Daily Archives: February 16, 2020

WAZIRI ZUNGU AMEAHIDI KUSHUGHULIKIA ATHARI ZA KIMAZINGIRA ZITAKAZO JITOKEZA KWA UNGUJA NA PEMBA.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mh. Mussa Azan Zungu ameahidi kuteua Wataalamu maalum wa masuala ya kimazingira watakaopewa jukumu la kuangalia athari za Mazingira zinazoendelea kujitokeza katika Maeneo tofauti ya Visiwa vya Unguja na Pemba.

Alisema hatua hiyo ikiwa ni Jukumu la Ofisi yake imekuja kuafuatia Maeneo mengi hasa zile Sehemu zilizo Pembezoni mwa Barahi ya Hindi kukumbwa na changamoto mbali mbali za kimazingira ikiwemo mmong’onyoko wa Ardhi.

Mh. Mussa Azan Zungu alitoa ahadi hiyo wakati wa mazungumzo yake na Makamu wa Pili wa Rais wa  Zanzibar  Balozi  Seif  Ali Iddi   Vuga  Mjini  Zanzibar alipofika kujitambulisha rasmi baada ya kuteuliwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania  Dr. John Pombe Magufuli kushika wadhifa huo.

Alisema Visiwa vikubwa na hata vile vidogo ni sehemu muhimu zinazopaswa wakati wote kushughulikiwa na kuangaliwa kwa umakini mkubwa kulingana na maumbile yake ya kuzunguukwa na maji sehemu zote ili kulinda mazingira yake licha ya mabadiliko ya tabia Nchi yanayoikumba Dunia hivi sasa.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira  alimuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba atapanga Ziara maalum ya kuangalia hali ya Mazingira katika maeneo ya Zanzibar kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar inayoratibu na kusimamia mambo yote ya Muungano na mazingira kwa upande wa Zanzibar.

Mh. Zungu aliupongeza Uongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  Dr. Ali Mohamed Shein akisaidiwa na Makamu wake Balozi Seif Ali Iddi kwa usimamizi wao makini wa kuwaletea maendeleo Wananchi wa Visiwa vya Unguja na Pemba.

Naye kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh.Mohamed  Aboud  Mohamed alimpongeza Mwenza wake kwa upande wa Muungano kwa Uteuzi aliopewa na kumuahidi milango iko wazi wakati wote katika kuona Jukumu alilokabidhiwa analisimamia vyema kwa upande wa Zanzibar.

Waziri Aboud alisema yapo mambo mengi yanayoendelea kushirikisha Viongozi wa pande zote mbili za Muungano ambayo Waziri Zungu atapaswa kupewa Ushirikiano wa kina ili kutekeleza jukumu lake hasa vile vikao vya Wataalamu, Watendaji Waandamizi, Mawaziri na  Viongozi wa juu wa pande hizo mbili wanaounda kamati ya pamoja na Muungano.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi  Seif Ali Iddi alisema Zanzibar kwa kiasi kikubwa imefaidika sana na uwepo wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar licha ya Wananchi wa pande hizo mbili kuwa na udugu wa damu kwa Karne nyingi zilizopita kabla ya Muungano huo.

Balozi Seif alimueleza Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira kwamba zipo fursa nyingi zinazoendelea kuwafaidisha  Wananchi wa Zanzibar ndani ya Ardhi yaJamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa upande wa Bara.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alizitaja baadhi ya fursa hizo kuwa ni pamona na Sekta ya Biashara na Ardhi inayowapa nafasi pana Wananchi wa Zanzibar walioamua kuishi Bara kuendeleza shughuli zao za uwekezji katika masuala ya kilimo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais  Muungano na Mazingira Mh. Mussa Azan Zungu alikuwepo Zanzibar kujitambulisha Rasmi baada ya kuteuliwa kushika nafasi hiyo iliyoachwa na Mh. George Simba Chawene aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani.

 

ZOEZI LA UANDIKISHAJI WA WAPIGA KURA WAPYA NA UHAKIKI WA TAARIFA ZA WAPIGA KURA LIMEANZA

Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar imeanza Rasmin kazi ya Uandikishaji wa Wapiga Kura wapya na uhakiki wa Taarifa za Wapiga kura waliokuwemo katika Daftari la kudumu la Wapiga kura Wilaya ya Kaskazini “a”  ambapo Wananchi wa Wilaya hiyo wamejitokeza kwa wingi katika vituo vya kujiandikisha.

Wakizungumza katika Vituo hivyo baadhi ya Wananchi wameipongeza Tume kwa kuandaa mazingira mazuri  huku wakiomba kuongezewa muda ili kila mtu ahakikishe anatumia fursa hiyo.

Mkurugenzi wa Uchaguzi Nd.Thabit  Idarous Faina wakati wakitembelea Vituo hivyo amewataka Wananchi kuutumia vizuri muda uliopangwa na Tume kujiandikisha badala ya kusubiri  kuongezewa muda.

Hata hivyo, Mkurugenzi huyo amesema Tume ya Uchaguzi itamuandikisha kila Mwananchi aliyetimiza sifa za kuandikishwa na kuhakiki Taarifa za Wapiga Kura wote watakaofika Vituoni kwa ajili ya kupata haki yao hiyo ya Kidemokrasia.

Zoezi la Uandikishaji na uhakiki wa taarifa za Wapiga Kura waliokuwemo katika Daftari la kudumu kwa Wilaya ya Kaskazini “a” litaendelea kwa muda Siku tano katika kila  Kituo kilichopangwa na Tume hiyo.

error: Content is protected !!