Daily Archives: March 3, 2020

UONGOZI WA WIZARA YA KATIBA NA SHERIA WAMETAKIWA KUENDELEZA UADILIFU NA USIMAMIZI MZURI WA KAZI ZAO

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameutaka Uongozi wa Wizara ya Katiba na Sheria kuendeleza uadilifu na usimamizi mzuri wa kazi zao hasa kwa vile Wizara hiyo ndio inayosimamia Sheria.

Hayo ameyasema leo, Ikulu Jijini Zanzibar alipokutana na Uongozi wa Wizara ya Katiba na Sheria wakati ilipowasilisha utekelezaji wa mpango kazi  kwa kipindi cha Julai hadi Disemba kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020.

Rais Dk. Shein alisema kuwa usimamizi mzuri wa kazi sambamba na uadilifu kwa Viongozi hao ni njia pekee ya kuimarisha utendaji wa kazi ikiwa ni pamoja na kutoa haki kwa Wananchi hasa ikizingatiwa kwamba Wizara hiyo inaigusa moja kwa moja Jamii.

Rais Dk. Shein aliupongeza Uongozi wa Wizara hiyo pamoja na Watendaji wote wa Kike na wa Kiume kwa kutekeleza vyema majukumu yao ya kazi na kuwasisitiza kuendeleza juhudi zao hizo ili Zanzibar izidi kuimarisha katika Sekta ya Sheria.

Alisema kuwa Wizara hiyo imeundwa kutokana na umuhimu wake mkubwa licha ya kujitokeza kwa baadhi ya changamoto ndogo ndogo pale ilipoanzishwa ikiwemo uhaba wa nyenzo lakini hata hivyo hatua kubwa imefikiwa na kuweza kufanya kazi zake vizuri.

Pamoja na hayo, Rais Dk. Shein alisema kuwa ili Watumishi wa Umma katika Kada zote waendelee kupata Maslahi mazuri Serikali kwa upande wake itafanya jitihada zake pale tu mapato yatakapoongezeka basi Watumishi wa Umma nao watatizamwa Kimaslahi.

Rais Dk. Shein alieleza azma ya kuanzishwa kwa Skuli ya Sheria hali ambayo itasaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha Sekta ya Sheria hapa Nchini.

Akieleza hatua zinazoendelea za kuanzishwa kwa Skuli ya Sheria, Rais Dk. Shein alisema haja ya kuwekwa mipango maalum kati ya Tume ya Mipango ya Serikali na Ofisi ya Utumishi wa Umma kwa ajili ya Mipango ya hapo baadae.

Alieleza kuwa ni wajibu kwa Uongozi wa Wizara hiyo kuzigeuza changamoto kuwa mafanikio, na ukaendelea kufanya Kazi zake kwa ufanisi zaidi hasa ikizingatiwa kuwa kwa upande wa Sheria Zanzibari iko vizuri na imekuwa ikijipatia sifa.

Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee alisema kuwa Taarifa hiyo imetayarishwa vizuri na kuwasilishwa vyema huku akisisitiza kuwa Wizara hiyo ni kioo hivyo ni vyema wakaendelea kutekeleza Kazi zao kwa Ufanisi huku Uongozi huo ukihakikisha kwamba kila mwenye haki yake anaipata.

 

Nae Waziri wa Wizara ya Katiba na Sheria Zanzibar, Khamis Juma Mwalim alieleza kuwa utekelezaji wa Wizara ya Katiba na Sheria umezingatia ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ambayo imezungumzia Sekta ya Sheria katika Ibara ya 121 ya ilani ya CCM  ya Mwaka 2015-2020.

Aidha, mipango mikuu ya Kitaifa ikiwemo Mkuza na Dira ya maendeleo 2020 ambapo vyote kwa pamoja vinazingatia na kusisitiza suala la upatikanaji wa haki, kudumisha amani, utulivu na usalama wa maisha ya Wananchi na mali zao.

Alisema kuwa Wizara imeendelea kuratibu na kusimamia utekelezaji wa miongozo mbali mbali ikiwemo Sera, Sheria na kanuni ambapo kwa Kipindi hiki imekamilisha matayarisho ya kuanzishwa kwa Jukwaa la pamoja la Wadau wa Sekta ya Sheria (JSF) na kuandaa Rasimu ya Sera ya Skuli ya Sheria na kuitafsiri kwa Lugha ya Kiswahili.

Aidha, alisema kuwa Wizara katika kuhakikisha kwamba azma ya Serikali ya kuona kwamba Wananchi wananufaika kwa kupata huduma ya Msaada wa Kisheria mambo mbali mbali yamefanyika ikiwa ni pamoja na kuchapisha na kusambaza nakala za Sheria ya Msaada wa Kisheria kwa lugha nyepesi ili ieleweke na kutumika ipasavyo.

Alieleza kuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu imeendelea na Kazi yake ya msingi ya kuishauri Serikali katika masuala mbali mbali ikiwemo ya Mikataba.

Pia, Tume ya kurekebisha Sheria imeendelea kuzifanyia mapitio Sheria 4 na kufanya Uchambuzi wa matumizi ya Sheria 44 zinazotumika Zanzibar pamoja na kuziweka katika Lugha nyepesi ya Kiswahili ikiwemo Sheria ya ukomo wa Madai ya Mwaka 1917 na Sheria ya Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana ya Mwaka 2007.

Pamoja na hayo, alisema kuwa uratibu wa masuala ya Kidini umeendelea ambapo Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana imeendelea na hatua za kuanzisha Mfuko wa Hijja ambapo matarajio ni kuuzindua katika Mwaka huu wa Fedha.

