Daily Archives: February 22, 2020

Dr.SHEIN AMEZITAKA NCHI WANACHAMA WA JUMUIYA YA SADC KUWA NA MFUMO BORA WA KUKABILIANA NA MAAFA

Rais  wa  Zanzibar  na  Mwenyekti wa  Baraza  la  Mapinduzi  Dr.Ali  Mohamed Shein  amesema  Nchi  Wanachama  wa  Jumuiya  ya  Maendeleo  Kusini  mwa  Afrika  zianapaswa  kuwa   na  Mfumo  bora  wa  pamoja  wa  kukabiliana  na  Maafa  yanayotokana  na  mabadiliko ya  tabia  Nchi.

Ametoa tamko  hilo wakati  akifungua  Mkutano  wa  wa  kwanza  wa   Kamati  ya  Mawaziri  wenye  dhamana  ya  Menejimenti  ya  Maafa  wa  Nchi  za  SADC  katika  Hoteli  ya  Madinatil Bahari  Mbweni  nje  kidogo  ya  Mji  wa  Zanzibar.

Dr .Shein  amesema  Nchi  za  ukanda  wa   SADC   zimekuwa  zikikabiliana  na  majanga  tofauti  ambayo  kwa  kiasi  kikubwa  yamekuwa  yakichangia  kudhoofisha  uchumi wa  Nchi  hizo  na  umasikini kwa  Wananchi  wake  hivyo  kuwa  na  mkakati  na  mfumo  wa  pamoja  ni  jambo  la  lazima  ili  kuzijengea  uwezo  na  kubadilishana  uzoefu  .

Ameyataaja  majanga  ya  ukame, mafuriko, vimbuinga  na  uvamizi wa  wadudu  katika  mazao ya  kilimo kuwa  ni   changamoto  kwa  Nchi  hizo  inayosababisha  fedha  za maendeleo  kutumika  katika  kurejesha  hali  ya kawaida  baada   ya majanga  na  kusimama  kwa miradi  ya  maendeleo.

Akizungumzia  jinsi  Zanzibar  inavyojiiandaa  juu  ya  kukabiliana  na  Maafa  Rais  wa  Zanzibar  amesema  Serikali  imekuwa  ikiendelea  kuimarisha  mkakati wa  kitaifa  wa  kukabilina  na  Maafa  kwa  kuwajengea  uwezo  Wananchi  ikiwemo  ununuzi wa  Boti  za  kisasa  za  uokozi ,  Drones  pamoja  na  kuwa  na   vituo  Rasmi  vya  uokozi.

Akizungumza  katika  Mkutano  huo  Waziri wa  Nchi  Ofisi  ya  Waziri  Mkuu , Sera ,Bunge  na  Watu  Wenye  Ulemavu  Jennista  Mhagama  amesema  kila  Sekta  hapa  Nchini  inapaswa    kuweka  mkazo  katika  uandaaji  wa  Bajeti  inayoyzingati namna  ya  kukabiliana  na  Maafa,

 

KATIBU MTENDAJI WA SADC DKT.STERGOMENA AMEFIKA IKULU ZANZIBAR KWA LENGO LA KUSALIMINA NA DK.SHEIN

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, amesisitiza umuhimu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kushirikiana ili kuyapatia ufumbuzi matatizo mbali mbali yanayoyakabili Nchi za Ukanda huo.

Dk. Shein amesema hayo Ikulu Jijini Zanzibar, alipokutana na Katibu Mtendaji wa (SADC )  Dkt. Stergomena  Lawrence  Tax  aliefika kwa ajili ya kusalimiana nae.

Alisema Nchi Wanachama wa SADC  zinakabiliwa na changamoto mbali mbali zinazofanana, zikiwemo za majanga pamoja na za kiuchumi, hivyo ni vyema zikashirikiana katika  kuzipatia ufumbuzi changamoto hizo.

Akigusia suala la  suala la majanga, Dk. Shein alisema  ni changamoto inayoikabili Dunia nzima, ambapo hutofautiana kulingana na Mazingira ya Kimaeneo.

Alisema kufanyika kwa mkutano wa kwanza wa Kamati ya Mawaziri wenye dhamana ya Menejment ya Maafa kwa Nchi Wanachama wa  SADC ni mwanzo mzuri katika muelekeo wa kuzipatia ufumbuzi baadhi ya changamoto hizo.

Alisema Zanzibar kwa upande wake imeanza kulitafutia ufumbuzi tatizo la kutuwama kwa maji ambalo husababisha majanga, (hususan katika Maeneo ya g’ambo) kwa kujenga Mitaro mikubwa inayopeleka maji moja kwa moja Baharini.

Aidha, Rais Dk. Shein alisema kuna haja kwa Nchi Wanachama wa  SADC kutafakari namna gani zitakavyoshirikiana na kusaidiana katika dhana ya kuimarisha Uchumi wa Nchi zao, kwa kubadilishana uzoefu pamoja na uapatikanaji wa mafunzo.

Alisema kuna umuhimu wa Nchi hizo kubadilishana bidhaa hususan zitokanazo na Kilimo kwa njia ya kuuziana, ikiwa ni hatua itakayopunguza gharama.

