisi hiyo ni vyema ikachukua juhudi za makusudi katika kuhakikisha kazi Pamoja na Shughuli za Mwanaharakati huyo alizozifanya katika uhai wake zinajulikana na jamii iliyopo pamoja na vizazi vijavyo.

Aidha, Rais Dk. Shein ambaye pia, ni Mshauri mMkuu wa Taasisi hiyo alisema kuwa katika suala zima la kumtangaza Bibi Siti Binti Saad ni vyema zikatumika kazi zake alizozifanya ikiwa ni pamoja na nyimbo zake ambazo zilikuwa na sifa, mvuto, ghaiba na elimu kubwa kwa Jamii wakati huo na huu uliopo.

Rais Dk. Shein alieleza kuwa Nyimbo za Bibi Siti Binti Saad zimeweza kuelemisha, kuburudisha, kuadabisha na kufunza Jamii kwani ziligusa katika mambo ya kisiasa, Kiuchumi na Kijamii.

Rais Dk. Shein alieleza kuwa iwapo kazi za Bibi Siti Binti Saad zitasambazwa zikiwemo Cd za nyimbo zake zitapataSoko kubwa sana katika Ukanda wa Pwani ya Afrika Mashariki, Kaskazini na Kusini mwa Afrika pamoja na nje ya Bara hilo.

Alisisitiza kuwa hatua hiyo ni nzuri ambayo mbali ya kumuenzi Mwanaharakati huyo pia, itasaidia kuzitangaza kazi zake sambamba na kuongeza mtaji kwa Taasisi hiyo.

Alieleza kuwa Soko la nyimbo za Bibi Siti Bint Saad litapatikana kutokana na Historia ya Msanii huyo ambaye alikuwa ni Mwanamke Jasiri na aliyekuwa na kipaji cha Sanaa na Sauti nzuri iliyowavutia watu wengi ambayo bado watu wanatamani kuisikia na kumfahamu vilivyo Mwanaharakati huyo.

Pamoja na hayo, Rais Dk. Shein aliipongeza Taasisi hiyo kwa kuendelea na harakati za kuzitunza kazi za Mwanaharakati huyo huku akisisitiza haja ya kuongeza kasi ya kumtangaza Msanii huyo ambaye alipata umaarufu mkubwa ndani na Nje ya Zanzibar.

Pia, Rais Dk. Shein alisisitiza haja kwa Taasisi hiyo kuandaa Mpango maalum wa muda mrefu, wakati na muda mfupi katika kumtangaza Mwanaharakati huyo ili Historia yake iendelee kutambulika.

Rais Dk. Shein aliutaka Uongozi wa Taasisi hiyo kutovunjika moyo kwa yale yote ambayo yalibuniwa na bado hayajafikia malengo yaliokusudiwa na kueleza kuwa waendelee na subira huku wakipanga mipango na mikakati ya kuyafanikisha.

Nae Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwanaharakati Bibi Siti Bint Saad, Bi Nasra Mohamed Hilal alimueleza Rais Dk. Shein mafanikio yaliopatikana katika Taasisi hiyo pamoja na malengo yaliyowekwa.

Katika maelezo yake Mwenyekiti huyo alimueleza Rais Dk. Shein kuwa Taasisi hiyo imeweza kufanya mambo mengi ikiwa ni pamoja na kufanya Tafiti mbali mbali zinazohusiana na Mwanaharakati Bibi Siti Binti Saad pamoja na Makongamano ya Kiswahili, kutoa Mafunzo ya Uchoraji, kutoa Vyeti vya Uwanachama na mengineyo.

Aidha, Mwenyekiti huyo alieleza kufarajika kwake kwa kuwa na Vijana waliojiunga katika Taasisi hiyo wenye fani mbali mbali ambao wamekuwa wakitoa msaada mkubwa kwa kuiendeleza na kuiimarisha taasisi hiyo.

Pia, Mwenyekiti huyo alieleza miradi mbali mbali ambayo imeandaliwa na Taasisi hiyo yenye lengo la kuongeza kipato kwa Taasisi pamoja na kuitangaza Taasisi hiyo kwa kuanzisha tovuti yake, kuanzisha Vijarida na mambo mengineyo.

Pia, uongozi huo ulieleza azma ya kuanzisha Redio ya ‘Siti Redio Fm” kwa ajili ya kuzitangaza kazi za Taasisi hiyo sambamba na hivi sasa kumiliki Televisheni Mtandao.

Bibi Siti Binti Saad alizaliwa katika Kijiji cha Fumba Mnamo Mwaka 1870 na kuishi miaka 80 ambayo iligawika kwa Miaka 40 ya kwanza ya uhai wake akiwa kwa Jina la Mtumwa Binti Saad wakati huo akiwa mfinyanzi wa vyungu vya kupikia na kazi nyengine za Usanii wa Mikono.

Miaka 40 ya Mwisho wa maisha yake kuanzia mwaka 1910 hadi 1950 alipofariki alikuwa Msanii na muimbaji kwa hivyo alikuwa maarufu kwa Jina la Bibi Siti Bint Saad ambapo Nyimbo zake zilipata umaarufu mkubwa kwa kua alikuwa muimbaji wa kwanza wa kike kuimba Nyimbo za Taarab tena kwa Lugha ya Kiswahili.