Aidha, mkakati wa kudhibiti migogoro ndani ya Ndoa na utoaji wa Talaka kiholela unaendelea na sasa matokeo ya utafiti wa ongezeko la Talaka yameanza kutumika katika Semina na utatuzi wa migogoro inayofikishwa katika Ofisi ya Mufti wa Zanzibar.  Aidha, Mafunzo ya muongozo wa kufundishia kwa Walimu wa Vyuo vya Qur-an na Mafunzo kwa Wana ndoa watarajiwa yameendelea kutolewa.

Mapema Katibu Mkuu wa Wizara hiyo George Joseph Kazi akisoma Taarifa ya utekelezaji wa Mpango kazi wa Wizara hiyo alieleza jinsi juhudi zilinavyochukuliwa  katika kuratibu masuala mbali mbali ikiwa ni pamoja na Mafunzo kwa Maafisa Habari kuhusu Uandishi Bora wa Taarifa za Kisheria.

Nao Viongozi wa Wizara hiyo walieleza kuwa katika Uongozi wa Rais Dk. Shein Sekta ya Sheria imepata mafanikio makubwa sana huku wakieleza  mafanikio yalivyopatikana katika Wizara hiyo ikiwa ni pamoja na kupungua kwa ongezeko na migogoro ya Talaka kutokana na Mafunzo yanayotolewa na Ofisi ya Mufti Zanzibar.

Aidha, Viongozi hao walieleza Suala la ushahidi wa Kesi zikiwemo za Ubakaji jinsi zinavyokosa Ushahidi licha ya juhudi kubwa zinazochukuliwa na Mahakama lakini wakati mwengine umakini wa Wananchi katika ushahidi unakosekana.

Pia, Viongozi hao wamepongeza utaratibu huo wa Bangokitita jinsi unavyowasaidia katika kutekeleza Majukumu yao pamoja na hatua wanazozichukua katika suala zima la upatikanaji wa haki.

Wakieleza kuhusu Mfuko wa Hijja, Viongozi hao walieleza kuwa Mfuko huo ukianzishwa utawasaidia sana hasa Vijana Kuhiji mapema ikilinganishwa na hivi sasa ambapo Wananchi wengi husubiri mpaka wapate viinua vyao mgongo na ndipo Wakahiji jambo ambalo hata Serikali itafaidika.

Hata hivyo, Uongozi huo ulieleza kuwa kutokana na Maradhi ya Virusi vya Corona yaliosambaa Duniani Serikali ya Saudia Arabia imezuia Ibada ya Umra lakini Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana imeambiwa matayarisho yote ya Ibada ya Hijja Mwaka huu yaendelee kama kawaida.

NCHI ZA AFRIKA ZIMETAKIWA KUWA NA USIMAMIZI MZURI WA MAWASILIANO KWA LENGO LA KUONGEZA UCHUMI

Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Tanzania Mhandisi Atashasta Nditiye amesema Nchi za Afrika zikiwa na Usimamizi mzuri wa Mawasiliano zitaongeza Uchumi wa Nchi na kupiga hatua kubwa za Maendeleo.

Akizungumza katika Mkutano wa kuwajengea Uwezo Wataalamu wa Mawasiliano kuhusu  Upimaji masafa ya Mawasiliano Mhandisi  Nditiye amesema Sekta hiyo inaweza kuleta mabadiliko makubwa ya Kiuchumi  kwa Mataifa yote .

Akitoa mfano kwa Uchumi wa Tanzania Mhandisi Nditiye amesema Sekta hiyo inaingiza kiasi cha Shilingi Trilioni 77 kwa Mwaka.

Mkurugezi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania TCRA  amesema kutokana  na umuhimu wa Mawasiliano suala la Elimu, Ujuzi na Uweledi linatiliwa mkazo ili kuepusha migogoro ya Matumizi na usimamizi wake.

Mkutano huo umeshirikisha nchi 16 za Afrika na unasimamiwa na Shirika la Kimataifa la Mawasiliano ya simu ITU.

 

TANZANIA ITAKUWA MWENYEJI WA MKUTANO WA WATAALAMU WA NCHI ZA JUMUIYA YA SADC UTAKAOFANYIKA MWEZI HUU

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mh.Jenista Mhagama amesema Tanzania itakuwa Mwenyeji wa Mkutano wa Wataalamu na Wadau wa utatu na Mkutano wa Mawaziri wa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika  SADC utakaofanyika  Mwezi huu Dar es salam.

Amesema Mikutano yote hiyo Miwili itafanyika Dar es salaam kuanzia tarehe 2 hadi 6  ambapo Mgeni Rasmi anategemewa kuwa Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania  Mh .Samia Suluhu Hassan na kuhudhuriwa Mawarizi 16 na Watendaji Wakuu wa Nchi hizo.

Akizungumza na Waandishi wa Habari Mh.Jenistar amewataka Wananchi kutoa Ushirikiano mzuri na Wageni watakaoingia Nchini.

Pia Mh.Jennistar amesema Mh.Samia  atazindua Programu ya Taifa ya Mafunzo kwa Vitendo Mahala pakazi kwa Vijana ambapo itawaendeleza Vijana katika Utamaduni na kupata uzoefu mahala pa kazi  na kuwawezesha Vijana kupata ujasiri wa Kujiajiri wenyewe.

 

Mapema Mkurugenzi msaidizi Idara ya  Ajira Nd.Rorbet Masingiri amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha Vijana wanasifa  na kuweza Kujiajiri katika Taasisi mbali mbali.

Mkutano huo ambao unakauli mbiu ya kukuza Ajira Mahusiano mema sehemu za Kazi kwa Maendeleo endelevu.

 

error: Content is protected !!