Akigusia matumizi ya lugha ya Kiswahili kwa Nchi Wanachama, Dk. Shein alisistiza umuhimu wa Nchi za  SADC kuwa na utaratibu na mikakati ya kuanza matumizi ya Lugha hiyo, na kuipongeza Burundi kwa mafanikio iliyofikia katika matumizi ya Kiswahili.

“ni vyema kila Nchi ikajitayarisha kutumia Kiswahili, lazima ianze kwa maeneo”, alisema.

Aidha, Dk. Shein alibainisha dhamira ya Serikali ya Jamuhuri ya Muungano na ile ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kusimamia Demokrasia Nchini kwa kuzingatia Sheria na Katiba za Nchi.

Mapema, katibu mtendaji wa sadc dkt.  Stergomena lawrence tax, aliishukuru serikali kwa kukubabali kuaanda mkutano huo muhimu, hatua aliyosema inatokana na kutambua mchango mkubwa wa Tanzania katika maendeleo na mustakbali wa Jumuiya hiyo.

Alisema hali ya ulinzi na usalama kwa Nchi Wanachama wa  SADC  ni nzuri mbali na kuwepo kwa matukio mbali mbali yanayojiri kabla na baada ya Uchaguzi.

Alishauri kutiliwa mkazo suala la upatikana wa Ajira kwa Vijana katika Nchi Wanachama ili kuondokana na kadhia mbali mbali zinazojitokeza.

Aidha, Dkt.Lawrence aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, chini ya Uongozi wa Dkt .Shein kwa maendeleo makubwa ya Kiuchumi na Kijamii iliyofikia, hivyo akabainisha azma ya  SADC  ya kuunga mkono juhudi  hizo.

 

 

 

 

 

 

 

MAKAMU WA PILI WA RAIS WA ZANZIBAR BALOZI SEIF AMEJIANDIKISHA KATIKA DAFTAR LA KUDUMU LA WAPIGA KURA

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi tayari ameshajihakiki katika Daftari la kudumu la Wapiga kura kwa mujibu wa Sheria ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar {ZEC} kujiandaa kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika baadae Mwaka huu.

Uhakiki huo ameutekeleza kwenye Kituo chake cha kawaida cha Kupiga Kura kilichopo Skuli ya Sekondari ya Kitope Shehia ya Kitope ndani ya Jimbo la Mahonda Wilaya ya Kaskazini “B” Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Balozi Seif Ali Iddi ambae pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda kupitia Chama cha Mapinduzi {CCM} anayemaliza muda wake wa kuwatumikia Wananchi wa Jimbo hilo  katika Kipindi cha Miaka Mitano tayari ameshatangaza kutogombea tena nafasi hiyo na kuamua kujipumzisha na shughuli za Kisiasa.

Akitoa maoni yake mbele ya vyombo vya Habari mara baada ya kujihakiki kwenye Daftari hilo la  Wapiga Kura Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema bado ipo changamoto kwa baadhi ya Wananchi kwa kutokupata Vitambulisho vyao vipya  vya Mzanzibari Mkaazi vinavyowapa fursa ya kufanya uhakiki kwenye Daftari la Wapiga Kura.

Alisema changamoto hiyo imejionyesha kwa baadhi ya Wananchi kutokuwemo majina yao na wengine kuelezwa Majina yao kuwepo Shehia nyengine mambo yanayoleata usumbufu kwao baada ya kuacha shughuli zao za kila siku za kujitafutia maisha.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inafanya taratibu za kuhakikisha  kwamba kila Mwananchi wa Taifa hili anapata haki yake ya Kidemokrasia ikiwemo ya Kupiga Kura kwa mujibu wa Katiba na Sheria za Nchi zilizopo.

Balozi Seif  aliiagiza Taasisi inayosimamia Vitambulisho wa Mzanzibari kuitafutia ufumbuzi  changamoto hiyo ili kila Mwananchi mwenye haki ya kupiga Kura anatumia nafasi yake.

Akielezea kuridhika kwake na zoezi la Uhakiki wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwenye Kituo chake liloanza Alhamisi na Kumalizia Jumatatu ya Tarehe 24 Mwezi huu Balozi Seif Ali Iddi aliwaomba Wananchi wote waliotimiza Sifa za Kujiandikisha Nchini kuitumia nafasi yao ya Kidemokrasia ili kupata fursa sahihi ya kuwachagua Viongozi wao katika Kipindi cha Miaka Mitano inayofuata.

Alisema si vyema wala si busara kupoteza nafasi yao kizembe inayotumia muda mfupi  kwa sababu ya uvivu na visingizio vya kuzongwa na shughuli nyingi za kujitafutia riziki ambazo upo muda, saa na wakati mwingi zaidi wa kuziendeleza.

Zoezi la Uhakiki wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ndani ya Jimbo la Mahonda limeanza Alhamis ya Tarehe 20 Febuari na kuendelea kwa muda wa Siku Tano hadi Jumatatu ya Tarehe 24 Mwezi huu.

 

 

error: Content is protected !!