Daily Archives: January 31, 2020

ZANZIBAR IMESHAJIPANGA KUKABILIANA NA VIRUSI VYA CORONA

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara inayosimamia Masuala ya Afya Zanzibar imeshajipanga kukabiliana na Virusi hatari vya Corona vinavyosababisha Homa Kali inayoambatana na Mafua vikiwa vimeibuka hivi karibuni Nchini Jamuhuri ya Watu wa China.

Hatua hiyo ya Serikali imechukuliwa kufuatia zaidi ya Mataifa Kumi Ulimwenguni kuthibitisha kutokea kwa kesi za maambukizi ya Virusi vya Corona ambavyo hadi sasa ni China pekee ndio iliyoripotiwa kupata wahanga wa maradhi hao.

Timu ya Wizara ya Afya Zanzibar ikiongozwa na Katibu Mkuu wake Bibi Asha Ali Abdulla ilitoataarifa hiyo kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi mara baada ya kumaliza mazungumzo yao na Madaktari Bingwa wa Taasisi ya kuhudumia Maradhi ya Moyo kwa Watoto {SACH} kutoka Nchini Israel.

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja Dr. Ali  Salum Ali alisema Kamati ya Majanga kupitia Kitengo Maalum kilichoanzishwa inamalizia matayarisho kujiandaa na kazi hiyo baada ya kupata nyenzo kutoka Shirika la Afya Ulimwenguni {WHO}.

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Afya Bibi Asha Ali Abdulla alisema kinachozingatiwa zaidi kwa wakati huu ni kwa Wataalamu wa Afya kujipanga katika kutoa Elimu itakayowasaidia Wananchi kujiweka tayari kukabiliana na Virusi vya  Corona.

Katibu Mkuu Asha alisema wakati jitihada hizo zikiendelea Taasisi, Mashirika, Jumuiya za Kiraia pamoja na Wadau wakubwa Wananchi wanapaswa kubeba jukumu katika kuhakikisha suala la utunzaji wa mazingira ndio jibu la kwanza la kujiepusha na maambukizi ya maradhi mbali mbali yanayoikumba Jamii.

Virusi vya Corona viligundulika kwa mara ya kwanza mwezi Septemba Mwaka 2012 huko Saudi Arabia katika nchi za Mashariki ya kati na kuendelea  kusambaa Ugonjwa huo katika nchi za Mashariki ya kati ikiwemo Jordan, Qatar, na Falme za Kiarabu (UAE).

Akizungumza na Madaktari Bingwa kutoka Taasisi ya kuhudumia Maradhi ya Moyo kwa Watoto {SACH} kutoka Nchini Israel Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema mfumo wa Wataalamu hao kuja Nchini kutoa huduma za Matibabu ya Moyo unatoa fursa kwa wagonjwa wengi kupata huduma hiyo muhimu.

Balozi Seif alisema Wananchi wengi hasa wale wenye kipato cha chini wamefaidika na Mfumo huo kwa kupunguza gharama za Matibabu ya kuwapeleka Nje ya Nchi Wagonjwa wao tokea kuasisiwa kwa Mpango huo ulioanzishwa mwishoni mwa Miaka ya Tisini.

Mapema Kiongozi wa Taasisi ya kuhudumia Maradhi ya Moyo kwa Watoto {SACH} Kutoka Nchini Israel Dr. Mara Chapira alisema Timu yake  inatarajiwa kuwafanyia Uchunguzi Watoto wapatao 400 katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja ambao wanasumbuliwa na Maradhi ya Moyo ndani ya Siku Tano za uwepo wao Zanzibar.

Dr. Chapira alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  kwamba wale Watoto watakaobainika kuwa na sababu za kufanyiwa huduma za Upasuaji utaratibu wa kuwasafirisha Nchini Israel utapangwa kama ilivyokuwa vipindi vilivyopita.

Mwishoni mwa Mwaka 2012 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alibahatika kuwatembelea Watoto wa Zanzibar waliliopata huduma za Upasuaji wa Maradhi ya Moyo kwenye Hospitali ya Rufaa ya Taasisi ya Magonjwa ya Moyo ya Sach iliyopo Mjini Tela Vive Nchini Israel.

Wasimamizi wa Wagonjwa hao kutoka Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja walielezea faraja yao kutokana na huduma walizopatiwa Wagonjwa wao baada ya kusumbuliuwa na maradhi ya Moyo wa muda mrefu.

 

 

BIDHAA ZENYE THAMANI YA SHILINGI MILION 27 ZIMETEKETEZWA NA TAASISI YA VIWANGO ZANZIBAR ZBS

Bidhaa zenye Thamani ya Shilingi Milion 27 zimeteketezwa na Taasisi ya Viwango Zanzibar  ZBS  baada ya kubainika kuingizwa Nchini zikiwa hazina kiwango kwa matumizi ya Binaadam.

Wakitoa Taarifa katika uteketezaji Mkuu wa Ukaguzi na udhibiti wa ubora Nd. Suleiman Abdallah na Afisa Uhusiano Nd.Umulkulthum Hamza kutoka Taasisi hiyo wamesma baada ya kufanyiwa Uchunguzi bidhaa hizo zimeonekana kuwa ni hatari kwa Usalama wa Afya ya mtumiaji.

Wameeleza kuwa ni vyema Wafanyabiashara kuwa makini wanapoingiza bidhaa Nchini na kuhakikisha kuwa ni salama kwa afya ya mtumiaji.

Afisa kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA Nd. Omar Khamis amesema hakuna Mfanya biashara yoyote anaelipishwa Kodi kabla ya kuhakikiwa mzigo wake unapofika Bandarini na kuangaliwa Kiwango na ubora wake.

Uteketezaji huo umefanyika katika eneo la Kibele Mkoa wa Kusini ambapo Bidhaa zikizoteketezwa ni pamoja na Paket 348 za Pempas, Juice Katuni 405 na Tende Boxi 17.

WANAFUNZI WANASTAHIKI KUPEWA ELIMU YA KUELEWA SEKTA MUHIMU NCHINI ZINAVYOENDESHA KAZI ZAKE

Wanafunzi wanastahiki kupewa elimu ya kuelewa Sekta muhimu Nchini zinavyoendesha kazi zake kwa vile wao ndio watendaji katika Taasisi hizo kwa siku zijazo.

Wakitoa  Elimu kwa Wanafunzi wa Sekondari wa Skuli ya Uzi Maafisa kutoka Bodi ya Mapato Zanzibar  ZRB juu ya kazi zinazofanywa na Bodi hiyo wamesema Wanafunzi kufahamu Majukumu ya Taasisi hiyo inayokusanya Mapato ya Zanzibar itawasaidia kuamsha ari ya kusoma na pia kuisambaza Elimu hiyo kwa Jamii ambayo itaisadia Bodi hiyo kuwarahisisha kazi zao.

Wanafunzi waliopata Elimu hiyo wamefarijika na kuongeza kuwa watakuwa ni Mabalozi Wazuri kwa Wenzao na Jamii iliyowazunguka juu ya Majukumu ya ZRB ya kukusanya Mapato kwa manufaa ya Taifa kwa ujumla.

error: Content is protected !!