Taasisi ya Mwanaharakati Bibi Siti Bint Saad ilizinduliwa Rasmi Januari 7 Mwaka 2014 na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein.

Wakati huo huo, Taasisi hiyo ilimkabidhi Rais Dk. Shein ambaye pia, ni Mshauri Mkuu wa Taasisi hiyo kadi yake ya Uwanachama,Ripoti ya Miaka mitano, kazi inazozifanya Taasisi hiyo pamoja na Picha yenye maelezo kuhusu kuibuliwa kwa muimbaji Siti Bint Saad na Bwana Muhsin Bin Ali.

MVUA ZINAZOENDELEA KUNYESHA ZASABISHA UGUMU KATIKA UJENZI WA JAA KATIKA MAENEO YA MPENDAE

Msimamizi Mshauri wa Ujenzi wa Mradi wa Jaa linalojengwa na Kampuni ya Kichina  Maeneo ya  Mpendae kwa Bint Hamrani Nd.David Masaoe amesema kufuatia Mvua iliyonyesha  Majira ya Asubuhi imewaletea ugumu wa Kazi zao kutokana na Mtaro waliouchimba kujaa Maji.

Akizungumza na ZBC  Msimamizi huyo amesema harakati za Uchimbaji walizokuwa wameshaanza  haziwezi kuendelea  na kupelekea zoezi la kutoa Maji kwa njia ya Mpira  na ndipo waendeleee na kazi hiyo ya uchimbaji.

Amesema Mradi huo unatarajiwa kukamilika kama ulivyopangwa na kuwataka Wananchi kulitumia Dampo hilo la kuhifadhia Taka ngumu kwa ajili ya kutunza Mazingira na kuacha kuzagaa Taka ovyo  na  Taka hizo kupelekwa Jaa kubwa Kibele.

Nao Wananchi wa Tomondo wameiomba Serikali kuwatengenezea Barabara yao ili kuondosha usumbufu wakati wa kipindi cha Mvua zinaponyesha.

Akizungumza na ZBC   iliofika katika Eneo  hilo Mmoja wa Wakaazi wa Tomondo Abdul Aziz Khamis amesema ni vyema kwa Wananchi kuchukua Tahadhari za uwangalizi wa Watoto katika Mvua hizi zinazoendelea kunyesha ili zisileta athari kwao  na Taifa kwa Ujumla

CORONA YASABABISHA VIKAO VYA ANA KWA ANA KWA MAWAZIRI WA JUMUIYA YA SADC KUSITISHWA

Mawaziri wa Afya Nchi Wanachama  wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wamekutana kwa dharura Jijini Dar es salaam kushauriana kusitisha Vikao vya ana kwa ana vya Jumuiya hiyo hadi mripuko wa Ugonjwa wa Corona utakapodhibitiwa.

Hatua hiyo imefikiwa wakati kunatarajiwa kufanyika kwa Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa SADC Jijini Dar es salaam kuanzia March 16 hadi 18 ambapo utawashirikisha Mawaziri wote kutoka Nchi 16 Wanachama wa  SADC.

Akitoa Maadhimio ya Kikao hicho Mwenyekiti   Mawaziri wa Afya wa Jumuiya hiyo ambae pia ni Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Mh. Ummy Mwalimu amesema ushauri huo wanautowa kwa Baraza la Mawaziri ambapo kwa Mikutano yote ya SADC  itakayofanyika Watu watatakiwa kukutana hivyo wameshauri kuisimamisha kwa muda na kutumika njia nyengine ikiwemo

Pia katika hatua nyengine Waziri Ummy amesisitiza Kikao hicho kimeangalia hali ya utayari na Maandalizi kwa kila Nchi Wanachama na kukubaliana kwa pamoja hata kama hakuna Mgonjwa katika Nchi za SADC, kuondoka kwenye Mfumo wa hali ya utayari na kuwenda katika hali ya kukabiliana na Ugonjwa huo ambapo kwa upande wa Serikali ya Tanzania inaendelea kuweka Vituo kwa washukiwa wa Virusi vya Corona.

Nae Naibu Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dk. Damas Ndumbaro ambae anamuakilisha Waziri Kabudi amesema Wanafunzi wa Tanzania 504 waliopo China wote wapo salama na kila siku wanapokea Taarifa zao.

Pia Katibu Mkuu Sekretariet ya SADC Dk. Sergomena Tax amesema wameshauri Nchi Wanachama kuwa na Mfumo bora na madhubuti wa Afya .

Mpaka sasa Nchi 101 Duniani tayari zimeshaathirika na Corona ambapo kwa upande wa  Nchi za  SADC  mpaka sasa Afrika ya Kusini pekee ndio iliyoathirika na Ugonjwa huo.

Wakati huo huo Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki   Balozi  Kanal Wilbert Ibuge amesema Maandalizi ya Kikao cha Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika SADC kilichapangwa kufanyika kuanzia Machi 16 na 17 kitafanyika kwa njia ya njia ya Video ambapo Mawaziri hao watashiriki wakiwa katika Nchi zao.

 

error: Content is protected !!