Daily Archives: January 30, 2020

BALOZI SEIF AMEWATAKA WAWEKEZAJI WA TANZANIA NA UTURUKI KUSHIRIKIANA KATIKA MIRADI YA KIUCHUMI

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema wawekezaji wa Tanzania na Uturuki wanapaswa kuutumia uhusiano uliopo wa pande hizo mbili kushirikiana katika kuwekeza Miradi ya Kiuchumi.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na ujumbe wa Viongozi Waandamizi wa Kampuni za Kimataifa za Gökyol na Dayk kutoka Nchini Uturuki waliofika Nchini Tanzania kuangalia maeneo wanayoweza kuwekeza katika nyanja ya miundombinu ya ujenzi.

Alisema Mataifa mengi ulimwenguni yamekuwa na uhusiano wa Kidiplomasia kwa miaka mingi baada ya uhuru ambapo kwa sasa uhusiano huo unastahiki kuelekezwa zaidi kwenye Diplomasia ya Kiuchumi itakayoweza kusaidia kustawisha maisha na maendeleo ya Wananchi walio wengi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliushauri Uongozi wa Kampuni hiyo kutenga muda mahsusi utakaowapata wasaa mpana zaidi wa kuangalia maeneo yanayostahiki kuwekezwa na Kampuni yao iliyoanza kuonyesha  Azma ya kutaka kutumia fursa zilizopo Nchini Tanzania.

Alisema Zanzibar na Tanzania kwa ujumla zimekuwa na maeneo mengi yenya ushawishi wa kuimarishwa miundombinu yake hasa katika Sekta ya Ujenzi na Mawasiliano yenye kuchukuwa nafasi kubwa ya ukuzaji Uchumi wake kupitia bidhaa zinazotokana na Sekta ya Kilimo zinazostahiki kuingia katika Soko.

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Zanzibar Nd. Mustafa Aboud Jumbe alisema zipo bara bara zisizopungua 11 katika maeneo mbali mbali ya visiwa vya unguja na pemba ambazo tayari zimeshafanyiwa uchambuzi yakinifu zikisubiri fedha kwa ajili ya ujenzi wake.

Nd. Mustafa aliueleza ujumbe huo wa Viongozi Waandamizi wa Kampuni ya Kimataifa ya Dayk kutoka Nchini Uturuki kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara hiyo iko tayari kushirikiana na  wadau wa maendeleo katika kuona Bara Bara hizo zenye urefu wa kilomita 150 zinajengwa na kutoa huduma nzuri.

Kwa upande wa Sekta ya Usafiri wa Baharini, Nd. Mustafa alisema jitihada zinaendelea kuchukuliwa na serikali katika kutafuta mbinu za kuipanua Bandari kuu ya Malindi ili iwe na uwezo wa kutoa huduma kwa Meli kubwa za Mizigo zaidi ya moja kwa wakati mmoja.

Mapema Viongozi hao Waandamizi wa Kampuni za Kimataifa za Gökyol na Dayk kutoka Nchini Uturuki walisema Kampuni zao zilizoasisiwa tokea miaka ya 1961 na 1971 zina uzoefu wa kimataifa katika Ujenzi wa Miundombinu ya Bara Bara kuu {Highway} pamoja na majengo ya Hospitali na Skuli.

Walisema Wahandisi wa Kampuni hizo waliobobea  hutekeleza Majukumu yao yanayokwenda sambamba na kushiriki katika Shughuli za Kijamii katika maeneo na Nchi wanazopata fursa za kushiriki katika Miradi Mikubwa ya Kimataifa.

WIZARA YA ARDHI IMEFANIKIWA KUPUNGUZA GHARAMA ZA USAMBAZAJI WA UMEME KWA WANANCHI

 

Wizara ya Ardhi Nyumba Maji na Nishati imesema imefanikiwa kupunguza gharama za usambazaji na kurahisisha upatikanaji wa huduma Nishati ya Umeme kwa Wananchi Mjini na Vijijini.

Hatua hiyo imeelezwa kufikiwa kupitia utekelezaji wa mradi wa miaka minne wa kusaidia upatikanaji wa nishati hiyo Zanzibar uliogharimu zaidi ya Shilingi Biloni 12 zilzotolewa na Serikali ya Sweeden.

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Mh. Ali Khalil Mirza akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo amesema pia umewajengea uwezo watendaji wanaosimamia na kutoa huduma ya nishati ya umeme pamoja na  kununua vifaa vya kisasa ikiwemo mita.

Akizungumza kikao cha tathimni ya mradi huo kulichohusisha Wizara ya Ardhi Nyumba Maji na Nishati na ujumbe kutoka Sweeden ameongeza pia imepitia Sera ya Nishati na kufanya tafiti za kuanzishwa Umeme wa kutumia Nishati mbadala Zanzibar na kupunguza utegemezi wa Nishati ya Umeme kutoka Tanzania Bara.

Balozi wa Sweeden Nchini TanzaniaNd. Anders Joberg aliongoza ujumbe huo amesema itaendelea kushirikiana na  Zanzibar katika kuimarisha upatikanaji wa uhakika wa Nishati ya Umeme kwa vile ndio msingi Mkuu wa kuharakisha maendeleo ya Uchumi wa Nchi.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Matumizi ya Nishati Zanzibar (ZURA) Nd. Haji Kali Haji amesema katika kuendeleza mikakati ya upatikanaji wa huduma bora ya Umeme Zanzibar wameanza ukaguzi wa Transoforma zilizowekwa katika maeneo mbalimbali na kutoa maelekezo kwa Shirika la Umeme Zanzibar ZECO wanapobaini kasoro.

error: Content is protected !!