Daily Archives: February 7, 2020

DK.SHEIN AMEUPONGEZA UAMUZI WA BUSARA KWA ANGOLA KUSHIRIKIANA NA ZANZIBAR KATIKA SEKTA YA UTALII

RAIS  wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameupongeza uwamuzi wa busara na wenye tija wa Angola wa kutaka kushirikiana na Zanzibar kwenye sekta ya utalii hatua ambayo itaimarisha uhusiano wa kihistoria uliopo.

Dk. Shein aliyasema hayo leo, Ikulu Jijini Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na Balozi wa  Angola katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  Sandro Agostinho de Oliveira aliyefika Ikulu kwa ajili ya kujitambulisha kwa Rais.

Rais Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuusifu na kuupongeza uwamuzi huo wa Angola wa kutaka kushirikiana na Zanzibar katika sekta ya utalii na kusisitiza kuwa hatua hiyo ni chachu ya maendeleo kwa pande mbili hizo.

Katika mazungumzo hayo, Dk. Shein alimueleza Balozi Oliveira kuwa Zanzibar na Angola  zina mambo mengi ya kushirikiana kwa pamoja ambayo yanaweza kuleta mafanikio makubwa kwa pande zote mbili yakiwemo mashirikiano katika sekta ya utalii.

Dk. Shein alieleza kuwa  uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo kati ya Zanzibar na Angola ni njia moja wapo kubwa itakayopelekea kuimarika zaidi kwa sekta ya utalii ambapo Zanzibar  imepiga hatua kubwa..

Aidha, Dk. Shein alimueleza Balozi Oliveira kuwa Zanzibar na Angola zote kwa pamoja zina mambo mengi ya kujifunza kwa kila upande ikiwa ni pamoja na namna ya kuendeleza na kuimarisha sekta ya utalii.

Alisema kuwa kwa upande wa  Zanzibar sekta ya utalii ni nguzo kubwa ya uchumi ambayo imekuwa ikichangia kiasi cha asilimia 20 ya Pato la Taifa na asilimia 80 ya fedha za kigeni.

Rais Dk. Shein alisisitiza kuwa mashirikiano katika sekta ya utalii yatazidisha na kuimarisha uhusiano wa kihistoria ulioanzishwa na waasisi wa pande mbili hizo kupitia vyama vyao vya  (CCM) na MPLA.

Dk. Shein aliongeza kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ina mashirikiano makubwa na nchi za Kusini mwa Bara la Afrika kwani iliweza kushirikiana nazo bega kwa bega katika kupigania uhuru ikiwemo Angola, Msumbuji na Afrika Kusini kupitia vyama vyao vya ukombozi vya siasa.

Aliongeza kuwa, kutokana na Angola kupata mafanikio makubwa katika sekta ya mafuta na gesi asilia ipo haja kwa Zanzibar na nchi hiyo kushirikiana kwa pamoja katika kuhakikisha Zanzibar inapanua wigo kwa nchi hiyo ambayo ni ya pili kwa uzalishaji wa mafuta na gesi asilia barani Afrika ikitanguliwa na Nigeria.

Akieleza kuhusu mashirikiano katika sekta ya elimu, Rais Dk. Shein alieleza kuwa ipo haja kwa pande mbili hizo kushirikiana katika sekta ya elimu hasa kupitia vyuo vya nchi hizo kikiwemo Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) katika Kada ya lugha hasa lugha Kireno.

Aidha, Dk. Shein aliongeza kuwa mashirikiano yanaweza kuimarishwa katika sekta hiyo ya elimu, ikiwa ni pamoja na kubadilishana utaalamu na wataalamu hasa katika lugha ya Kireno ambayo itasaidia sana Zanzibar katika kuimarisha sekta ya utalii.

Rais Dk. Shein pia, alitumia fursa hiyo kumpongeza Rais wa Angola Joao Lourenco kwa kazi nzuri anayofanya ya kuiongoza nchi hiyo kwa mafanikio makubwa ambapo hivi sasa uchumi wake unakuwa kwa asilimia 8.4 na kueleza kuwa hayo ni miongoni mwa mambo yaliopelekea ushindi wa kishindo wa kiongozi huyo pamoja na chama chake cha (The People's Movement for the Liberation of Angola) MPLA.

Nae Balozi wa Angola nchini Tanzania Sandro Agostinho de Oliveira alimueleza Dk. Shein kuwa Angola iko tayari kushirikiana na Zanzibar katika sekta ya utalii  hasa ikizingatiwa kwamba Zanzibar imeanza kupata mafanikio na kutajika duniani kote katika sekta hiyo.

Balozi Oliveira alimueleza Rais Dk. Shein kuwa Angola ina mambo mengi ya kujifunza kutoka Zanzibar katika sekta ya utalii, hivyo iko tayari kushirikiana na Zanzibar katika kuimarisha sekta hiyo muhimu ya kukuza uchumi.

Katika maelezo yake Balozi Oliveira alimueleza Dk. Shein, kuwa Angola pia, iko tayari kutoa nafasi za masomo kwa Zanzibar katika Chuo chake kinachotoa mafunzo ya mafuta na gesi asilia ikiwa ni njia moja wapo ya kuendeleza ushirikiano wa kihistoria uliopo.

Alieleza kuwa kutokana na mafanikio makubwa yalioipata nchi yake katika sekta ya mafuta na gesi asilia, Angola iko tayari kushirikiana na Zanzibar katika sekta hiyo.

Sambamba na hayo, Balozi huyo alimueleza Rais Dk. Shein juhudi zinazochukuliwa na nchi yake katika kupambana na rushwa huku akisisitiza kuwa nchi yake itaharakisha mchakato wa  mashirikiano na Zanzibar katika kuendeleza sekta mbali mbali za maendeleo ikiwemo sekta ya utalii, elimu, mafuta na gesi asilia pamoja na kuendeleza utamaduni.

SERIKALI YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR IMEDHAMIRIA KUVIIMARISHA VYUO VYA VIKOSI VYA IDARA MAALUMU ZA SMZ

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imedhamiria kuviimarisha Vyuo vya Mafunzo ya Watendaji wa Vikosi vya Idara Maalumu za  SMZ  ili kutoa Wahitumu wenye ueledi zaidi katika kuvitumikia Vikosi hivyo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais  Tawala za Mikoa Serikali za Mitaa na Idara Maalum Mh.Haji Omar Kheri amesema pia wanaendelea kuipitia upya Mitaala ya Mafunzo ili kuendana na matakwa ya mabadiliko ya utendaji kazi.

Akifunga Mafunzo ya Kijeshi Mkupuo wa 03 Mwaka 2019/2020, iliyoshirikisha Wahitimu Elfu Mbili Mia Tisa 90 amesema Vikosi hivyo ni muhimu katika kutoa huduma kwa Wananchi na kukuza Uchumi Serikali na kukemea baadhi ya Wananchi wanoawahadaa Vijana kuwaingiza katika Vikosi.

Msimamizi Mkuu wa Mafunzo hayo Meja Said Ali Juma Shamhuna amesema Mafunzo hayo ya awali yamehusika na mbinu za Kijeshi na kutoa huduma kwa Jamii.

Wahitimu hao wameiomba Serikali kurekebisha kasoro  zilizopo Makambini na kuahidi kuchangia Mfuko mmoja mmoja wa Saruji kwa ajili ya ukarabati wa Vyuo vya Mafunzo.

Wahitimu hao waliomaliza  Mafunzo ya Kijeshi na kutunukiwa Vyeti  Wanaume ni 2251 na Wanawake 739.

ND. KHAMIS HAJI MKAAZI WA MICHENZANI ASHIKILIWA KWA TUHUMA ZA KUKUSANYA FEDHA KINYUME NA SHERIA.

Mamlaka ya Kupambana na Rushwa naUhujumu Uchumi Zanzibar ZAECA  inamshikilia Nd.Khamis Haji Mussa mkaazi wa Michenzani kwa tuhuma za kukusanya Fedha Vijana ili kuwapatia Ajira katika Taasisi za Serikali.

Afisa Elimu wa Taasisi hiyo amesema kuwa  Mzee huyo mwenye umri wa Miaka 62 amekamatwa akiwa na vielelezo vya Vyeti  vya kumalizia Masomo,  vya Kuzaliwa na vitambulisho vyaMzanzibar vya Vijana na Fedha na  Vijana 14 ambapo kila mmoja alitakiwa kutoa Shilingi Laki Mbili.

Amewaambia  Waandishi wa  Habari kuwa wamefanikiwa kumkamata katika mtego maalum waliouweka ZAECA  ambapo makosa yote anatuhumiwa ni kinyume na kifungu cha 42 na 43 cha Sheria namba 1 ya Mwaka 2012 ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi.

Mapema akifunga Mafunzo kwa Askari wa Vikosi Maalum vya Idara za  SMZ  Waziri Haji Omar Kheri amekemea tabia ya baadhi ya Wananchi wanoawahadaa Vijana na kuwaibia Pesa kwa madai ya kuwapaia Aijira katika Serikali ikiwemo  katika Vikosi hivyo.

SERIKALI YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR ITAENDELEA KUHAKIKISHA USTAWI WA WAZEE NCHINI UNAIMARISHWA

Waziri wa kazi uwezeshaji Wazee Wanawake na Watoto Dk Modline Castico amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kuweka mifumo ya kisera na kisheria ili kuhakikisha Ustawi wa Wazee Nchini unaimarishwa.

Amesema miongoni mwa juhudi hizo ni pamoja na  kuhakikisha  mpango wa kuwalipa Wazee Pencheni Jamii unakuwa endelevu kwa kuwekewa masharti bora kupitia Sheria hiyo.

Akiwasilisha mswada wa Sheria ya kuweka masharti yanayohusiana na haki na huduma za Ustawi wa Wazee, na kuanzisha mpango wa Pencheni Jamii amefahamisha kuwa Sheria hiyo inaanzishwa ili kuwawezesha Wazee kuwa na haki ya kutambuliwa pamoja na kushirikishwa katika huduma za Kijamii ikiwemo Afya Usafiri na Michezo.

Wakichangia mswada huo Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wameiomba Serikali kuweka muongozo wa Wazee kuhusu huduma za Usafiri ikiwa ni pamoja na kulipa nusu nauli.

Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wameupitisha Mswaada huo.

error: Content is protected !!